Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA- 6: Lule azuiwa Tanzania, Nyerere amwangukia

40911 Pic+tanzania TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA- 6: Lule azuiwa Tanzania, Nyerere amwangukia

Tue, 12 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati Godfrey Lukongwa Binaisa akifurahia kuchaguliwa na Baraza la Ushauri la Taifa (NCC) kuwa rais mpya wa Uganda huku akiwa amejificha kwenye hoteli ya Nile Mansions, Redio Uganda ilitangaza Juni 20, 1979 mchana kuwa wananchi wameanza kukusanyika mitaani kumpinga.

Hadi kufikia jioni mitaa ya Kampala ilikuwa imejaa watu waliokuwa wakiimba “tunamtaka Lule, tunamtaka Lule”. Usiku kucha wananchi walizidi kumiminika mitaani.

Kelele zilizidi kiasi cha kuweza kumkosesha usingizi Binaisa.

Majeshi ya Tanzania yaliingia Kampala kujaribu kurejesha hali ya utulivu, lakini wengine walirushiwa mawe.

Wakati huo, Profesa Yusuf Lule alikuwa amezuiwa ikulu ya Entebbe ambako alikuwa akipewa taarifa za maandamano hayo. Hii ilimfanya aendelee kudai kuwa yeye bado ni rais halali wa Uganda.

Wafanyakazi na wafanyabiashara wengi mjini Kampala waligoma. Lakini Waziri wa Ulinzi, Yoweri Museveni akaenda studio za Redio Uganda na kupiga marufuku maandamano yote. Waandamanaji waliondoka mitaani, lakini biashara zilisimama.

Binaisa na Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, wakalazimika kufikiria namna ya kushughulikia tatizo la Lule.

Kwa kuwa Lule alikuwa bado akidai kuwa yeye ni rais wa Uganda wakati NCC ikiwa imeshateua rais mwingine, hakupaswa kuendelea kubaki Uganda. Nyerere akampigia Binaisa akamwambia alitaka kuongea na Lule na kwamba wakutane Dar es Salaam.

Ingawa Lule alikuwa amesema anataka kwenda Nairobi, aliposikia Nyerere anamhitaji aliamua kumfuata.

Lule alisafiri kwenda Dar es Salaam akisindikizwa na mmoja wa viongozi wa NCC, Dani Wadada Nabudere. Kwa mujibu wa kitabu cha UPC and National-Democratic Liberation in Uganda kilichoandikwa na Yoga Adhola, Lule alipokewa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na Waziri wa Ulinzi, Rashid Kawawa na katibu wa Rais, Joseph Butiku na kupelekwa Ikulu.

Asubuhi iliyofuata, Nyerere alikutana na Lule na kuongea naye. Alimwambia kuwa alipata taarifa za kutatanisha kutoka Entebbe, nyingine zikisema Lule amejiuzulu kwa hiari yake na nyingine zikidai amelazimishwa. Nyerere alimtaka amwambie ukweli, lakini Lule alimjibu Nyerere kuwa hakuja Dar es Salaam kujadili masuala hayo, jambo lililomuudhi Nyerere, akakasirika akaondoka.

Msaidizi wa Lule anayeitwa James Senabulya, kwa mujibu wa habari iliyoandikwa na Ssemujju Ibrahim Nganda katika gazeti la The Observer la Agosti 10, 2009, Nyerere alimpelekea Lule waraka na kumwambia “weka saini hapa kuwa umeng’atuka urais wa Uganda kwa sababu kwa sasa tuna rais mwingine”.

Lule aligoma, lakini aliendelea kubaki Dar es Salaam kwa siku kadhaa. Siku chache baadaye Nyerere (au wajumbe wake) alimwendea tena Lule na kutaka kujua kama ameshabadili mawazo. Lule aligoma.

Lakini Nyerere alimtembelea Lule mara kadhaa. Wakati mmoja akamuuliza Lule: “Unadhani bado wewe ni rais halali wa Uganda?” Hii ilimkera Lule. Nabudere akamwambia Lule aache kuendelea kulalamika. Lule akasema dhamira yake inamsuta na kwamba alitaka Uganda kuwe na kura ya maoni.

Nabudere akamwambia kwa hali ya ghasia ilivyokuwa Uganda, suala la kura ya maoni halingewezekana na kwamba kama angetoa kauli ya kumuunga mkono Binaisa, kusingekuwa na shida yeye kurejea Uganda. Nyerere alianza kumuona Lule kuwa ni mkaidi.

Baadaye Nyerere akasema kama Lule asingekana kauli yake ya kwamba yeye ni rais wa Uganda, asingeruhusiwa kuondoka Dar es Salaam. Alisema aliweza kumzuia Milton Obote mjini Dar es Salaam kwa miaka minane na amekwenda vitani na kumuondoa Idi Amin, kwa hiyo isingekuwa shida kwake kumzuia Lule.

Kwa hiyo Lule akaanza maisha yake katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Kwa vyovyote vile, Lule alikuwa aondolewe madarakani. Kwa mujibu wa Mica Kiribedda katika kitabu chake cha Uganda’s Political Turmoil Post Idi Amin: The Untold Stories, Lule alikuwa akamatwe na kutiwa nguvuni.

“Katika hali hii, chochote kile ambacho Lule angefanya au kutofanya, tayari NCC walikuwa wameshatengeneza njama ya kumwangusha wakimtuhumu kuwa aliteua mawaziri bila kushirikisha baraza. Na katika mazingira ya kushangaza, ilionekana kana kwamba ni Rais Nyerere aliyekuwa akiamuru hayo akiwa Dar es Salaam,” ameandika.

Ilipojulikana tu kwamba Lule alizuiwa kuondoka Dar es Salaam, familia yake mjini London, Uingereza, ilianza kulalamika kupitia vyombo vya habari. Madaktari wake nchini Uingereza wakadai kuwa afya ya Lule inahitaji uangalizi wa mara kwa mara na

kwamba kwa ‘kushikiliwa’ Dar es Salaam kulimaanisha hatari kwa afya yake. Balozi wa Uingereza mjini Dar es Salaam, Sir Peter Moon, naye akaingilia kati jambo hilo.

Lakini kila siku iliyopita Nyerere alizidi kukerwa na ukaidi wa Lule. Lule alitaka kwenda Kenya, Nyerere akamkatalia na akaendelea kubaki Dar es Salaam. Wakati huo mgomo mjini Kampala ulikuwa umepungua. Maduka yalianza kufunguliwa.

“Lule angeruhusiwa tu kurejea Uganda iwapo angefuta kauli yake ya kuisuta Tanzania kwa kuondolewa kwake madarakani.

Lule aligoma kufuta kauli kwa sababu hakuhitaji ruhusa ya Tanzania kurejea nchini mwake,” ameandika Ogenga Otunnu katika kitabu cha Cricis of Legitimacy and Political Violence in Uganda, 1979 to 2016.

“Hata hivyo (Lule) alikosea sana. Tanzania ilimzuia kurejea Uganda,” likaandika jarida la New Africa la Septemba 1979. Baada ya hapo, “Dk Paul Kawanga Ssemogerere akawa kiongozi wa chama cha DP” kilichokuwa kikiongozwa na Lule, liliandika jarida Africa Confidential la Julai 16, 1980.

Baada ya Uingereza kumwambia Nyerere kuwa wangemzuia Lule kujihusisha na siasa, Nyerere alipunguza hasira kwa Lule. Hata hivyo hakuona faida yoyote ya kuendelea kumzuia Dar es Salaam.

Baada ya Lule kupewa tiketi ya ndege, Nyerere alimsindikiza Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam. Akapanda ndege ya Shirika la Uingereza, British Airways na kurejea Uingereza kukutana na familia yake.

Ndani ya wiki moja kuanzia hapo Malkia Elizabeth alitarajiwa kuzuru Tanzania na ilidaiwa, angeshukia kwenye vyumba vile vile vilivyotumiwa na Lule. Kwa maana hiyo ilidaiwa kuwa ujio wa Malkia Elizabeth ulichangia kuondoka kwa Lule.

Baada ya kuona asingeweza kurejea maradakani, Lule alianzisha kikundi alichokiita Uganda Freedom Fighters (UFF) akiwa nje ya Uganda.

Kikundi hicho kilikuja kuungana na kikundi kingine kilichoanzishwa na Yoweri Museveni kilichoitwa Popular Resistance Army na kuunda kile kilichoitwa National Resistance Army (NRA).

Soma zaidi: TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA: Binaisa ambadili Lule baada ya matukio kibao - 5

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz