Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sinema ya wanasiasa nchini inavyomuumiza mtazamaji

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Matukio ya kimaigizo kwenye tamthiliya mara nyingi humteka mtazamaji mpaka kuhisi anayoyatazama ni halisi, wakati ni maigizo tu. Anachokiona kwenye runinga huwa kimeandikwa na mtu au watu, kisha wahusika wanapangwa kabla ya kurekodiwa.

Hutokea mtu kutoa machozi kwa anachokiona kwenye runinga. Zipo nyakati matukio ya ndani ya kioo cha televisheni huwafanya watazamaji wawe na maumivu makali. Mathalan, mtoto anakuwa anapewa mateso makali au mwanamke mjamzito anasimangwa na kufanyishwa kazi ngumu.

Unapotazama mkusanyiko wa matukio ya wakati wa kurekodi ambayo huitwa behind the scene, utaona kwamba wakati wa mateso, mtesaji na mteswaji walikuwa wanacheka au hata kukosoana. Anayeteswa anamsahihisha anayemtesa ili amtese vizuri na kujenga uhalisia kwa mtazamaji.

Kumbe sasa, mtazamaji huumizwa na hata kutoa machozi kwa kuona matukio ndani ya tamthiliya yamezidi mateso. Humhurumia anayeteswa au kunyanyaswa. Ni hisia tu za kutekwa na matukio, maana ukweli wa wazi ni kwamba watu huwa wapo kazini. Machozi ya mtazamaji ni furaha ya waigizaji, yaani mtesaji na mteswaji.

Unakuta mtu anasemwa ana roho mbaya sana, naye anafurahi kwa sababu anakuwa amefikisha maudhui inavyotakiwa mpaka kuchukuliwa ni tukio la kweli. Mwandishi wa filamu au tamthiliya, vilevile waandaaji na waongozaji, mtazamaji anapolia, wao hufurahi kweli. Maana lengo linakuwa limetimia.

Siasa kama tamthiliya

Siasa za Tanzania hivi sasa zinabeba sura ya tamthiliya. Matukio mfululizo yanajiri. Yenye kuonekana hayakidhi uzani wa ubongo kwamba huo ndiyo ukweli wenyewe. Pamoja na uhalisia wa kimatukio kujaa walakini, lakini wananchi wanaumia sana. Wapo kama watazamaji wanaoshuhudia mtoto akinyongwa kwenye runinga.

Ni wakati ambao Watanzania wanahitaji sana kuoneshwa matukio nyuma ya kamera. Waone kile hasa ambacho hujiri hatua kwa hatua mpaka mwanasiasa kufikia uamuzi wa kuhama chama kimoja kwenda kingine. Hitaji hilo linakuwa kubwa kwa sababu yenye kuonekana yanabeba tafsiri ya kiini macho kuliko hali halisi.

Ipo dhana kutoka kwa wanasaikolojia na wataalamu wa ukaguzi wa uadilifu kupitia mtindo wa maisha ya watu, yaani lifestyle audit, kwamba kipindi cha wiki mbili ni kikubwa mno kutosha kumfanya binadamu awe wa tofauti. Hata hivyo, katika siasa za Tanzania hivi sasa, hasa kwa vyama vya upinzani, kipindi cha saa 24 ni kikubwa mno.

Madiwani wanahama kwa kasi kubwa. Wananchi wanarudishwa kwenye uchaguzi mara nyingi kuliko wakati wowote kwenye historia ya nchi. Ilizoeleka uchaguzi mdogo unafanyika kwa sababu wabunge au madiwani kutenguliwa ushindi wao na mahakama au kufikwa na mauti, siku hizi wanajiuzulu wenyewe.

Kwa kawaida hakuna kitu ambacho mwanasiasa aliyeshinda hakipendi kama kurudishwa kwenye uchaguzi kabla ya wakati. Uchaguzi huwagharimu fedha nyingi wagombea, vilevile muda. Ni tofauti na wabunge pamoja na madiwani wa upinzani siku hizi, wao wakati wowote wapo tayari kurejea kwenye uchaguzi, tena wakijiuzulu kwa hiari yao.

Mbunge anapojiuzulu anafanya stahiki zake za ubunge zikome. Asilimia kubwa ya wabunge wanadaiwa mikopo. Halafu huyohuyo kwa sababu ya kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli, anaamua kuhama. Anahamia chama ambacho hana uhakika kama atakubaliwa au atakataliwa. Na akikubaliwa, ataingia gharama mpya kufanya kampeni aweze kushinda uchaguzi.

Juu ya hapo ni kwamba anayehama, chama anachohamia kinampokea kwa nderemo, hoihoi na vifijo. Chama kinavunja utaratibu wa kuchuja wagombea kwa kumpitisha mgeni aliyehamia bila kupingwa. Mchakato wote huo unapoufanyia tafakuri ya kina lazima ubaki na swali hili; haya yanatokea kama ajali au ni mipango?

Tuone nyuma ya kamera

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, kama alivyotambuliwa na upande wa Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad, Jumamosi iliyopita (Agosti 11), alitangaza kujiuzulu uongozi kwenye chama hicho, vilevile kujivua uanachama, kisha kuweka wazi nia yake ya kujiinga na CCM.

Februari 27, mwaka huu, yaani miezi mitano iliyopita, Mtatiro alifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza kwamba Serikali ilikuwa imetenga Sh10 bilioni kwa ajili ya kununua wabunge na madiwani. Alisema, huo ulikuwa mpango mahsusi wa kuua demokrasia.

Mtatiro alidai kuwa viongozi ambao walibainika kuendesha mpango wa rushwa ya kununua madiwani walipandishwa vyeo. Alisema huo ni ufisadi mkubwa mno kwa Serikali kutenga fedha za kununua wabunge na madiwani. Alieleza kwamba walifanya uchunguzi na kubaini kuwa mpaka hiyo Februari 27, Serikali ilikuwa imeshatumia Sh10 bilioni kununua wabunge na madiwani.

Juni 24, mwaka huu, Mtatiro akitumia kofia yake ya uongozi CUF, alifanya uchambuzi wa bajeti ya Serikali mwaka 2018-2019, na kukosoa vipaumbele vyake. Alisema, bajeti hiyo haijatoa mikakati ya kuinua sekta jumuishi ambazo zinaajiri watu wengi kama kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara na utalii.

Alisema kuwa kilimo ambacho kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania kila mwaka kinapangiwa bajeti chini ya asilimia mbili, na fedha zinazopitishwa na Bunge hazitolewi zote. Akaeleza kwamba uchumi hauwezi kukua kama Serikali haitaweka mikakati ya kuchochea sekta zinazoajiri watu wengi.

Jumamosi wakati anajivua uanachama CUF, alisema anakusudia kufanya siasa za maendeleo. Hivyo, anataka kushirikiana na Rais Magufuli. Wakati huohuo, mwezi mmoja na siku 18 kabla, alisema Serikali ya Rais Magufuli haiwezi kuleta maendeleo na kukuza uchumi. Hapo lazima kujiuliza; nini kimembadilisha Mtatiro ghafla?

Mtatiro ni mchambuzi wa siasa, uchumi na jamii kwa jumla. Amekuwa mstari wa mbele kuikosoa Serikali. Julai 5, mwaka huu, alikamatwa, akapekuliwa nyumbani kwake na simu yake kuzuiwa, akidaiwa kuandika mtandaoni maneno yenye kumshusha hadhi Rais Magufuli. Mwezi mmoja na siku sita baadaye, amegeuka mtiifu hasa. Lazima ujiulize kuna nini ambacho Watanzania wengi hawakioni?

Hapana, hii si bure

Aliyekuwa mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara, taarifa zake kwamba alikuwa njia moja kuhamia CCM zilipovuja, alikuwa mkali. Alisema yeye si mtu wa kununuliwa. Vilevile Waitara alikuwa mstari wa mbele kuwashambulia wenye kuhama kwa hoja kwamba wananunuliwa. Naye tayari alishatimkia CCM na anatarajiwa tena kugombea jimbo hilohilo.

Mbunge wa Hai (CCM), Godwin Mollel, kabla alikuwa Chadema. Na ilipoelezwa kuwa kulikuwa na mpango wa yeye kujiuzulu ubunge ili ahamie CCM, alitishia kuwapeleka mahakamani watu waliosema maneno hayo aliyoyaita ni ya uzushi. Muda ulipowadia Mollel alihama, akajiunga CCM, akagombea tena na kushinda.

Mshindi wa kiti cha ubunge na udiwani atamani arudi kwenye uchaguzi, kisha aingie gharama mpya. Uchaguzi unagharimu mabilioni ya shilingi kwenye jimbo moja, lakini mbunge haoni woga fedha hizo kuteketea. Serikali nayo haiumii kuona fedha za umma zinatumika kwa wingi kugharamia uchaguzi ambao iliwezekana kuuepuka.

Uchaguzi nao unapofanyika hali inakuwa mbaya. Watu wanaumizwa na hata kusababisha vifo. Gharama zote hizo zinaingiwa kwa sababu ya utashi tu. Kwamba mbunge au diwani anakaa na kuwaza ni kwa nini asijiunge CCM ili awe mstari mmoja na Rais Magufuli? Mwisho anaamua kuhama. Eti bila ushawishi wowote. Hapana, kuna namna, si bure.

Juu ya kila kitu kinachoendelea, wanasiasa watambue kuwa wameigeuza siasa ya Tanzania kuwa tamthiliya isiyovutia. Hii hamahama inafanya tamthiliya hiyo ifikie sehemu mbaya ambayo watazamaji wanaumia, wananung’unika, wanaishia kusonya tu. Ni kama wanatazama kipande cha mateso ya mtoto. Pengine siku wakiona yaliyojiri nyuma ya kamera, watapata ahueni.

Columnist: mwananchi.co.tz