Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA: Yusuf Lule awa rais, adumu siku 68 tu - 4

40566 LULE+PICTANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA: Yusuf Lule awa rais, adumu siku 68 tu - 4

Thu, 7 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mara baada ya Mkutano wa Moshi uliomalizika Machi 26, 1979 na taarifa kutolewa kwa waandishi wa habari siku iliyofuata, Yusuf Lule alirejea Dar es Salaam ambako aliandaa tangazo la redio lililorekodiwa kwenye mkanda wa kaseti na baadaye kutumwa Kampala kwa ajili ya Redio Uganda.

Kwa mujibu wa jarida la Summary of World Broadcasts: Non-Arab Africa la Ijumaa ya Aprili 13, 1979, katika mkanda huo Lule alisema: “Najisikia heshima na faraja kuwatangazia muundo wa serikali ya mpito kwa nchi yenu. Serikali yenu itakuwa kama ifuatavyo....”

Baada ya kujitaja kuwa rais wa serikali ya mpito ya Uganda na majina ya mawaziri wake aliowateua akiwa mjini Dar es Salaam, Lule aliahidi kuwa kutafanyika uchaguzi mkuu nchini Uganda “mapema kadiri hali itakavyoruhusu”.

Miongoni mwa waliotajwa katika baraza lake ni pamoja na Sam Sabagareka, Otema Alimadi, Paulo Mwanga, Dk Arnold Bisasi, A. Biararuha, Mathias Ngobi, Profesa Asavia Wandira (Elimu), Dani Wadada Nabudere (Utamaduni na Maendeleo ya Jamii), George Wilson Kanyeihamba (Sheria) na Luteni Kanali William Omaria.

Siku ya kuapishwa kwake ilipangwa iwe Alhamisi ya Aprili 12, 1979. Siku hiyo asubuhi, Lule na mawaziri aliowateua waliondoka Dar es Salaam kwa ndege kupitia Mwanza. Lakini ndege hiyo ilipotua Mwanza, maofisa usalama wa Tanzania walianza kutilia shaka kama kweli kuna usalama wa kutosha mjini Kampala. Iliamuliwa kuwa ndege ya Lule izuiwe kwanza hadi siku iliyofuata.

Lule aliapishwa Ijumaa ya Aprili 13, 1979. Siku chache baada ya kuapishwa alianza kupuuza maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano wao wa Moshi ambayo yaliwekwa kwenye katiba ya Umoja wa Kitaifa wa Kuikomboa Uganda (UNLF).

Katiba ya UNLF haikumpa Rais madaraka makubwa kama ya kuwateua mawaziri wake. Mamlaka makubwa yaliwekwa mikononi mwa Baraza la Ushauri la Taifa (NCC). Hapo ndipo mgogoro ulipoanza. Profesa Lule na washauri wake, akiwamo Dk Andrew Lutaakome Kayiira, ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la wapiganaji wa msituni lililopambana na serikali ya Obote na Tito Okello, walianza kufanya uteuzi wa nafasi kubwa bila kuishirikisha NCC.

Hali hiyo iliwakasirisha maofisa wa UNLF na wajumbe wa NCC. Lule aliwajibu kwa kuwaambia kuwa maazimio yaliyopitishwa na Mkutano wa Moshi hayakuwa na nguvu ya kisheria na kwamba angeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutumia katiba iliyokuwapo kabla Idi Amin hajatwaa madaraka. Katiba hiyo iliyotengenezwa na Dk Milton Obote na ilimpa rais madaraka makubwa.

Vitendo vya Lule vilianza kuonekana wakati aliposhindwa kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa wajumbe wa NCC na hata ilipopangwa kufanyika upya, Lule alihudhuria lakini akaondoka baada ya kutoa hotuba fupi, hata kabla ya wajumbe kuapishwa, jambo lililowakasirisha zaidi.

Bila kuishirikisha NCC, Lule aliendelea kuwateua mawaziri na manaibu aliowataka. Aliwateua mawaziri 24 na manaibu wake 20 na moja kwa moja wakawa wajumbe wa NCC, wakiwazidi kwa idadi wajumbe waliochaguliwa na Mkutano wa Moshi.

Wajumbe wa NCC walikerwa zaidi pale Lule alipompa kila waziri wake Dola 5,000 za Marekani kama posho ya kukarabati nyumba zao.

Walipomuuliza kwa nini akaamua kumpa kila mjumbe kiasi hicho cha fedha kutoka mfuko wa Serikali iliyofilisika, wajumbe waligomea fedha hizo.

Yote hayo yalikuwa yakifanyika wakati Kampala ikiwa katika hali ya hatari. Milio ya risasi ilikuwa ikisikika kila siku—hasa usiku—na miili ya watu ikiwa inaokotwa kila asubuhi.

Wakati mgogoro kati ya Profesa Lule na NCC ukifikia hatua mbaya, Rais Julius Nyerere alikutana na viongozi wa serikali ya Uganda, akiwemo Lule na Paulo Muwanga, mkoani Mwanza. Walipata chakula cha mchana Hoteli ya Mwanza.

Kitabu cha New African Yearbook 1991/92 kinasema katika mabadiliko ya baraza la mawaziri ya Lule, mawaziri kumi kati ya 19 walikuwa Wabaganda. Na baada ya kukutana na Nyerere mjini Mwanza, alifanya mabadiliko mengine na kuongeza mawaziri sita.

Baada ya kupata chakula, Muwanga alipokea taarifa kutoka Kampala kwamba Redio Uganda imetangaza mabadiliko ya baraza la mawaziri na kwamba hata yeye mwenyewe ameguswa. Aliondolewa Wizara ya Mambo ya Ndani akapelekwa Wizara ya Kazi. Hatua hii ilimkasirisha Muwanga, kwa mujibu wa kitabu cha UPC and National-Democratic Liberation in Uganda kilichoandikwa na Yoga Adhola.

Pia mwandishi wa kitabu cha Guardian Angel: Volume Two: The Moshi Conspiracy, Dk Arnold Spero Bisase anasema Muwanga aliapa kuwa lazima amshughulikie Lule. Lule alianza kuonekana sugu kwa kufanya mabadiliko bila ya kuishirikisha NCC, alikuwa haambiliki. Waliona hata baada ya kuonywa na Nyerere, aliendeleza kiburi na kwa tabia hiyo waliona hata kiongozi huyo wa Tanzania hangeweza kumuokoa.

Nyerere alimwambia Lule afuate Azimio la Moshi linalotaka mamlaka makubwa yawe kwa NCC na si ya Rais. Lule alimsikiliza Nyerere, lakini ni kama hakumsikia.

Ijumaa ya Juni 8, 1979, wajumbe waliokuwa na hasira wa NCC, walikutana mjini Kampala na kupitisha azimio la kumtaka Lule akabidhi uteuzi wote “haraka” kwa NCC ili ujadiliwe na kuidhinishwa. Siku nne zilipita bila NCC kupata jibu. Wajumbe wakakutana tena na kupitisha azimio jingine lililomtaka Lule atekeleze matakwa yao “mara moja”. Hata hivyo hawakupata jibu.

Juni 19, 1979 NCC wakakutana tena, safari hii Ikulu ya Entebbe, wakianza mkutano wao saa 9:22 alasiri chini ya uenyekiti wa Edward Bitanywaine Rugumayo.

Lule naye alihudhuria mkutano huo. Alipotakiwa kueleza sababu za kupuuza maazimio ya NCC, alijibu hakufanya hivyo kwa sababu huko kungemaanisha “kuhusisha masuala muhimu ya kikatiba”.

Mjadala mkubwa uliibuka, kwa mujibu wa kitabu cha UPC and National-Democratic Liberation in Uganda. Mazungumzo ya wajumbe wengi yalikuwa Azimio la Moshi. Ingawa Lule alijitetea sana, alibanwa.

Alisema hakuwahi kupata mawasiliano yaliyotumwa kwake na NCC, lakini barua ya NCC aliipeleka Rugumayo mwenyewe ofisini kwa Lule.

Muda mfupi baadaye, Profesa Paulo Wangoola akatoa hotuba ndefu, akisema “demokrasia imewekwa majaribuni. Uamuzi unafanywa nje ya NCC, Lule ameibaka UNLF. Tumefikia mahali pagumu sana. Kuna ombwe la kisiasa. Rais (Lule) haikubali UNLF na hatuwezi kuwa na Rais asiyeikubali UNLF. Ingawa Lule alifanya kazi muhimu kutuleta Kampala, sasa anatukwamisha”.

Wangoola akahitimisha kwa kuleta hoja ya kutokuwa na imani na Profesa Lule. Mjadala mrefu ukaanza na kuendelea hadi usiku wa manane.

Hatimaye ilipohitimu saa 7:00 usiku, kura za siri zikapigwa. Dakika 35 baadaye matokeo yakatangazwa. Wajumbe 18 waliunga mkono hoja, 14 walipinga. Rugumayo akamgeukia Lule, na kumwambia kuwa yeye si Rais wa Uganda tena.

Baada ya kumwambia hivyo Lule, aliwageukia wajumbe na kusema “waliomwodoa Lule kwenye kiti chake pia wamewaondoa na mawaziri wake”. Lule, pamoja na wajumbe wengine tisa wa NCC wakasusa na kuondoka kikaoni. Lule akakoma kuwa Rais wa Uganda, akiwa ameongoza nchi kwa siku 68 tu.

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz