Katika kujiajiri kupitia mitandao ya kijamii, mtu anaweza kujitengenezea soko lake mwenyewe. Jack Ma ni moja ya tajiri mkubwa duniani kutokea China, Februari 1999 wakati Kampuni ya Alibaba imetoka kuanzishwa, aliwaambia wafanyakazi wenzake kuwa ni lazima waifanye kampuni hiyo ya kimataifa.
Alisema hivyo kwa kuwa walijua namna ya kulifikia soko la kimataifa hasa kwa kutumia nguvu ya mitandao na intaneti.
Leo hii tunapozungumzia Alibaba, ni moja ya duka kubwa mtandaoni (online store) linaloshindana na kampuni kubwa duniani kama Amazon.
Wenzetu Wazungu na Wachina wametambua thamani na umuhimu wa intaneti na mitandao na kuendesha biashara zao katika mfumo na teknolojia hiyo na hatimaye kutengenezea soko la uhakika katika biashara zao duniani.
Hivyo basi hata sisi tunaoingia katika biashara au ujasiriamali hatuna budi kuziingiza biashara zetu katika mifumo na teknolojia ya kisasa ili kukidhi na kulifikia soko la ndani na nje ya nchi ubora na viwango vya hali ya juu kimataifa katika huduma na bidhaa zetu.
Hivyo, kama umeamua kujiajiri kwa kuanzisha biashara, kazi au huduma yako, lazima uwe una mawazo ya kuja kuifanya kuwa ya kimataifa.
Ikiwa kama mfanyabiashara au mjasiriamali mdogo hutaanza kwa kufikiri katika mfumo huo hutafanya bidii ya hali ya juu ili iweze kuwa bora kuliko kawaida na baadaye kuwa na mguso mkubwa ulimwenguni.
Bahati mbaya sana katika ulimwengu huu wa kidigitali ambao wengi wanasema enzi za ushindani mkuu ni lazima kuwa na ubora wa viwango vya kimataifa hata kama unataka kuuza bidhaa yako mtaa wa pili au kijijini. Watanzania wanaingia sokoni na bidhaa au huduma hafifu sana. Ndugu zangu ni muhimu kutambua kuwa kazi yako au bidhaa yako inaacha alama na kukutambulisha kila sehemu uendayo.
Kumbuka kuwa kazi nzuri ni utambulisho mzuri na wakati kazi mbaya inakupa sifa mbaya. Kwa msingi huo Elimika Ung’are tumejidhatiti kuhakikisha tunawasaidia na kuhamasisha watu wote katika jamii nchini walioamua kujiajiri kwa kuwapa mbinu na miongozo inayoweza kuwasaidia na kufanya shughuli zote za kiuchumi.
Kwa elimu ya biashara, ujasiriamali na kilimo biashara fuatilia kupitia kurasa zetu; Facebook, Instagram na Twitter kwa jina la Elimika Ung’are.