Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Suala la marehemu wa Mbeya lifike mwisho

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maisha ya binadamu yana thamani yake. Ndio maana nchi mbalimbali zimetunga sheria kuhakikisha watu wake wanalindwa na usalama wao linaendelea kuwa jukumu la Serikali.

Si hivyo tu, karibu nchi zote duniani zinasisitiza kuwa kila raia ana haki zake za msingi.

Mmoja ya haki hizo ni heshima. Kila mtu anapaswa kuheshimiwa bila kujali umri, jinsi, kabila, taifa au rangi yake.

Ni dhahiri kuwa katika vitu ambavyo kila mtu hutaka kufanyiwa kutoka kwa wengine ni kuheshimiwa.Heshima ni jambo la msingi kwa binadamu.

Kutokana na umuhimu wa heshima kwa kila mtu, ndio maana sheria mbalimbali zimewekwa kuhakikisha kuwa jambo hilo linakuwa haki ya msingi ya kila mtu.

Kila mtu anastahili heshima kuanzia anapozaliwa mpaka anapofariki dunia. Hili ni jambo la msingi na ndio maana hata mtu anapofariki dunia huagwa kwa mila, desturi, tamaduni na heshima zote za jamii husika.

Tumeanza kwa ufafanuzi huo mfupi, huku tukiwa tunasikitishwa na jinsi mwili wa marehemu Frank Kapange (21) kuendelea kuhifadhiwa mochwari ya Hospitali ya Rufaa, Kanda ya Mbeya kwa miezi saba.

Tunatambua kuwa suala hilo lipo mahakamani, lakini si nia yetu kugusa mwenendo wa kesi hiyo wala kuingilia kesi yenyewe.

Lengo letu ni kuomba pande zinazohusika katika kulishughulikia suala hilo; iwe ndugu, mahakama au waendesha mashitaka wafanye haraka ikiwezekana kwa dharura.

Haileti picha nzuri hata kidogo kuona mwili wa binadamu anayestahili kupumzishwa kwa heshima zote ukiendelea kukaa mochwari kwa zaidi ya siku 230.

Tangu Frank alipofariki dunia Juni 4 mwaka jana huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na ndugu kudai kuwa kijana wao ambaye alikuwa mfanyabiashara wa nguo za mitumba Soko la Sido alifariki kutokana kipigo akiwa mikononi mwa Polisi, bado suala hilo halijapata ufumbuzi wa mwisho.

Ndugu walifungua shauri Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mbeya itoe amri ya kufanyika kwa uchunguzi wa kifo hicho.

Mahakama hiyo ilitupilia mbali shauri hilo kwa maelezo kuwa halina mashiko na kuamuru mwili huo kuzikwa huku ikitaka ndugu kubeba gharama zote za mazishi.

Ndugu hawakuridhika na uamuzi huo wakaamua kukataa rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo nayo ilitoa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo baada ya kujiridhisha kuwa mlalamikaji hakufuata taratibu wakati wa kufungua kesi hiyo.

Hata hivyo, Januari 3, wakili wa familia hiyo, Moris Mwamwenda aliliambia gazeti hili kwamba wanakwenda Mahakama ya Rufani na sasa anachosubiri ni kuitwa na msajili wa mahakama hiyo ili kujulishwa kama shauri hilo limeshafanyiwa kazi ili awasilishe sababu za rufaa yake.

Hatupendi kurudi kwenye historia ya tukio hilo, tunachotaka ni kuona marehemu akipewa heshima yake ya ubinadamu. Tunaamini kuwa suala hilo linaweza kuharakishwa mahakamani ili likamilike mapema na haki ipatikane.

Huu si utamaduni wetu Tanzania, kuchukua muda mrefu kiasi hiki bila kuzika mtu aliyefariki dunia. Kwa hali ilipofikia busara inahitajika zaidi kutatua suala hili ili marehemu apewe haki yake ya msingi ya kuzikwa kuliko kuendelea kuhifadhiwa mochwari kwa muda wote huo.



Columnist: mwananchi.co.tz