Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Somo la Mengi kwa Watanzania

11592 Mengi+picTanzaniaWeb

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watanzania wana kiu ya kujua safari za mafanikio za viongozi, matajiri na watu wengine maarufu.

Wanapowajua, wanajifunza mengi ikiwamo kufahamu mabonde na milima waliyopitia na njia walizotumia kukabiliana na vikwazo.

Njia mojawapo ya Watanzania kuwajua watu hawa, ni kusoma vitabu vinavyowahusu.

Hiki ndicho alichofanya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, aliyeamua kuweka historia ya maisha yake katika maandishi ili kuwatia moyo na kuwazindua wengine watakaokisoma.

Mengi amechapisha kitabu kilichozinduliwa na Rais John Magufuli hivi karibuni. Ni kitabu chenye utajiri wa hekima, ushauri, wosia kwa watu wa kila kada nchini.

Japo ametumia lugha ya Kiingereza isiyofahamika kwa hadhira pana ya Kitanzania, nikiri kuwa ni kitabu muhimu cha kusomwa na kila mtu makini.

Mengi ameandika wasifu huo aliouita kwa jina la ‘I Can, I Must, I Will, The spirit of success,’ akielezea maisha yake ya kutoka kutembea peku kwenda shuleni, hadi kuwa mmoja wa wahasibu wa kiwango cha juu nchini na tajiri wa kupigiwa mfano nchini.

Nini ambacho hajazungumzia katika kitabu hiki? Unataka kujua undani kuhusu ujasiriamali, mafanikio ya kimaisha, mifumo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, usamaria wema na mengineyo? Nakushauri usome kitabu hiki.

Mengi na viongozi

Mengi anaacha wasia mzito kwa viongozi wetu na natarajia viongozi wetu katika kada mbalimbali za uongozi, watajihimu kusoma japo maeneo machache anayozungumzia kuhusu uongozi. Kwa mwanasiasa, hiki si kitabu cha kukosa kwa kuwa kina kioo unachoweza kujitazama. Katika moja ya maelezo yake anaandika: ‘’Naitunza sifa yangu ya kuwa msikilizaji kwa sababu hakuna mtu duniani anayeweza kudai kuwa anamiliki a mawazo na kuamua kipi sahihi na kipi si sahihi…’’

Anaongeza: “…Uongozi bora ni matokeo ya uwezo wa kusikiliza, kuwahusisha watu, kutoa motisha, kutia moyo na kuzungumza na wengine na kupima mawazo yao kutokana na umuhimu wao…. Kwa kweli, uwezo wa kukubali na kuheshimu mawazo kinzani, ni sifa muhimu ya uongozi mzuri.” (Uk 9-10).

Mengi na uendeshaji wa uchumi

Mengi amegusa na hata kukosoa mifumo yetu ya kuendesha mambo, hususan upande wa uchumi.

Kwa kiasi kikubwa anachambua mifumo na sera za kiuchumi tangu enzi za Ujamaa mpaka sasa akionyesha nguvu na udhaifu katika maendeleo ya taifa letu.

Kwa mfano, pamoja na Azimio la Arusha kutumika kama chachu ya ujenzi wa mfumo wa kijamii na kiuchumi kwa Taifa tangu mwaka 1967, analishukia kuwa halikuwapa Watanzania fursa ya kushiriki katika maendeleo yao hasa ya kiuchumi.

Anaandika: “Chini ya Azimio, Watanzania hawakuweza kufanikisha mawazo na shauku zao za maendeleo ya kijamii na kiuchumi; iliwalazimu kuchagua kutoka katika kile ambacho Serikali iliagiza.” (Uk 71)

Imani katika uchumi wa soko

Unapomsoma hukosi kubaini kuwa Mengi ni muumini mzuri wa mfumo wa uchumi wa soko. Anaushangaa uongozi wa siasa nchini kuendelea kuushikilia mtazamo wa kijamaa hata katika kipindi ambacho mfumo wa uchumi wa soko ndio unaotamalaki.

Anaamini kuwa katika uendeshaji wa uchumi wa nchi, Serikali inapaswa kuwa kama kocha badala ya kujipa nafasi ya ukapteni wa timu kama tunavyoendelea kushuhudia.

Uwekezaji na hatma ya wazawa

Isingetarajiwa Mengi aandike kitabu pasipo kuzungumzia ushirikishwaji wa wazawa katika uwekezaji nchini. Ni kilio chake cha muda mrefu kwa kuwa naye ni mwathirika wa sera za kiuchumi zinazothamini zaidi wageni kuliko wazawa.

Kwa mfano, anataka kufanyike mabadiliko katika Sheria ya Uwezeshaji wananchi Kiuchumi. Anasema:

“Kwa umuhimu kabisa, sheria ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, inahitaji kupitiwa na kubadilishwa, ili irandane na mazingira yaliyobadilika ya kiuchumi katika muongo uliopita ambao umeshuhudia wimbi la uwekezaji wa kigeni, huku ukiweka kando maslahi ya wazawa. Haja ya kuwa na uwekezaji wa ndani ni haja iliyo bayana.”

Kwa nini amekuwa mkosoaji?

Mengi, anaamini katika misimamo yake na ndio maana haoni taabu kukosoa sera na baadhi ya mambo anayoona yanakwenda ndivyo sivyo nchini.

Pamoja na ukosoaji wake kumjengea uadui na baadhi ya watendaji serikalini, anasema ataendelea kuiwajibisha Serikali, kwa sababu anaamini anayoyakosoa ni kwa manufaa ya mustakabali, amani na umoja wa nchi.

“Natarajia wafanyabiashara wenzangu, wataamka na kutetea misimamo yao, alimradi wanafanya hivyo kwa maslahi ya jamii,” anaandika. ( uk 65)

Falsafa ya I Can, I Must, I Will na mafanikio kibiashara

Maneno haya ndiyo yaliyobeba siri ya mafanikio yake kama mfanyabiashara na kiongozi wa jamii. I Can, I Must, I Will, yaani Ninaweza, Lazima nifanye, Nitafanya (tafsiri yangu). Ni kauli mbiu si tu inayotakiwa kufanyiwa kazi na wajasiriamali, lakini hata katika maeneo mengine.

Asemapo ‘I Can’ (Ninaweza), anamaanisha ushupavu wa mtu kuendelea na dhamira aliyo nayo. ‘I Must’ ( Lazima nifanye), ni kushikamanana kuishi katika kile ulichoamua kukifanya. I Will (Nitafanya) ni utayari wa kubadili mustakabali kama anavyoupanga mtu. Anasema kuwa historia ya maisha yake ya unyenyekevu kwa watu vilimfanya asione tabu kujichanganya na watu wa aina mbalimbali, bila kujali hadhi na nafasi zao kiuchumi na kijamii.

Kwenye matatizo, kulalamika pekee hakusaidii, bali mjasiriamali makini ni yule anayetumia hali hiyo kama fursa, si tu ya kibishara lakini pia kusaidia jamii yake.

Hiki ndicho alichokifanya baada ya kugundua kuwapo kwa uhaba wa kalamu za wino ambazo miaka ya 1983 ilikuwa ni bidhaa iliyoagizwa kutoka nje. Huu ukawa mwanzo wa Mengi kuingia katika ulimwengu wa biashara akianza na utengenezaji wa kalamu alizozipa jina la ‘Epica.

Mengi na wajasirimali

Kwa wewe mjasiriamali, kitabu kinakuonyesha namna Mengi alivyoamini katika kutumia fursa na kujifunga kibwebwe kutekeleza aliyodhamiria.

Anakufungulia njia unayoweza kupita kuelekea katika mafanikio yako kama mjasiriamali. Inawezekana njia aliyopitia isiwe na tija kwako, lakini bado ukweli unabaki kuwa anakupa mwanga wa nini ufanye, nini usifanye kuelekea kwenye mafanikio si tu ya kijasiriamali, lakini maisha kwa jumla.

Mengi aliuvaa ujasirimali nao ukamvaa angali kijana kabisa. Hata hivyo, mifumo ya kiuchumi ya miaka ya 1970, aliiona kama kikwazo kwa ukuaji wa ari ya ujasiriamali kwa Watanzania.

Anatoa mfano wa ‘Operesheni Maduka’ mwaka 1972, ambayo ilishuhudia utaifishaji hata wa biashara ndogo kama mabucha ya nyama.

“Nilihisi ule moyo wa watu kujihusisha na biashara binafsi na ujasiriamali ukipotezwa na sera na hatua za kiutawala. Nilishangaa uchumi wa nchi ungewezaje kujengwa bila ya kuwa na watu wenye nguvu ya kiujasiriamali,” anaeleza. (uk 42).

Anawananga Watanzania kwa kutojiamini kuhusu biashara huku wengi wanaotamani kuwa wajasiriamali wakiogopa hatari za kuanguka.

“Kitakwimu, biashara nyingi zinazoanza, hufeli, hata hivyo, moyo wa ujasiriamali unatambua kufeli, lakini pia unamtaka mtu asikubali anguko hilo kuharibu shauku yake ya biashara.” (uk 80).

Mengi mpenda kwao

Kama kijana msomi aliyeiva barabara katika uhasibu, fani aliyoisomea nchini Scotland, Mengi hakutaka kulowea ‘majuu’ na kufanya kazi huko japo angeweza kufanya hivyo kama ilivyokuwa kwa wasomi wengi wa Kiafrika. Shauku ya kurudi nyumbani ikamvaa, hata alipopangiwa kazi jijini Nairobi na kampuni ya Coopers Brothers aliyokuwa akifanyia kazi, aliomba haraka uhamisho ili akafanye kazi kwao mjini Moshi.

Ni ishara ya kijana mpenda kwao, sifa ambayo Watanzania na Waafrika wengi kwa jumla wanaikosa hasa wale wanaopata fursa ya kusoma katika nchi zilizoendelea.

Ukitoa utaongezwa

Mengi anatudhihirishia ukweli wa msemo; ‘Toa utaongezewa’. Kwa muda wote kama mfanyabiashara ameishi katika kuutekeleza msemo huu ambao kwa walio wengi ni mfupa mgumu kuutafuna.

Anaeleza: “Napenda kujiona kama bomba linalopitisha maji kwa ajili ya watu wenye kiu… Naridhika nitoapo msaada kama huo na wala sitaraji wanaoupokea walipe fadhila kwangu,” (uk 175).

Mengi na lugha

Mengi anadhihirisha ulumbi alionao wa lugha ya Kiingereza. Uchaguzi wa maneno ikiwamo matumizi ya rejista za kiuchumi, rejea na maelezo ya kitaalamu, vinanogesha kitabu chake ambacho katika baadhi ya maeneo unaweza kufikiri unasoma kitabu cha profesa wa uchumi.

Aidha, nikiri uwezo wake mkubwa wa kunukuu kutoka kwa waandishi mbalimbali duniani. Mtindo wa kunukuu (machapisho zaidi ya 80), si tu vinaipa upekee kazi yake, lakini unampambanua kama mtu anayependa kusoma na hata kuamini katika mawazo ya wengine.

Kasoro niionayo

Kwa kuwa ni kitabu cha mtu anayesimulia safari yake kutoka katika umasikini hadi utajiri, pengine lugha ya kitabu ingesadifu walengwa yaani masikini wa Tanzania.

Kutumia Kiingereza, lugha ngeni kwa Watanzania wengi masikini, kwangu ni kasoro niliyoiona katika upitiaji wa kitabu hiki.

Sehemu ndogo ya hadhira ya Watanzania ndio wanaoweza kunufaika na uhondo wa maarifa uliomo kitabuni. Tena hawa ni wale ambao rafiki yangu Moustapha Puya amewaeleza katika ukurasa wake wa Facebook kwa maneno yafuatayo: “Matajiri walioalikwa wao watakisoma na kufurahia tu kazi ya fasihi, kukosoa lugha na mpangilio wa sura na hata mwonekano wa jalada.”

Pengine ni busara kuhitimisha kwa kusema Kiswahili kingefaa zaidi kuandikia kazi hii na hata Diamond Jubilee pangefaa zaidi kuzindulia kitabu kuliko Serena Hotel!

Columnist: mwananchi.co.tz