Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TANZIA: Kwa nini namlilia Sharifa Hussein Kalala

97696 PIC+johari TANZIA: Kwa nini namlilia Sharifa Hussein Kalala

Mon, 2 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ilikuwa Ijumaa Februari 21, 2020 takriban saa 4:00 usiku kwa saa za Malaysia, wakati Balozi AshaRose Shaaban Mtengeti-Migiro aliponipigia simu kutaka kuzungumza nami kuhusu mambo mawili. La kwanza lilikuwa la kiofisi lakini la pili ilikuwa kunipa taarifa kuwa Sharifa Hussein Kalala anaumwa na hali yake ni mbaya. Kwa maneno yake Balozi Migiro, “kilichobaki ni Rehma ya Mwenyezi Mungu”.

Kwa hakika nilihuzunika na kushtuka sana. Nilihuzunika kwa sababu namfahamu Sharifa kwa zaidi ya robo karne. Lakini nilishituka kwa sababu Alhamisi ya Februari 13, 2020, nilimtumia Mzee Yusuf Kalala (mume wa marehemu Sharifa) ujumbe mfupi wa simu (sms) kumuarifu kuwa Mzee Iddi Simba amefariki dunia.

Mzee Kalala alinijibu kwa ufupi akisema “Innallillah Wainnaillahi Raajiuun” kisha akaniarifu kuwa yupo Uwanja wa ndege wa Zurich akielekea Marekani, kwa sababu Sharifa anaumwa.

Haikunijia kabisa kuwa hali yake ilikuwa mbaya hadi aliponipigia simu Balozi Migiro siku moja tu kabla ya Sharifa kufikwa na umauti. Kwa huzuni kubwa, nilipoamka asubuhi ya Jumamosi Februari 22, nikakuta ujumbe wa simu uliotumwa kadri ya saa tatu zilizopita kuniarifu kuwa Sharifa Hussien Kalala amefariki dunia!

Nimewahi kusema mara kadhaa kuwa kuandika tanzia ni jambo zito hasa inapohusu mtu unayemfahamu sana. Mara zote niandikapo tanzia hutamani sana kuwa hiyo iwe ndiyo ya mwisho lakini hii ni ya saba, hujikuta nabakiwa na majonzi kwa siku kadhaa baada ya kuichapisha kwa sababu kila inaposomwa, baadhi ya wasomaji hunipigia simu au kunitumia ujumbe kueleza hisia zao.

Jambo hili huwa linavuta hisia zangu na inakuwa kana kwamba msiba ule ndio kwanza umetokea; ni sawa na kutonesha kidonda. Hivyo basi, kwa kila tanzia niliyoandika msiba kwangu huwa haumaliziki mapema. Kutokana na sababu hii, mara hii niliamua nisiandike chochote kuhusu Sharifa. Hata hivyo, nafsi yangu inanisuta kuacha kuandika kutokana na ukaribu wangu na familia ya Mzee Yusuf Kalala.

Pia Soma

Advertisement
Ndipo leo ikiwa ni siku ya tano tangu afariki, nilipoamua nibadili uamuzi wangu kwa sababu ningekuwa sikumtendea haki. Katika mazingira haya, ni bora kwangu mimi kuendelea kuwa na majonzi kwa siku kadhaa baada ya kusomwa tanzia hii, kuliko kuacha kuandika machache kati ya mema yake mengi aliyowafanyia binadamu wenziwe.

Nimemfahamu Sharifa tokea miaka ya 1990 wakati nilipokuwa Mkurugenzi wa Masoko ndani ya iliyokuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA). Kipindi hicho nilikuwa nasafiri mara kwa mara kwenda Marekani kikazi na wakati huo Bi Sharifa na mumewe Mzee Yusuf Kalala walikuwa wanafanya kazi Washington DC.

Katika kumbukumbu zangu, mara zote nilipokwenda Washington DC ziara yangu inakuwa haikamiliki bila kufika nyumbani kwa Mzee Kalala.

Mara kadhaa Mzee Kalala mwenyewe alikuwa ananifuata Baltimore Washington International (BWI) au International Airport Dulles (IAD), viwanja vya ndege vinavyotumiwa sana na abiria wa Washington.

Marehemu Sharifa pamoja na mumewe Mzee Kalala, watu wenye ukarimu usio na kifani. Nyumba yao ilikuwa nyumba ya Watanzania ambayo milango yake ilikuwa wazi muda wote kwa watu wa aina zote. Kama zilivyo familia nyingi za Marekani, ya kwao pia haikuwa na mtumishi wa ndani. Mkewe, Sharifa alikuwa anafanya kazi Benki ya Dunia na akirudi nyumbani jioni anakuta kundi la wageni nyumbani kwake.

Bila kujali uchovu, Sharifa aliwapokea kwa bashasha na kuingia jikoni kuanza kupikia wageni. Wakati mwingine, mara tu baada ya kumaliza kula, kundi lingine la wageni huwa linaingia na anaingia tena jikoni. Hayo yalikuwa ni maisha yao ya kila siku. Alikuwa akiyafanya hayo kwa furaha ambayo ilidhihiri kwa watu wote kiasi cha kuwafanya wajione wapo nyumbani.

Yapo mengi sana mazuri ambayo Sharifa na mumewe Mzee Kalala wameyafanya katika kusaidia jamii ya Watanzania. Nakumbuka katikati ya miaka ya 1990 walianzisha utaratibu wa kuwasaidia vijana wa Kitanzania kwenda kusoma Marekani. Chini ya mpango huo, vijana hao walikuwa wanakwenda kuanza masomo kwenye Community Colleges kwa sababu ada ya masomo zilikuwa chini ukilinganisha na ada za vyuo vikuu.

Walipofika Marekani, vijana hao walikuwa wanafikia kwenye nyumba ya Sharifa na Mzee Kalala hadi watakapoweza kujikimu na kupata makazi yao ya kudumu. Vijana wengi wamenufaika na mpango huu na wamesoma hadi kupata shahada huko Marekani. Baadhi yao wamerudi nyumbani na wengine hadi leo wanaishi Marekani na wanafanya kazi kwenye kampuni kubwa. Ni watu wa fani mbalimbali kama vile uhasibu, uhandisi, uanasheria na nyingine kadha wa kadha. Baadhi yao leo wanamiliki kampuni zao binafsi Marekani na zinafanya vizuri. Msingi wa yote haya ni mapenzi na ukarimu uliooneshwa na marehemu Sharifa na mumewe Mzee Kalala.

Miongoni mwa sifa zake kubwa Sharifa ni kutokuwa na kinyongo na mtu hata pale ambapo alikosewa. Nakumbuka vyema Januari 2001 pale kijana mmoja alikwenda Marekani na kama ilivyokuwa kwa wengi waliotangulia kabla yake, naye alifikia nyumbani kwa Sharifa.

Baada ya miezi minne, kijana yule akapata marafiki Uingereza ambao walimshawishi aende huko kwa kuambiwa kuwa kuna fursa nyingi zaidi kuliko Marekani.

Kijana yule aliondoka bila kuwaaga wenyeji wake, hivyo kusababisha taharuki pale waliporejea nyumbani na kukuta kijana hayupo.

Siku ya pili tu baada ya kuondoka Marekani, nilipata taarifa kuwa yule kijana amehamia Uingereza na ameondoka bila kuaga. Nilimpigia simu Sharifa na kumtaka radhi kwa yaliyotokea. Jibu lake lilinituliza sana moyo wangu na kuona kuwa alikuwa na moyo wa pekee kabisa. Kwa kifupi tu aliniambia “Bwana Dau, fulani (kamtaja jina) ni kijana mdogo sana. Amefanya makosa na katika maisha yake ataendelea kufanya makosa. Wajibu wetu sisi kama wazazi ni kumsamehe na kumuongoza, haifai kabisa kumkasirikia”. Huyo ndo alikuwa Sharifa!

Binafsi nimeumizwa na msiba huu kwa sababu Sharifa alikuwa mzungumzaji wangu. Kila nilipokwenda Marekani ilikuwa lazima nifike nyumbani kwao kuwatembelea na mara nyingi hulala hapo.

Mke wangu ameshakwenda Marekani mara kadhaa na zote amefikia nyumbani kwa Sharifa. Walipoamua kurejea Tanzania zaidi ya miaka 10 iliyopita, mara nyingi tumekuwa tukitembeleana. Pamoja na ukarimu wake, Sharifa atakumbukwa kwa ucheshi wake usio kifani.

Katika mazungumzo yetu, mara kwa mara nilikuwa nikimtania kuwa amruhusu mumewe aoe mke wa pili ili bi mdogo amsaidie kazi ya kumlea Mzee Kalala. Kwa kusisitiza suala hili, nilikuwa namkumbusha ule wimbo maarufu wa taarabu kuhusu uke wenza ulioimbwa na Sami Haji Dau na Mwapombe na haswa pale Sami Haji Dau aliposema “Ukewenza ndio wenye maliwaza, kazi na mwenzio atakupokeza”. Siku zote jibu la Sharifa lilikuwa “Jambo zuri kama hili bora uanze wewe Bwana Dau”. Baada ya jibu hilo tunaishia kucheka!

Kifo ni siri kubwa ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka. Aidha maisha baada ya kufa ni siri kubwa zaidi ambayo hakuna mwanadamu anayejua. Hata hivyo katika mafunzo yake, Mtume Mohamed (SAW) anatuambia kuwa binadamu wenyewe ndio mashahidi wakubwa wa hatima ya mtu anapokwenda baada kifo. Iwapo mtu ameishi vizuri na binadamu wenziye, hao binadamu wenziye ndio mashahidi wa wema alioufanya. Kwa wale waliotenda mabaya wakati wa uhai wao, binadamu huwa mashahidi wa hayo. Kwa sisi tuliomfahamu Sharifa, tunashuhudia kuwa wakati wote wa uhai wake aliwafanyia wema watu wengi ambao kwa kupitia wema wake, leo wamepata msingi mzuri wa maisha. Pamoja ya kuwa hakuna binadamu mwenye haki ya kuhukumu hatima ya binadamu mwenziwe baada ya kufa, lakini sisi ambao tumeamiliana na Sharifa, tuna dhana njema kuwa amepata mapokezi mema huko Barzaq.

Dhana hii inathibitishwa na kauli ya Nassor Basalama ambaye alimuuguza Sharifa kwa kuwa naye muda wote mpaka alipoaga dunia. Kwa maneno ya Nassor, siku za mwisho za uhai wake, Sharifa alikuwa katika hali mbaya kiasi ambacho muda wote alikuwa amefumba macho.

Kwa muda wote huo Nassor alikuwa hospitali na kumsomea visomo mbalimbali ikiwemo Sura Yassin na Swalat Naria huku akiwa amemshika mkono. Hata hivyo muda mchache kabla hajaaga dunia kwa mara ya kwanza Sharifa alikunjua mkono wake na akawa anaupigapiga mkono wa Nassor kumpa ishara kuwa amtazame. Alipomtazama usoni, akamuona Sharifa akiwa na tabasamu kubwa, kisha akamwambia kwa sauti ya chini kuwa “nimefurahi sana kukuona”. Muda mchache baadaye alifariki dunia saa 8 dakika 32 mchana akiwa amezungukwa na mumewe wa zaidi ya miaka 40 Mzee Yusuf Kalala, binti zake wawili Farida na Rahima, wadogo zake wawili, Zahra na Shekha wote wakiwa na waume zao. Kwa mujibu wa Nassor, Sharifa ameiaga dunia huku akiwa na utulivu na tabasamu pana usoni mwake. Alifariki akiwa hana hofu wala huzuni. Na hizo ndizo sifa za watu wema wakati wanakata roho kama alivyosema Mwenyezi Mungu kwenye Quran Sura ya 41 Aya 30:

Hakika waliosema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu, kisha wakadumu katika waliloliamini, hao huwateremkia malaika (wakati wa kukata roho) wakawaambia: msiogope, wala msihuzunike; furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Azithibitishe amali za Sharifa, ampe makazi mema peponi na amuongezee ucheshi wake aliokuwa nao hapa duniani awe nao katika Barzaq na siku ya hesabu. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe sisi wafiwa subira njema.

Aaaamin, Yaa Rab!

Columnist: mwananchi.co.tz