Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Super Sunday Makala: Usomaji wa vitabu unaongeza fikra kwa kiwango kikubwa

7868 Zwas2qwe TZW

Sun, 13 May 2018 Chanzo: bongo5.com

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), iliyotolewa May 2016 ilieleza kuwa utamaduni wa watu kujisomea vitabu unazidi kupungua duniani.



Wakati Tanzania ikifikia kiwango cha juu kabisa cha usomaji miaka ya 1970, kiwango hicho hadi leo hakijawahiwi kufikiwa.

Makala yangu imelenga kuangazia hilo ili kuibua upya motisha ya kusoma vitabu. Awali tunapaswa kujua kwa nini utamaduni huo unaenda ukipotea.

Ni wazi watu wengi hujikuta wakiingia katika gereza hili kutokana na shughuli za kila siku za kujitafutia kipato, hivyo moja kwa moja wanajikuta wamejitenga katika ulimwengu huo.

Maisha kwa sasa yapo kasi, kila mmoja anajaribu kikimbizana nayo kadiri pumzi zake zinavyoruhusu, ni watu au familia chache zinazoweza kupata muda wa kusoma vitabu, majarida na magazeti pia.

Hata waliokuwa na utamaduni wa kujisomea huenda wakajikuta hamasa yao ikishuka siku hadi siku kutokana na ukuaji wa teknolojia. Ujio wa mitandao ya kijamii umechukua nafasi kubwa katika utamaduni wa watu kujisomea vitabu.

Utitiri wa taarifa zinazopatikana katika kurasa za mitandao ya Facebook, Twitter, Instagram pamoja na YouTube umewaondolea watu sababu ya kusoma vitabu. Hata hivyo ukuaji huo wa teknolojia ndio umewezesha kuwepo kwa vitabu katika mitandao (e-Book) ambavyo mara nyingi hupatikana katika App na baadhi huwa katika mfumo wa sauti.

Jahman Anikulapo mwandishi kutoka nchini Nigeria anasema utamaduni wa kupakuwa (downloads) vitabu mtandaoni haupo katika kizazi hiki, labda wale waliozaliwa kuanzia mwaka 2000. Pia anaeleza wasomaji wa vitabu vya kimtandao ni wachache sana wanaoweza kutunza kumbukumbu.

Kwanini Tunasoma Vitabu?

Mwanafizikia mwenye asili ya Kiyahudi kutoka nchini Ujerumani, Albert Einstein (1879–1955) aliyepata umaarufu mkubwa duniani aliwahi kutoa msimamo wake kuhusu usomaji wa vitabu.

Eistein alisema; Usomaji wa vitabu baada ya umri fulani unaongeza fikra kwa kiwango kikubwa na kuboresha uwezo wa kutafakari. Mtu yeyote anayesoma sana na kutumia ubongo wake vyema hawezi kutumbukia katika vitendo ya kizembe.

Hivyo tunaweza kukubaliana kuwa kuna mambo muhimu na makubwa yaliyofichwa ndani ya vitabu, hata hivyo hatari ni kwamba idadi kubwa ya watu ipo mbali na hilo kama walivyoeleza UNESCO.

Kutokana na hilo kuna uwezekano mkubwa maarifa yatakayoubadili ulimwengu yakasalia katika maandishi na sio katika maisha ya watu.

Mwanafalsafa mmoja alipata kusema; Utajiri wa dunia upo katika makaburi. Maana ya kauli yake ni kwamba watu wanafariki wakiwa na mawazo au maarifa mapana ambayo yangeweza kuutajirisha ulimwengu na wao pia.

Waandishi wa vitabu dunia kote hawataki kuupeleka utajiri huo katika makaburi, bali wamelenga kuuacha katika maktaba (vitabu) ili uweze kunufaisha vizazi vijavyo.

Hata hivyo kusoma vitabu pekee hakukuhakikishii kupata maarifa bali inategemea ni kitu gani unasoma kwa wakati huo.

Inaelezwa kuwa kichwa cha binadamu ni sawa na kiwanda cha kutengeneza mawazo, kama ilivyoa ada ili kiwanda kiweze kutengeneza bidhaa nzuri na bora ni lazima kuwepo kwa malighafi nzuri pia.

Hivyo kama unahitaji kuwa mtu mwenye mawazo bora/maarifa siku zote katika biashara, uhasibu, michezo, dini, kwenye ndoa, mahusiano nakadhalika ni kusoma mambo yatakayo kujenga katika eneo husika.

Watu wanapenda kusoma nini?

Frank Shayo ambaye ni muuzaji wa vitabu Posta, Dar es Salaam alinieleza idadi ya watu kujisomea vitabu inaongezeka ingawa ni kwa kusuasua.

Akiwa ana miaka zaidi 15 katika kazi hiyo, anabainisha kuwa vitabu ambavyo vinaelezea maswala ya ujasiriamali, biashara na namna ya kufanikiwa katika maisha vimekuwa na soko kubwa.

Vitabu vya waandishi maarufu duniani kama Napoleon Hill, Ben Casto, Robert Kiyosaki na watu waliofanikiwa katika mambo makubwa duniani kama Mark Zuckerberg na Steve Jobs vimekuwa vikiuliziwa mara nyingi na kununuliwa na watu wengi bila kujali hali zao kiuchumi.

Hata hivyo anaonya kuwa ugumu wa maisha kwa sasa ukilinganisha na kipindi cha nyuma utapelekea watu wengi kushindwa kumudu gharama za kununua vitabu.

Kutokana na hali hiyo Shayo anaeleza idadi ya watu hasa vijana kupenda kusoma vitabu vinavyoelezea maswala ya kimahusiano na ndoa si kubwa kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Kwa kipindi hiki idadi kubwa ya wanataka kusoma mambo yatakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Anaongeza kuwa vitabu vya sheria vimeanza kusomwa na watu wengi miaka hivi karibuni hata wale wasiokuwa na taaluma hiyo. Hilo linatokana na watu wengi kutaka kujua baadhi ya mambo ambayo ni ya kawaida katika sheria.

Mbinu za Kufanikiwa Unaposoma

Kuna mbinu ijulikanayo kama SQ3R (Survey, Question, Read, Recite, Review); hii msomaji anasoma kitabu kwa kuangalia lengo kuu kisha unajiuliza baadhi ya maswali juu ya hilo.

Kwa mfano umesoma kuhusu msimu wa mvua katika mkoa wa Kagera ili kujipanga kwa ajili ya kilimo. Unaweza kujiuliza Kagera kuna misimu mingapi ya mvua kwa mwaka, hivyo unarudia kusoma upya ili kupata jibu la swali lako.

Pili ni OK5R (Overview, Key idea, Read, Record, Recite, Review, Reflect), njia hii msomaji atatafuta lengo kuu katika kurasa (mada) akishapata ataandika pembeni kile alichoelewa.

Baadaye ataanza kuyatoa kwa kuzungumza yale aliyosoma kama vile umekariri, njia hii inamsaidia msomaji kutunza kumbukumbu. Tukutane Jumapili ijayo kwa Makala kama hizi.

Loading...
Columnist: bongo5.com