Kwenye kitabu chake cha Jobs Ends, milionea kijana Taylor Pearson anaandika, ‘Kwa enzi hizi za matumizi makubwa ya mashine na intaneti, ajira yako ni kitu kinachoweza kupotea kufumba na kufumbua, kwa hiyo ujasiriamali ni salama zaidi ya ajira.’
Na mimi nasema ‘katika enzi hizi za matumizi makubwa ya mashine na intaneti na siasa chafu za Kiafrika, hakuna usalama katika ajira wala ujasiriamali. Kama ambavyo unaweza ukaamka ukaambiwa kampuni iliyokuajiri inapunguza wafanyakazi, ndivyo ambavyo unaweza ukaamka ukaambiwa Serikali imepiga marufuku uuzwaji wa nguo za mitumba, wakati huo wewe una shehena ya mashati ya mitumba stoo’
Ninachojaribu kukwambia ni siku yoyote unaweza kuwa huna chimbo la kupata pesa tena. Na mwanaume bila pesa ni mwanaume suruali. Na hili sio mpaka uambiwe, hapana! Litaanzia kwako mwenyewe, taratibu utaanza kujiona unapoteza ‘hamu’ ya kuwa mwanaume.
Sasa kila mwanaume anajua cha kufanya asipokuwa na kazi ambacho ni kimoja tu kutafuta kazi nyingine, lakini wengi hatujui nini hatutakiwi kufanya tusipokuwa na kazi, na leo ndiyo tutazungumzia hicho.
Hata kama huna mahali pa maana pa kwenda, hakikisha haukai nyumbani kabisa. Amka asubuhi, toka nenda zako hata Ubungo pale simama, angalia jinsi fly-over za Magufuli zinavyotengenezwa siku nzima, ikifika jioni rudi nyumbani kama umetokea ofisini vile.
Pia Soma
- ANTI BETTIE: Sifikirii kuachana naye, tabia zake zinanilazimisha
- USHAURI WA DAKTARI: Hawa wasifanye hivi kipindi cha corona
- ANTI BETTIE: Mwaka wa nne sasa sijaonana naye, ila bado anasisitiza nivumilie
Usiwe na mtazamo hasi
Mwanaume ukiwa huna hela, huna kazi, uko nyumbani tu, unakuwa kama kamusi, kila neno litakalosemwa wewe una tafsiri yake. Mkeo akisema baba Rashidi naomba muangalie mtoto mara moja niende dukani… Wewe utasikia kasema ‘baba Rashidi, kwa sababu huna hela na huna kazi umekaa hapa siku nzima unapoteza muda kwa kuangalia TV utadhani unalipwa, sasa kaa na mtoto mimi naenda dukani kununua cha kupika ili nipike ule, ujaze hilo tumbo, upate nguvu ya kushika rimoti na kuendelea kubadilisha chaneli na kupoteza muda zaidi.’
Kuanzia hapo utamjibu vibaya, atakujibu vibaya pia, mtajibizana matokeo yake hakuna hata kitakachopikika. Kwa hiyo ili usifike huku ni vyema sana kujitahidi kutokuwa na mtazamo hasi kuhusu mkeo. Yaani usiwe na mtazamo hasi kiasi kwamba hata akisema jambo baya kukuhusu wewe lichukulie chanya.
Usione kila kitu sawa
Kwa sasa huna kazi labda huna hela pia kwa hiyo lazima kuna vitu havitaenda kama kawaida nyumbani hili ni jambo la la kutegemea. Kitu ambacho hutakiwi kufanya wakati huu ni kuigiza kwamba kila kitu kiko sawa. Inuka changamsha ubongo kurekebisha mambo nyumbani.