Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA 1979-1986: Mtifuano mkutanoni, Lule achaguliwa Rais-3

40284 Pic+mtifuano TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA 1979-1986: Mtifuano mkutanoni, Lule achaguliwa Rais-3

Wed, 6 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkutano wa Moshi ulitarajiwa kuanza Ijumaa ya Machi 24, 1979 mjini Moshi katika ukumbi wa YMCA (Young Men’s Christian Association), lakini ulichelewa kwa sababu wajumbe walitumia siku nzima kujisajili.

Usajili ulikuwa ni muhimu kwa sababu, kama ilivyoelezwa na mmoja wao, ilikuwa ni lazima sifa za washiriki zijulikane kwa sababu walijitokeza wajumbe wengi kuliko ilivyotarajiwa. Wote walidai wana haki ya kushiriki mkutano huo kiasi kwamba ilifikia wakati baadhi walitupiana maneno na wengine hata kurushiana makonde.

Mkanganyiko mkubwa uliibuka kuhusu nani mwenye sifa ya kuhudhuria. Zaidi ya Waganda 200 walifika Moshi, wengi wao wakiwa wafuasi wa Obote, lakini wakidai kuwa wanawakilisha makundi tofauti.

Ingawa kila mmoja aliambiwa ajisajili jambo ambalo lilifanywa na kila Mganda aliyefika Moshi, siku iliyofuatia zaidi ya nusu waliarifiwa kuwa hawakuwa na sifa za kuhudhuria mkutano huo na hivyo walizuiwa.

Katika dakika za mwisho kamati ya usimamizi iliamua kuwa kutokana na ufinyu wa nafasi ukumbini, kila kikundi kitoe wawakilishi wawili na waangalizi wawili.

Kwa ujumla karibu watu 80 walishiriki mkutano huo uliotawaliwa na usiri mkubwa huku wengine zaidi ya 140 wakizuiwa. Kamati ya uongozi haikuweka wazi vigezo ilivyotumia kuwazuia baadhi ya watu waliotaka kushiriki.

Miongoni mwa waliozuiwa ni Godfrey Lukongwa Binaisa, mwanaharakati aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Uganda (1962-1968) na baadaye kushika urais kwa mwaka mmoja (1979-1980).

Binaisa, akiongozana na rafiki yake mkubwa aliyeitwa Isreal Mayengo alifuata mkutano huo akitokea New York, Marekani. Masaibu yake hayakuanzia katika mkutano bali akiwa Marekani. Tiketi yake ya ndege iliporwa na mtu ambaye hakumjua. Lakini baadaye alipatiwa nyingine na aliwasili hadi Dar es Salaam Machi 22.

Ingawa Binaisa alipewa tiketi ya ndege na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya safari yake ya Dar es Salaam—Moshi, ikimaanisha kwamba alikuwa na baraka zote za Serikali ya Tanzania, bado alizuiwa kuingia ukumbini kwa madai kwamba kundi lake la Waganda la nchini Marekani, Uganda Freedom Union, lilishaingiza wajumbe wanne kwenye mkutano. Binaisa alikaa nje ya ukumbi wa YMCA na baadaye kurejea hotelini kwake.

Wanasiasa wawili wakongwe wa Uganda - Paulo Muwanga na Otema Alimadi nao walizuiwa, lakini mwakilishi wa Tanzania kwenye mkutano huo, Benjamin Mkapa (aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje), aliingilia kati na kuhakikisha kuwa Muwanga na Alimadi wanaruhusiwa kuingia ukumbini na kwa hadhi ya ujumbe maalumu kama Lule.

Hiyo ni kwa mujibu wa Dk Arnold Spero Bisase aliyeandika katika kitabu chake cha Guardian Angel: Volume Two: the Moshi Conspiracy (uk. 135).

Alimadi alikuwa akifanya kazi kwa karibu sana na Obote na, kulingana na maelezo ya Ogenga Otunnu katika kitabu chake cha Crisis of Legitimacy and Political Violence in Uganda (1979 to 2016), Obote alimpa Alimadi maelekezo ya kwenda kuhakikisha wafuasi wao wengi wanahudhuria.

Mkapa pia aliishawishi kamati ya usimamizi ya mkutano kumruhusu Askofu Yona Okoth kama mjumbe maalumu. Okoth alikuwa askofu wa Kanisa la Anglikana mjini Tororo. Mwaka 1977, baada ya kuuawa kwa Askofu Janani Jakaliya Luwumu aliyekuwa mkuu wake, Okoth alikimbilia Marekani. Luwumu aliuawa na Idi Amin Februari 17, 1977.

Mkapa aliwataka washiriki waache kulumbana na watambue kuwa kazi yao ilikuwa ni kuunda umoja wa kumng’oa Idi Amin na kuiongoza Uganda. Aliwashauri waruhusu watu wengi kadiri inavyowezekana washiriki na kuwaonya kuwa mkutano huo lazima utoke na muafaka na si kupigiana kura. Mwishowe akawataka wamalize “haraka sana” suala la usajili ili mkutano uanze.

Ingawa Tanzania ilimzuia Obote kuhudhuria mkutano huo, ilizuia wafuasi wake wasiondolewe mkutanoni. Ilihakikisha pia kwamba Waganda waliopigana vita Uganda wanawakilishwa mkutanoni.

Asubuhi ya Machi 24, mkutano ulianza kwa siri katika Bwalo la Polisi mjini Moshi. Waandishi na wanadiplomasia walizuiwa kuingia, ingawa ofisa mmoja wa ubalozi wa Uingereza nchini alifanikiwa kujipenyeza. Washiriki walisisitizwa kutotoa taarifa zozote za kinachoendelea ndani ya mkutano.

Mkutano huo ulifunguliwa na Profesa Tarsis Kabwegyere, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kundi la Nairobi lililoitwa Nairobi Consultative Committee, akitangaza kaulimbiu ya “Lazima Sote Turudi Nyumbani”.

Baadaye akamwalika Mkapa kuhutubia wajumbe. Katika hotuba yake fupi, Mkapa aliwaambia wajumbe kuwa wao ndio wanaopaswa kuamua hali ya baadaye ya Uganda na si Watanzania. Aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa mkutano huo ni Semei Nyanzi, ambaye aliliongoza kwa mafanikio Shirika la Maendeleo la Uganda (UDC) kabla ya kukimbilia Uingereza mwaka 1973 kuukwepa utawala wa Idi Amin.

Mara kwa mara wafuasi wa chama cha UPC cha Obote walikuwa wakisusia vikao, lakini Obote alilazimika kuwapigia simu kuwataka warudi mkutanoni. Mkapa naye akawaambia hata kama wangesusia, Serikali ya Tanzania inautambua mkutano na itatambua azimio lolote litakalofikiwa.

Kauli hiyo ilisababisha wajione wanafanya kazi bure hivyo wengi wakarudi ukumbini na mambo yakaendelea. Ilipofika saa 11:00 jioni chombo cha kuikomboa Uganda kikazaliwa, kikijulikana kwa jina la Uganda National Liberation Front (UNLF) na Lule akachaguliwa kuwa mwenyekiti wake.

UNLF ikawa na vyombo vinne vya utendaji, kikubwa kikiwa ni Baraza la Ushauri la Taifa (NCC) ambalo lilikuwa na mamlaka ya kutengeneza sera na kusimamia utawala. Mwenyekiti aliwajibika kwa NCC.

Katika kumchangua mwenyekiti wa NCC, Edward Bitanywaine Rugumayo, ambaye alikuwa mwanasiasa, mwanadiplomasia, msomi na mwanaharakati wa mazingira aliyewahi kuwa spika wa Bunge la Uganda, alipita bila kupingwa baada ya Martin Jerome Okec Aliker na Paul Kawanga Ssemogerere kuondoa majina yao. Wajumbe wa baraza hilo, ambao walichaguliwa kutoka miongoni mwa makundi yaliyowakilishwa katika Mkutano wa Moshi, walikuwa na hadhi ya ubunge.

Chombo cha pili cha UNLF kilikuwa Kamati Kuu ya UNLF (NEC) ambayo kazi yake ilikuwa ni kutekeleza sera za NCC. Chombo hicho kilikuwa chini ya NCC.

Profesa Yusuf Kironde Lule, ambaye alikuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Makerere kuanzia mwaka 1964 kabla ya kuukimbia utawala wa Idi Amin, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa UNLF katika mkutano huo na kwa hiyo angekuwa Rais wa Uganda baada ya Amin kung’olewa.

Kisha kulikuwa na Tume ya Siasa na Diplomasia ambayo ingeshugulika na mambo ya nje. Chombo cha nne kilichoundwa chini ya UNLF kilikuwa ni Tume ya Kijeshi (MC) ambayo kazi yake ilikuwa ni kushughulikia masuala ya kivita—kama vile kuunda jeshi la kitaifa baada ya kuangukwa kwa Idi Amin.

Mkutano ulimalizika Machi 26, 1979 na siku iliyofuata, Lule akafanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa hoteli ya Moshi na kusema kuwa walipanga kuandaa uongozi wa mpito “haraka iwezekanavyo”.

Wakati kukiwa na shangwe miongoni mwa Waganda mjini Moshi, jijini Dar es Salaam, Obote alihuzunishwa sana na matokeo ya mkutano, alihisi kutengwa. Aliona mambo yanayohusu utawala wa Uganda yakifanyika bila yeye kushirikishwa.

Alihisi hadhi yake imeporwa. Hata hivyo hakuwa na la kufanya zaidi ya kusubiri na kutazama hali ya mambo ilivyokuwa ikienda.

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz