Kwa kuwa bado kuna baadhi ya watu wanaonekana kutofahamu ubeberu kwa kuzingatia muktadha wa Tanzania mpya, nimeona niandike, japo kwa kifupi, kutoa ufafanuzi kidogo.
Ni vigumu kuuelewa ubeberu iwapo hujui dhana ya uchumi wa dunia. Nimeona maeneo mbalimbali watu wakipoteza muda kudhani kuwa ubeberu ni rangi ya mtu, au mtu mmojammoja, la hasha. Ubeberu ni njama za kimataifa zikiongozwa na mataifa tajiri – Amerika na Ulaya, kuhakikisha umiliki wa uchumi wa dunia unaendelea kubaki kwenye himaya zao.
Mabeberu hutumia vyombo vya kibeberu kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na taasisi za Bretton Woods (BWI) – Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Shirika la Biashara Duniani (WTO), Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Binadamu (ICC), Mahakama Kuu ya Kimataifa (ICJ), Kituo cha Kimataifa cha Kutanzua Migogoro ya Uwekezaji wa Kimataifa (ICSID) na mashirika mengine.
Ubeberu ndio chimbuko la umaskini, vita, maradhi na ujinga katika nchi zinazoendelea. Aidha, ubeberu ndio chanzo cha nchi tajiri kuendelea kuwa tajiri. Kitakwimu, utajiri wa nchi za mabeberu una mwambatano kinyume na ufukara wa nchi maskini duniani.
Ubeberu ni miundo na mifumo ya kunyonya nchi changa ili nchi tajiri ziendelee kuwa tajiri. Ni mwendelezo wa njia ya unyonyaji, kunyonya nchi changa baada ya ukoloni mkongwe kuondoshwa. Ubeberu ni mjukuu wa ukoloni mkongwe.
Mwaka 1945, mara baada ya vita kuu ya pili ya dunia (vita baina ya mabeberu wakigombea kunyonya mataifa maskini), mataifa tajiri yaliasisi na kuweka muundo wa kuitawala dunia na kujimilikisha rasilimali duniani kote.
Kwa hiyo, miundo na mifumo (sheria na kanuni za kimataifa) ya siasa, biashara, uchumi, utamaduni, teknolojia na kadhalika, iliwekwa kwa lengo kuu la kuhakikishia mataifa ya Ulaya na Amerika yanaendelea kutawala dunia.
Pengine tunaweza kusema kuwa kuibuka kwa China na mataifa mengine machache kuchagiza mabadiliko ya sera na sheria zinazoongoza vyombo vya kibeberu ni fursa pekee kwa nchi changa kupambana na kuushinda ubeberu.
Hadi sasa ni zaidi ya miaka 70 dunia imekuwa ikiongozwa na sera za mabeberu ambazo hupikwa na kupakuliwa London, Brussels, Washington au New York – hii kwa pamoja huitwa Washington. Sera za nchi changa zikienda kinyume na sera za Washington Consensus, taifa husika hupigwa vita, hufitinishwa au kuwekewa vikwazo vya kiuchumi. Lakini, kukubaliana na sera za Washington ni kuhakikisha taifa hilo linaendelea kuwa maskini, lenye watu fukara, wagonjwa na wajinga pia – wananchi wanaozeeka haraka (umbo) na kufa na umri mdogo.
Hapa kuna mfano halisi mdogo. Kati ya mwaka 1997-1998, WB iliyafanyia makampuni ya nje ukuwadi, kuja kuwekeza kwenye uchimbaji wa dhahabu nchini Tanzania, ambapo bei ya wakia moja ilipigiliwa kwa dola za Marekani 260 kwa wakia moja.
Ingawa tangu wakati huo bei ya dhahabu iliendelea kupanda hadi kufikia dola 1,300 kwa wakia moja, hadi leo mikataba ya madini (MDAs) inayotumika bado inatambua dola 260 kwa wakia. Hao ndio mabeberu na hiyo ndio dhima ya ubeberu – kuzinyonya nchi maskini. Taifa likikataa sera na mipango ya mabeberu linakiona cha moto – kuwekewa vikwazo, kuingizwa kwenye vita, fitina za kisiasa, kususiwa na wawekezaji na kadhalika.
Hata Rais John Magufuli alipotangaza kuwa angeiongoza Tanzania inayozingatia maslahi na matakwa ya Watanzania wanyonge, ndio kwanza tulianza kusikia na kuona mengi – BW, EU na washirika wao wakitaka kuzimia mkaa wa moto kwenye macho ya Watanzania.
Wanataka serikali ifumbe macho ili mabeberu waendelee kunyonya nchi kama watakavyo, na kama walivyozoea huko awali, wakitumia zana zao za kawaida – mikopo na misaada. Mabeberu hawataki kufanya biashara na Tanzania kila upande unufaike na kuridhika, ila wanataka watupangie bei za bidhaa au mazao yetu – kahawa, chai, korosho, pamba na kadhalika
Kupitia mkakati wa kutanguliza makampuni yao, wanataka watupangie bei ya madini, gesi asilia na kadhalika.
Huo ndio ubeberu unaoendeleza ujinga, umaskini na maradhi kwenye nchi yetu na hata nchi changa nyingine. Tukiendekeza matakwa ya sera za mabeberu umaskini hauwezi kuisha; maradhi yataendelea; na ujinga utatawala sawia.
Kuna mfano mwingine. Kwa mujibu wa ripoti ya 2012 ya World Gold Council (WGC), kati ya 2007 na 2009, kampuni za kuchimba dhahabu nchini zilizalisha na kuuza dhahabu katika soko la kimataifa na kisha kujipatia dola za Marekani bilioni 5. Katika kipindi hicho, Tanzania iliambulia dola za 78 milioni tu.
Kwa mfano huu, tunaweza kuona usahihi wa dhima ya serikali kufanya mabadiliko makubwa katika tasnia ya uziduaji. Na hii ndio Tanzania mpya.
Mwaka 2017 Bunge lilitunga sheria mahsusi tatu za rasilimali za taifa na zimeanza kutumika ili kuhakikisha rasilimali hizo zinanufaisha wananchi katika umoja na ujumla wao, badala ya mabeberu na mawakala wao.
Haishangazi sheria hizi zimelalamikiwa na mabeberu pamoja na mawakala wao.
Ni bahati mbaya, kwa kutofahamu kwao, utasikia watetezi wa ubeberu na mabeberu wakisema kuwa msimamo wa kisera wa Tanzania mpya utawakasirisha ‘wadau wa maendeleo’.
Pengine tuchukue fursa hii kuwafahamisha watetezi wa ubeberu kuwa mabeberu hawatoi bure vyandarua au hata hizo ARVs. Ukweli ni kwamba makampuni ya kusindika madawa au hata kutengeneza na kusambaza vyandarua ni taasisi za kibeberu ambazo hupewa tenda za kandarasi nono na kulipwa pesa nyingi kutoka Global Fund kufanya kazi hizo.
Fedha za mfuko huo huchangwa na mabeberu haohao kisha kampuni na taasisi kutoka nchi hizo hutumia fedha hizo kutengeneza dawa, vifaa tiba au kutoa huduma za kitaalamu ili kuendeleza uzalishaji mali na kuhifadhi ajira za nchi zao.