Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TIMUA VUMBI : Hili la Kabwili liachwe kwenye vyombo vya dola

93754 Kabwili1+pic TIMUA VUMBI : Hili la Kabwili liachwe kwenye vyombo vya dola

Fri, 31 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

MAPEMA wiki hii kipa wa Yanga, Ramadhan Kabwili amesikika akielezea tuhuma za upangaji matokeo msimu uliopita ambazo zinahusisha uongozi wa klabu ya Simba.

Kabwili aliweka wazi tuhuma hizo kwenye chombo cha habari alipohojiwa ambapo alisema viongozi wa Simba walimshawishi kumpa gari aina ya IST mpya ili acheze vibaya na kupewa kadi ya njano katika mechi yao, Yanga na JKT Tanzania msimu uliopita.

Hiyo ilikuwa ina maana kwamba kipa huyo endapo angekubaliana na ushawishi huo kama ni kweli basi angefanya kama vile alivyoshawishiwa ili azawadiwe kadi hiyo na kufikisha idadi ya kadi tatu za njano kwani tayari alikuwa na kadi mbili.

Imeelezwa mechi ambayo Kabwili angeikosa endapo angefanya jambo hilo ni dhidi ya watani hao, Simba na Yanga ya msimu uliopita ambapo golini angesimama Klaus Kindoki raia wa DR Congo ambaye kwao huenda waliona ni rahisi kumfunga kuliko Kabwili.

Ni tuhuma nzito katika soka la hapa nchini na hata ingetokea nchi nyingine kwa sababu vitendo vya upangaji matokeo haviruhusiwi na ni kosa kubwa ambalo husababishahata watu kufungiwa kucheza ama kuongoza soka kwa maisha yao yote.

Tuhuma kama hizo ziliwahi kutokea miaka ya nyuma kwa baadhi ya wachezaji ambao wengi wao walihusishwa na klabu ya Simba akiwemo Ulimboka Mwakingwe, akituhumiwa kutumwa kumpelekea pesa mlinda mlango Shaban Kado wa Mtibwa Sugar - tukio lililodaiwa kutokea mwaka 2010.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Ukiachana na hilo, kuliibuka tuhuma zingine za upangaji matokeo kwa waliokuwa wachezaji wa Azam, Deogratius Munishi, Saidi Morad na Agrey Morris ambao pia walituhumiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Simba katika moja ya mechi za Ligi Kuu ikidaiwa kuwapo nia ya kupanga matokeo.

Jambo hilo liliwafanya viongozi wa Azam kuchukua hatua ya kuwasimamisha nyota wao.

Imeshuhudiwa mara kadhaa Shirikisho la Soka nchini (TFF) likitoa adhabu kwa viongozi mbalimbali wanaojihusisha na matukio kama hayo kwenye soka, hasa pale wanapobaini ukweli hiyo yote ni kuondoa taswira mbovu kwenye soka kwa watu ambao hawalitakii mema soka la Tanzania.

Hatua ambayo Sekretarieti ya TFF imeifanya ni kuiandikia barua Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo ili kufuatilia tuhuma hizo kwa undani na kuweka nia ya kuvijulisha vyombo vya dola ili visaidie kwenye uchunguzi kubaini ukweli na hatua stahiki zichukuliwe.

Simba ambao ni watuhumiwa wametoa taarifa ya kupinga vikali tuhuma hizo na kusisitiza kuwa TFF imefanya uamuzi sahihi kuingilia kati suala hilo katika uchunguzi ili kubaini ukweli, kwani hata kwao ni tuhuma ambazo hazileti afya kwa klabu yao.

Tuhuma hizo ni nzito, hata kama ni mambo yaliyotokea muda mrefu kidogo, lakini siyo ya kufumbia macho ni lazima ibainike nini kilitokea kupitia mchezaji huyo ambaye anafahamu ukweli ni upi.

Kabwili pekee ndiye anayeweza kusaidia vyombo vyote vitakavyochunguza tuhuma zake kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa, kwani anafahamu ukweli na kiongozi aliyekuwa akimpigia simu juu ya hilo.

Nadhani huu ni wakati wa wadau wa soka na michezo kwa ujumla kutulia na kusubiri ukweli baada ya vyombo husika kufanya kazi yake.

Hii ni kwa sababu ishu kama hii si rahisi tu kwa mtu mmoja kuifanya kwani inalazimika taasisi husika kuingia na kufanya kazi ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Takukuru hawashindwi kitu kwenye mambo yanayohusiana na rushwa, hivyo ni suala la muda tu kubaini ukweli juu ya tuhuma hizo na mhusika aliyekuwa akimpigia simu Kabwili kumrubuni juu ya hilo na kumhonga hilo gari aina ya IST.

Kupata ukweli wa hili kunahitaji muda, na si kama linavyojadiliwa kwenye mitandao na vijiwe vya kahawa, hili ni jambo zito pande zote aliyetaka kuhongwa na mhongaji. Ukweli ukijulikana kutoka mamlaka husika basi hatua zinazostahiki zitachukuliwa kulingana na tuhuma jinsi ilivyo.

Tanzania inahitaji kusonga mbele kisoka kama ilivyo mataifa mengine yaliyoendelea kisoka hivyo kuna haja sasa ya viongozi wa mpira hasa TFF kuwa makini na watu wenye nia ya kurudisha nyuma soka.

Columnist: mwananchi.co.tz