Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Spidi ya Makonda inaishia wapi?

69946 Pic+makonda

Mon, 5 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Siku za nyuma alikuja na wazo la waalimu kutolipa nauli za daladala. Lengo likiwa kuwapunguzia makali ya maisha. Kukawa na sintofahamu nyingi sana za namna ya kufanikisha zoezi hilo.

Si tu halikutekelezeka, bali hata nusu bei kwa madenti ni vita tosha na makonda wa daladala kwa miaka mingi.

Mbaya zaidi walimu wanaojaribu kuonyesha vitambulisho ili wasilipe nauli wanadhalilishwa na maneno ya ovyo kutoka kwa makondakta.

Akaja na zoezi la kukamata wanaolala gesti mchana. Hili pia licha ya kutofanyika, hata nia, lengo na shabaha yake haikuwahi kuwekwa wazi kabisa. Kwa Dar Salama hii angeishia kuua biashara za gesti na kujaza magereza. Pengine zoezi lingefanyika tungeelewa nia yake.

Kuna ule mipango wa kutaka filamu za nje zitozwe kodi kama si kupigwa marafuku. Lengo lilikuwa kupigania soko la filamu za wasanii wetu. Dhamira ilikuwa njema, njia ikawa batili, na mpaka leo hii hakuna mwendelezo. Kwenye hili bila shaka aliangushwa na wadau.

Moja ya kero kwa mkoa wake wa Dar Salama ni mabasi ya mwendokasi. Ni vile Wabongo tuna kipaji cha kuzoea shida. Ndiyo maana tuko kimya husikii malalamiko.

Pia Soma

Makonda aliibuka alfajiri pale Kimara kushuhudia na kuahidi kulisimamia hilo na tatizo litaisha. Abiria bila shaka wako salama ndiyo maana hakuna kelele. Lakini, ukifika vituoni utashangaa mtiti na jinsi wanavyosubiri magari kwa matumaini.

Likaja la wakwepa jukumu la malezi ya watoto. Mtiti uliojazana Ilala Boma ulitoa picha kamili kuwa ni tatizo kubwa. Makonda alisimama kama bosi wa mkoa, Ustawi wa Jamii, Polisi na Mahakama. Kina mama wa Dar Salama waliimba jina lake. Na wale wa mikoani walitamani awe kwao. Nia ilikuwa njema, utatuzi ukawa mtihani. Kimyaa.

Kabla vumbi halijatulia likaja jipya la migogoro ya ardhi. Wanasheria wakaandaliwa na watu kwa mamia wakasikilizwa. Hatujasikia ile spidi ilikomea wapi!

Huyo ndiye Makonda. Sasa tumesikia la kwenda mjini umeoga na kufua. Anaibua mambo kibao umaliziaji unakuwa tatizo.

Msukumo wake una nguvu mwanzoni lakini mwishoni hutoweka. Hata jambo likiwa la Dar Salama tu, linageuka gumzo nchi nzima. Ni kama usafi wa kila Jumamosi mwanzoni ilikuwa hekaheka nyingi.

Umesikia ya hivi karibuni? Atashughulika na walio ‘beti’ Taifa Stars ifungwe. Yaani watu tupo ‘bize’ kuomba Mungu tushinde mechi kimiujiza. Kumbe kuna wengine nao wanaomba Mungu tufungwe!

Na Mungu si Athumani anatoa kulingana na hitaji lako. Kwa hili sidhani kama angeishia hewani, labda angechukua hatua zaidi ili siku za baadaye tuweze kushinda.

Columnist: mwananchi.co.tz