Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA: Binaisa ambadili Lule baada ya matukio kibao - 5

40770 Pic+uganda TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA: Binaisa ambadili Lule baada ya matukio kibao - 5

Mon, 11 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Urais wa Profesa Yusuf Lule ulidumu kwa siku 68 tangu Aprili 13 hadi Juni 20, 1979. Kosa lake kubwa ni kutotii mamlaka ya Baraza la Ushauri la Taifa (NCC) kwa kujiteulia mawaziri na manaibu bila kushauriana na chombo hicho.

Kwa maana hiyo, Lule, ambaye wakati huo alikuwa na miaka 68, akawa ni rais aliyeitawala Uganda kwa muda mfupi zaidi katika historia ya nchi hiyo baada ya kukaa madarakani kwa siku 68. Aliondolewa madarakani usiku wa manane.

Kwa mara nyingine tangu kuanguka kwa Idi Amin, Uganda ikawa haina rais. Majina matatu yalipendekezwa; Paulo Muwanga, Edward Rugumayo na Godfrey Binaisa. Wawili kati yao - Muwanga na Rugumuyo walikuwa kwenye mkutano uliompigia kura Lule ya kutokuwa na imani naye na kuanza mchakato wa kumpata mbadala wake na hivyo wawili hao kutakiwa kuondoka kwenye chumba cha mkutano ili wajadiliwe.

Zikafuata hotuba nyingi za kuwasifia watu hao watatu, lakini akajitokeza Yonasani Kanyomozi, ambaye alisema miongoni mwa wote hao, ni Binaisa pekee ambaye hakuwa mjumbe wa NCC na ni mtu pekee ambaye hakushiriki katika kikao chochote cha kumwondoa Lule madarakani.

Hoja ya Yonasani ni kwamba kwa kumchukua Binaisa na kuwaacha wale wengine ingetoa taswira kwamba NCC haikumuondoa Lule ili imuweke mjumbe yeyote wa NCC.

Mkutano uliahirishwa kwa dakika chache, kisha ukaanza tena saa 9:30 usiku. Ulianza na hoja ya Edward Rugumayo ya kuwarejesha wale walioondoka mkutanoni pamoja na Lule na hivyo kuibuka ubishi kidogo, wengi wakijenga hoja kuwa walisusia kikao.

Hatimaye ikaamuliwa kuwa Tarsis Bazana Kabwegyere aende kuwaita walioususia mkutano na ambao wakati huo walikuwa eneo la Ikulu wakijadiliana pamoja na Lule.

Ilipotimu saa 10:18 alfajiri alirudi mkutanoni na kuripoti kwamba aliwakuta ‘wasusiaji’ kwenye ‘moyo wa uasi’, na “bado wanamtaja Lule kama rais wa Uganda”. Baadhi waliamua kurejea, lakini kwa shingo upande.

Katika raundi ya kwanza ya upigaji kuta, Paulo Muwanga aliondolewa kwenye kinyang’anyiro baada ya kuambulia kura tatu. Rugumayo alipata kura tisa na Binaisa akapata kura saba.

Katika raundi ya pili, Binaisa aliibuka mshindi kwa kupata kura 11 na Rugumayo akipata kura nane. Saa 11:45 asubuhi ikatangazwa kuwa “Uganda imepata rais mpya”. Jitihada za kumpata rais mpya zilikamilika kabla Waganda wengi hawajaamka.

Lakini, hadi wakati NCC inamchagua kuwa rais mpya, Binaisa alikuwa usingizini. Wakati wakisubiri kujua aliko na namna ya kumpasha habari hizo, wajumbe hao wa NCC pia walitumia fursa hiyo kupanga mambo kadhaa ambayo yalihitaji kushughulikiwa haraka.

Ilipofika saa 1:45 asubuhi ya Jumatano ya Juni 20, 1979, Yoweri Museveni aliingia kwenye ukumbi wa mikutano akiwa na Binaisa na kupokewa na makofi ya wajumbe 19 waliobakia ukumbini.

Binaisa, aliyesomea Uingereza na ambaye alikimbilia Marekani mwaka 1971, ndiye aliyezuiwa kuingia ukumbini kwenye Mkutano wa Moshi, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Guardian Angel: The Moshi Conspiracy cha Arnold Spero Bisase. Siku hiyo alikuwa amekaa nje ya ukumbi bila kutambua kuwa katika kipindi cha miezi michache baadaye angekuwa rais wa Uganda.

Akiwa bado anashangaa, Binaisa alitambulishwa kwa kila mjumbe wa NCC na baadaye kuahidi kuwa angetekeleza maazimio ya Mkutano wa Moshi na kuitii NCC.

Mmoja wa viongozi wa NCC, Dani Wadada Nabudere, alimtaka Binaisa ajione kuwa ni mwenyekiti wa Kamati Kuu ya UNLF na si rais wa Uganda. Urais wa Uganda ulimjia Binaisa kama bahati nasibu kwa sababu alikuwa Uganda—tena Kampala—wakati wa anguko la Yusuf Lule.

Alikuwa ndio kwanza amerejea Uganda akitokea New York, Marekani, na nia yake ilikuwa ni kugombea nafasi ya kuwa mwakilishi wa kudumu wa Uganda wa Umoja wa Mataifa, kumbe nia hiyo iligongana na kuondolewa kwa Lule, huku wajumbe wengi wakifurahia kuwepo kwake jijini Kampala.

Binaisa aliahidi kufanya kazi na NCC na kuepuka yaliyofanywa na Lule. Walimuahidi kumsaidia kuteua baraza lake la mawaziri papo hapo. Paulo Muwanga akateuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Museveni (Wizara ya Ulinzi), aliyeondoka na Lule ukumbini, Dk Arnold Bisase (Waziri wa Afya).

Dk Bisase alikubali uteuzi huo ingawa kwa shingo upande, na akaonya kuwa baraza limeweka mfano mbaya sana kwa kumuondoa Lule madarakani.

Kisha Dk Bisase akautaarifu mkutano kuwa ametumwa na Lule atangaze kujiuzulu wadhifa wake kwa sababu za kiafya. Baraza lilipokea kauli hiyo kwa furaha kwa sababu wafuasi wa Lule nchi nzima hawangeleta shida.

Ghafla wajumbe wakaanza kumsifia Lule. Yale masuto ya usiku uliotangulia yakawa yamesahaulika. Baraza likapiga kura ya kumpa Lule nyumba, ulinzi na mafao kwa muda wote uliobakia wa maisha yake. Wakati yote hayo yakifanyika, bado Lule alikuwa Ikulu.

Wajumbe walimuita na wakaendelea kumsifia. Baadaye akapata nafasi ya kuzungumza ambayo aliitumia kuwapongeza wajumbe, akisema alitamani kutoa hotuba mbili—moja kwa NCC na nyingine kwa vyombo vya habari.

Kwa NCC alisema: “Nilichaguliwa kule Moshi (Tanzania) kuendeleza vita dhidi ya Amin hadi mwisho. Si tu kwa kuikomboa Kampala bali nchi nzima. Uganda imekombolewa. Sihitaji zaidi ya hilo. Kama sasa baraza (NCC) halinitaki, siwezi kupinga. Naliomba baraza liniruhusu nizungumze na vyombo vya habari.”

Kisha akaondoka chumba cha mikutano na kupanda ghorofani kwenda kurekodi hotuba yake kwa vyombo vya habari. Mkutano ukaahirishwa kwa muda.

Wakati mkutano ulipoanza tena, Muwanga akatoa hoja kwamba rekodi ya sauti ya Lule isikilizwe kwanza kabla haijapelekwa kituo cha Redio Uganda. Alisema hawakuwa na hakika na kile ambacho angekisema kwa waandishi wa habari.

Baadaye mkanda wa sauti yake ukasikilizwa na wajumbe wa baraza. Lule alisema katika mkanda huo kuwa alilazimishwa kujiuzulu na kwamba kuondolewa kwake ni njama za kumrejesha Milton Obote madarakani.

Mjadala mzito ulifuatia na hatimaye kura zikapigwa. Ikaamuliwa kuwa taarifa peke yake ambayo ingetolewa hadharani ni ile ya Rugumayo kutangaza kuwa Lule ameondolewa madarakani na Binaisa amechaguliwa kuwa rais mpya wa Uganda.

Saa 11:00 jioni baada ya mkutano kudumu kwa zaidi ya saa 25, uliahirishwa. Hata kabla kikao hakijamalizika, Binaisa alikuwa ameshafikishwa Kampala. Viongozi wa dini mbalimbali walialikwa kwenye hafla ya kuapishwa kwa Binaisa katika eneo lilelile ambalo Lule aliapishwa siku kadhaa zilizopita. Binaisa aliapishwa haraka hata kabla ya wageni wengi waalikwa kufika.

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz