Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA 1979-1986: Obote afanyiwa zengwe, Nyerere ambana Dar

39960 Pic+obote TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA 1979-1986: Obote afanyiwa zengwe, Nyerere ambana Dar

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hakuna asiyeamini kuwa kiongozi wa zamani wa kijeshi wa Uganda, Idi Amin aliondolewa na majeshi ya Tanzania kwa kushirikiana na waasi wakati wa kukamilisha Vita vya Kagera vilivyoanzia katika ardhi ya Tanzania. Lakini unajua kuwa viongozi wengine waliofuata baada ya Yusuf Lule, aliyembadili Amin, waliingia madarakani kwa msaada kutoka Tanzania? Kuanzia leo, William Shayo anatuletea makala mfululizo za jinsi viongozi wa Uganda walivyoingia na kuondoka hadi Yoweri Museveni alipochukua nchi na jinsi Tanzania ilivyohusika.

Vita vya Kagera vilivyokuwa mwishoni mwa miaka ya sabini, vilisababisha kiongozi wa kijeshi wa Uganda, Idi Amin kuondolewa madarakani na wanajeshi waliomuasi kwa kushirikiana na majeshi ya Tanzania.

Baada ya Idi Amin kuondolewa Aprili 11, 1979, ilikuwa ni lazima apatikane raia wa Uganda kwa ajili ya kuiongoza nchi hiyo. Wakati vita vikiendelea nchini humo, kulikuwa na mkutano uliokuwa ukifanyika mjini Moshi, maarufu kama Mkutano wa Moshi.

Mkutano huo uliohusisha watu walioikimbia Uganda ulifanyika kuanzia Jumamosi ya Machi 24 hadi Jumatatu ya Machi 26, 1979. Makundi 28 ya Waganda yaliwakilishwa katika mkutano huo kwa nia ya kuanzisha umoja wa kuikomboa Uganda na kurejesha demokrasia. Umoja huo ukaitwa Uganda National Liberation Front (UNLF).

Mipango ya kuanzisha mkutano huo ilifanyika Dar es Salaam ingawa wakimbizi wa Uganda walikuwa wameanzisha mipango hiyo miezi kadhaa hata kabla ya Idi Amin kuivamia Tanzania.

Waganda waliokuwa nchini kwao, Kenya, Zambia, Uingereza na Marekani walikuwa wameshaanzisha harakati hizo, kila kikundi kivyake, lakini hakuna mtu aliyewaunganisha wote kuwa kitu kimoja na chenye nia moja.

Mara baada ya majeshi ya Idi Amin kuivamia Tanzania, Rais Julius Nyerere alimwita Obote aliyekuwa Lusaka, Zambia na kumwambia aandae watu kutafakari mustakabali wa Uganda. Obote ndiye aliyeiongoza Uganda kupata uhuru mwaka 1962 na baadaye kushika urais kuanzia mwaka 1966 hadi 1971, hivyo wakati huo alikuwa uhamishoni baada ya Serikali yake kupinduliwa.

Baada ya ushauri huo, Obote aliwasiliana na Waganda waliokuwa barani Ulaya, Afrika Mashariki na ndani ya Uganda kama Paulo Muwanga (ambaye baadaye alikuwa Waziri Mkuu) na Otema Alimadi (Waziri wa Mambo ya Nje na baadaye Waziri Mkuu kwa miaka mitano kuanzia 1980).

Wengine ni Edward Rugumayo (mwanadiplomasia na msomi aliyekuwa waziri chini ya watawala watatu tofauti na baadaye mwenyekiti wa Bunge), Eleker Ejalu, Dani Wadada Nabudere (msomi na mwanaharakati, waziri na kinara wa harakati za kumuondoa Idi Amin) na Omwony Ojwok, mwanasiasa ambaye baadaye aliteuliwa kuwa waziri chini ya utawala wa sasa.

Obote hakuwasiliana na Yoweri Museveni, wakati huo akiwa kijana, mhitimu wa chuo kikuu, mwanaharakati wa mapinduzi aliyepata mafunzo ya upiganaji wa msituni nchini Msumbiji. Museveni alitafutwa na maofisa wa Tanzania akitakiwa akutane na Obote, lakini kwa wakati huo tayari Museveni alikuwa kwenye mapigano Bukoba na hivyo hakuweza kurudi kukutana na Obote hadi ilipofika Machi 1979.

Katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam Jumanne ya Novemba 28, 1978, watu walioitwa na Obote walipitisha azimio la kuanzishwa kwa kamati ya kuandaa mkutano wa wawakilishi wa vikundi vyote vilivyokuwa vinampinga Idi Amin.

Nyakati fulani katika majadiliano, Nabudere, msomi aliyejulikana kuwa na msimamo mkali alibishana sana na Obote akimtuhumu kuzuia wazungumzaji kuongea kwa uhuru. Pia alimtuhumu Obote kuwa alikuwa akikutana na vikundi vidogo, jambo lililowatia shaka kwamba alikuwa na nia ya kuwagawa.

Mwezi uliofuata Nabudere alijitenga na Obote na kuanzisha kundi lake ambalo liliwajumuisha baadhi ya wajumbe ambao pia walijitoa kwenye makundi mengine.

Baadhi ya wajumbe wa vikundi vingine vilivyokuwa vinakutana Nairobi, Kenya na London, Uingereza na kwingineko wakaonyesha kutokumkubali Obote. Ndipo hatimaye ukaja Mkutano wa Moshi.

Dk Milton Obote hakuhudhuria mkutano huo na wajumbe wa mkutano huo hawakuelezwa sababu, lakini katika kitabu chake cha mwaka 2000 alichokiita What is Africa’s Problem?, Museveni, ambaye alihudhuria mkutano huo alidokeza jambo. “Kwa ujumla haijulikani kama Tanzania ndiyo iliyomzuia Obote kwa lazima asihudhurie Mkutano wa Moshi na ni Tanzania ilitushawishi tumkubali (Profesa Yusuf) Lule kuwa kiongozi wetu ingawa hatukumfahamu sana kisiasa,” ameandika Museveni katika kitabu hicho.

Hii inamaanisha kuwa Tanzania, na kwa maana hiyo Mwalimu Nyerere, ndiyo ilihusika katika kuamua Profesa Lule awe kiongozi wa Uganda baada ya kuanguka kwa Idi Amin.

Ingawa habari za mkutano huo zilisambaa mapema kwa waalikwa, Obote alifichwa. Nia ya Tanzania ilikuwa ni kumzuia Obote kuhudhuria. Alhamisi ya Machi 8, 1979— majuma mawili kabla ya Mkutano wa Moshi kuanza Mwalimu Nyerere alimwita Obote na kumwambia kuwa kuna mkutano umeandaliwa na kwamba ingekuwa bora zaidi kwa mkutano huo ikiwa yeye (Obote) asingehudhuria.

Kwa zaidi ya siku kumi kuanzia siku hiyo Obote na mwenzake, Otema Alimadi, walijaribu bila mafanikio kupata dondoo au angalau ajenda za mkutano huo.

Walijaribu hata kuwadodosa maofisa wa Serikali ya Tanzania, lakini hawakuambulia chochote.

Jioni ya Jumatano ya Machi 21, 1979, yaani siku mbili kabla ya kuanza kwa mkutano huo ofisa mmoja wa Serikali ya Tanzania alimpelekea Obote barua ya kumwalika pamoja na wawakilishi wengine wa chama chake cha Uganda People’s Congress (UPC) kuhudhuria mkutano huo. Ingawa hiyo ilikuwa ni Machi 21, barua hiyo iliandikwa juma moja lililokuwa limepita—yaani Jumatano ya Machi 14.

Dani Wadada Nabudere, ambaye ndiye alikuwa amepewa jukumu la kumtafuta Obote ili ampe ujumbe wa mwaliko huo, baadaye alikiri kuwa alimtafuta “kwa siku kadhaa bila mafanikio”. Baadaye mwaka huo, Nabudere aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na katika badiliko la baraza la mawaziri akateuliwa tena kuwa Waziri wa Utamaduni na Maendeleo ya Jamii.

Baada ya kupata mwaliko, Obote aliwaambia maofisa wa Tanzania kwamba lazima angehudhuria mkutano huo na papo hapo alianza kuwapigia simu wafuasi wake waliokuwa Afrika Mashariki na Ulaya na kwenda Moshi “haraka iwezekanavyo”. Ndani ya saa 48 alifanikiwa kuwapata zaidi ya watu 80 walioahidi kuhudhuria.

Alhamisi ya Machi 22, ikiwa ni siku moja kabla ya mkutano, Mwalimu Nyerere, akijua kuwa Obote alikuwa amejiandaa kwenda katika Mkutano wa Moshi, alimtembelea nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na kumwambia asihudhurie na badala yake atume watu wa kumwakilisha.

Pia alimwambia atume ujumbe wa kuunga mkono azimio litakalofikiwa katika mkutano huo. Alimwambia pia kuwa kama angehudhuria, huenda mkutano huo ungevunjika.Obote alitamani sana kuhudhuria na alikuwa amejiandaa vya kutosha, lakini hakuthubutu kumbishia Nyerere. Vyovyote vile asingeweza kumkatalia Nyerere.

Alikubali kutohudhuria ingawa kwa shingo upande. Kisha akaandaliwa barua fupi ya kuunga mkono maazimio ya mkutano huo na kutakiwa atie saini - jambo ambalo alilifanya.

Kitabu cha War in Uganda: The Legacy of Idi Amin, kilichapisha barua hiyo.

“Natuma salamu zangu kwa washiriki wote wa mkutano huu. Nilitamani sana kuhudhuria lakini sikuweza kuja kuungana nanyi. Lakini nitakuwa nanyi kiroho na nina matumaini makubwa kuwa uamuzi utakaofikiwa na mkutano huu utakuwa ndio mwanzo wa Uganda mpya,” kitabu hicho kimenukuu barua hiyo.

“Macho ya dunia yako kwenye mkutano huu. Macho hayo ni muhimu sana, lakini muhimu zaidi ni macho ya Waganda. Washiriki wengi wametoka mbali, lakini wana shauku moja ambayo ni kutafuta njia ya pamoja dhidi ya hofu iliyotanda nyumbani.

“Nawatakia nyote mafanikio mema na nataka kuwahakikishia kuwa ingawa sitahudhuria, nitashirikiana nanyi kutekeleza uamuzi uliofikiwa kwenye mkutano.”

Andrew Mwenda, mwandishi wa habari ambaye pia ni mwanzilishi wa gazeti The Independent la Uganda, alifanya mahojiano na Obote katika siku za mwisho za maisha yake. Katika makala aliyoiita Upon Meeting Him, I Found Museveni a Consummate Liar, Mwenda alimnukuu Obote akielezea kitendo cha kuzuiwa kushiriki.

“Nilipata mwaliko ... Niliufurahia sana. Uliletwa kupitia kwa mkurugenzi wa usalama na [nilimwambia] nimekubali kuhudhuria. Kisha Nyerere alikuja kuniona na kusema ‘Milton usiende. Hawa watu hawajafanya chochote. Huna hadhi kama ya hawa wanaokutana Moshi’, Mwenda amemnukuu Obote katika makala hiyo.

“Baadaye akaniandikia barua nzuri yenye nukuu za (William) Shakespeare... Nyerere hakuniambia sababu hasa za yeye kunizuia kwenda Moshi. Niwe mkweli tu. Sababu alizonipa hazikunishawishi, sikufurahi. Lakini kwa heshima aliyokuwa nayo, na kutokana na urafiki wetu, nilikubali uamuzi wake.”

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz