Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA 1976-1986: Idd Simba apendekeza jina la Lule urais Uganda-2

40158 Pic+uganda TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA 1976-1986: Idd Simba apendekeza jina la Lule urais Uganda-2

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa miaka mingi tangu Serikali ya Uganda ilipopinduliwa na Idi Amin mwaka 1971, Profesa Yusuf Lule hakuwa kiongozi muhimu wala maarufu kwa Waganda walioikimbia nchi yao, lakini katika yale majuma machache tu kuelekea siku ya kuanza kwa Mkutano wa Moshi, kampeni zilianza kufanyika miongoni mwa Waganda waliokuwa katika miji ya Dar es Salaam, Nairobi na London.

Pamoja na wajumbe kuanza kuona dhahiri kuwa angeibuka kuwa kiongozi wa umoja wa kuikomboa Uganda, wengi waliulizana kuhusu Lule na hilo linadhihirishwa na kauli ya Yoweri Museveni katika kitabu chake cha mwaka 2000 cha What is Africa’s Problem? alipoandika “Lule ... hatukumfahamu sana kisiasa”.

Lakini wako walioona kuwa Lule angeweza kuwaunganisha Waganda wa ndani na nje ya nchi. Kukubalika kwa Lule kulichangiwa pia na Waingereza ambao walikuwa na wasiwasi kuwa huenda Tanzania ingemsimika Milton Obote

Lule alipata elimu yake ya juu katika vyuo vya Fort Hare (Afrika Kusini) na Bristol na Edinburgh (Uingereza) na alianza kazi ya uhadhiri Chuo Kikuu cha Makerere cha Uganda. Kuanzia mwaka 1964 hadi 1970 alikuwa makamu mkuu wa chuo hicho, lakini baadaye alikimbia utawala wa Idi Amin na kwenda kuishi London, Uingereza.

Mkewe, Hannah Lule, alikuwa akiendesha biashara kubwa ya duka la nguo mjini Kampala wakati wa utawala wa Idi Amin.

Mmoja wa wanasiasa wa Tanzania walioonekana kumpigia Lule chapuo ni Idd Simba, ambaye kwa wakati huo alikuwa mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika jijini Abijan, Ivory Coast. Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, Simba alikuwa wa kwanza kupendekeza jina la Lule na kusisitiza kuwa ndiye anaweza kuiongoza Uganda baada ya Idi Amin kuangushwa.

Na kulikuwa na sababu ya Idd Simba kuwa na msimamo huo. Kwa mujibu wa kitabu cha Contesting Global Order: Development, Global Governance, and Globalization cha James H. Mittelman (uk. 36), Idd Simba ni mmoja wa maofisa wa Serikali ya Tanzania waliowahi kufukuzwa na Idi Amin nchini Uganda. Hiki ni kipindi kile ambacho Watanzania wengine walikuwa wakikamatwa na kutiwa kizuizini nchini Uganda, na wengine kuuawa au kufukuzwa.

Kuna wakati ofisi yake ilikuwa Arusha na wakati mwingine Kampala. Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipovunjika mwaka 1977, Simba akawa mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Ingawa alikuwa CCM, alionekana ana mrengo wa kibepari zaidi kuliko wa kijamaa.

Idd Simba alianza kulipigia kampeni jina la Yusuf Lule hata kabla ya kuitishwa kwa Mkutano wa Moshi na ndiye alikuwa kiungo muhimu kati ya Waganda waliokuwa Uganda na Kenya, ubalozi wa Tanzania na maofisa wa Serikali mjini Dar es Salaam.

Lule, kama walivyokuwa Waganda wengine waliokuwa uhamishoni nchini Uingereza, alikuwa akiwasiliana na Serikali ya Tanzania kupitia kwa ubalozi wa Tanzania jijini London, na vikao vingi vilikuwa vikifanyika ubalozini. Kwa hiyo kwa sehemu kubwa ilikuwa ni kana kwamba Lule alichaguliwa na wanasiasa wa nje ya Uganda kuliko Waganda wenyewe.

Jumamosi ya Machi 10, 1979 Lule na Dk Arnold Spero Bisase waliwasili Dar es Salaam.

Wiki iliyofuata Lule alikutana na Nyerere na katika kikao chao ndipo Nyerere alipoona kuwa Lule angefaa. Nyerere alimuuliza Lule kama binafsi alikuwa amepanga kwenda Moshi au kama mwakilishi wa kikundi. Lule alijibu kwamba anakwenda kama sehemu ya kundi la akina Roger Makasa.

Kati ya makundi yaliyokuwa yakiendelea na harakati za kumuondoa Idd Amin, moja lililoweka kambi yake jijini Nairobi lilijulikana kwa jina la Kundi la Katoliki, liliongozwa na Mukasa, ambaye alikuwa kwenye Serikali ya zamani ya Obote lilifanya majaribio kadhaa ya kuingiza silaha na askari nchini Uganda.

Lakini Nyerere alimwambia Lule kuwa kwa hilo atakuwa anakosea kwa sababu anapaswa asionekana kuegemea upande wowote. Baada ya mazungumzo na Nyerere, ndipo Lule akaalikwa kwenye mkutano kama “mjumbe maalumu”.

Nyerere akamtaka Lule afanye kazi kwa karibu na Obote kwa kuwa bado Obote alikuwa na watu wengi nyuma yake. Nyerere alimtaka Lule akae nyumbani kwa Obote kwa siku nzima ya Jumapili ya Machi 18 kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu mustakabali wa Uganda.

Habari zinasema wawili hao wakawa wanaulizana maswali ya kutegana.

Lule alikataa kumwambia Obote kwamba alikuja Dar es Salaam kwa sababu ya Mkutano wa Moshi, bali ni kwa sababu ya kazi za Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Afrika ambalo yeye alikuwa katibu wake mkuu. Alimwambia pia kuwa ndani ya wiki chache alihitaji kwenda Kenya na baadaye Uingereza kwa ajili ya matibabu.

Siku iliyofuata, yaani Jumatatu ya Machi 19, Lule na Grace Stuart Katebariirwe Ibingira walikwenda kumtembelea Dani Wadada Nabudere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Wakati huo, Nabudere alikuwa profesa mshiriki, kwa mujibu wa kitabu chake alichokiita From Agriculture to Agricology: Towards a Global Circular Economy cha mwaka 2001.

Akiwa naye, Lule alimueleza kuwa alikuja Tanzania kufanya kazi za msaada kwa wakimbizi wa Uganda, lakini akamdokeza kuwa amekutana na Nyerere pamoja na Obote.

Nabudere akawaambia Lule na Ibingira kuhusu mpango wa Mkutano wa Moshi. Siku iliyofuata, Nabudere aliwakuta Lule na Ibingira wakiandaa hotuba ndefu hotelini kwao kwa ajili ya mkutano huo.

“Hii inaonyesha alikuwa amejiandaa vilivyo kwa Mkutano wa Moshi,” Martha Honey, ambaye ni mwandishi wa habari, anakariri jinsi Nabudere alivyomwambia baada ya tukio hilo.

Ingawa alikuwa akidanganya wenzake, Lule alikuwa Dar es Salaam kujipigia kampeni baada ya yeye na wenzake kufanikiwa kumshawishi Nyerere kuwa alifaa kuiongoza Uganda.

Jina lake lilikuwa linajadiliwa sana na wajumbe wa mkutano kiasi kwamba mshiriki mmoja alisema “jina la Lule lilikuwa likichomoza na la Obote lilikuwa likizama”.

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz