Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simulizi za watu walioishi miaka 100

90913 Pic+simulizi Simulizi za watu walioishi miaka 100

Mon, 6 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Aliyekuwa mkuu wa majeshi nchini, Jenerali David Musuguri ametimiza miaka 100, huku akimshukuru Mungu kwa kumuepusha na kifo cha risasi katika kipindi chote alichokuwa akilitumikia jeshi.

Jenerali Musuguru aliyezaliwa Januari 4, 1920 na kushiriki vita kadhaa ikiwamo vita ya pili ya dunia, alisema sasa atakufa na kuzikwa nyumbani kwao Butiama mkoani Mara.

Akizungumza kwenye ibada ya shukurani iliyofanyika nyumbani kwa Musuguri juzi, Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma, Michael Msonganzila alisema siri ya Jenerali Musuguri kuishi miaka 100 ni mazoezi ya kijeshi, nidhamu ya maisha na vyakula vya asili. Pia hofu ya Mungu ni siri nyingine iliyomfanya Jenerali Musuguri kuishi miaka mingi.

Askofu Msonganzila alisema maisha ya amani na heshima kuanzia ndani ya familia, serikalini na jamii ni miongoni mwa sababu nyingine za Jenerali Musuguri kuishi miaka 100.

Jenerali Musuguri ni miongoni mwa watu wachache duniani waliobahatika kuishi miaka 100 na zaidi.

Katika hali ya sasa ambako kuna maradhi kama saratani, Ukimwi, malaria na mengineyo pamoja na ajali, ni nadra kushuhudia mtu akiishi umri kama huo.

Ukiacha maradhi hayo na ajali, uwepo ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanatokana na mtindo wa maisha, nayo yanatajwa kuchangia watu katika miaka ya sasa kuishi miaka michache.

Hadithi za watu waliofanikiwa kuishi miaka mingi zinaelezwa kuwa ni kula vyakula vya asili, kufanya mazoezi pamoja na kufuata kanuni nyingine za maisha.

Unaweza kukuta mtu anatoka nyumbani kwa kutumia usafiri wake binafsi, akifika eneo lake la kazi na kupata kifungua kinywa, huendelea na kazi akiwa amekaa. Baadaye mchana hupata chakula na kuendelea na kazi mpaka jioni, kisha kurudi nyumbani kwa kutumia gari.

Ratiba ya mtu huyo kwa siku unaona haitoi nafasi ya kufanya mazoezi hata ya kutembea nusu saa kwa siku. Ni rahisi kupatwa na maradhi yasiyoambukiza.

Walioshi miaka mingi

Mzee Rashid Mkwachu, Baba mzazi wa mke wa Rais Mstaafu, Dk Jakaya Mrisho Kikwete, Mama Salma Kikwete ni miongoni mwa watu walioishi miaka mingi.

Mzee Mkwachu aliyekadiriwa kuwa ameishi kwa miaka 104 au 107, alifariki dunia Julai 19, 2018.

Msemaji wa familia, Ridhiwani Kikwete, alisema “Babu yetu alikuwa mzee sana, zamani utunzaji wa kumbukumbuku haukuwa mzuri, lakini anakadiriwa kuwa ameishi kwa miaka 104 au 107.”

Ridhiwani ambaye pia ni mbunge wa Chalinze alisema babu yake alikuwa mtu mwenye upendo kwa wajukuu zake, alipenda masuala ya kijamii na alikuwa mtu wa kufanya ibada.

Naye Masazo Nonaka kutoka mkoa wa Hokkaido nchini Japan, aliyekuwa akishikilia rekodi ya umri mkubwa duniani kwa mujibu wa kitabu cha rekodi za dunia cha Guinness, alifariki dunia akiwa na miaka 113, Januari 20, 2019.

Nonaka aliyezaliwa Julai 1905, kwa mujibu wa ripoti ya DW, aliishi umri mrefu zaidi kuliko mke wake na watoto wake watatu.

Japan inashikilia rekodi ya kuwa na watu wengi wanaoishi miaka mingi, kwani ina idadi kubwa ya watu walio na miaka zaidi ya 100.

Nchini Italia, Emma Morano aliyezaliwa Novemba 29, 1899 eneo la Piedmont, alifariki dunia akiwa na miaka 117.

Ilielezwa aliishi miaka mingi kutokana na maumbile ya jeni na chakula chake ambacho ni mayai matatu kwa siku, mawili yakiwa mabichi kwa kipindi cha zaidi ya miaka 90.

Alikiri kuwa kuishi kwake miaka mingi kulichangiwa na jeni kwa kuwa mama yake alifariki akiwa na miaka 91 na dada zake nao waliishi miaka mingi.

Nchini Indonesia, Mbah Ghoto ameishi miaka 146. Ameishi muda zaidi kushinda wake zake wanne, ndugu zake 10 na wanawe wote. Alifariki dunia mwaka 2017.

Daktari wake wa miaka 27 Carlo Bava, aliambia AFP kuwa hakuwa akila mboga wala matunda.

“Nimeishi muda mrefu kwa sababu nina watu wanaonipenda na kunitunza,” alisema Ghoto aliyekuwa akivuta sigara hadi mwisho wa maisha yake.

Mjukuu wake, Suryanto alisema kwa mujibu wa stakabadhi rasmi za serikali, Mbah Gotho alizaliwa 31 Desemba 1870.

Mjukuu wake huyo alisema mzee huyo huwa hana masharti mengi na huwa hahitaji chakula maalum.

Kauli ya Daktari

Dk Samwel Shita anasema watu wanaoishi muda mrefu ni wale wenye kinga nzuri za mwili ambazo zinawasaidia kujihami na magonjwa ya kuambukiza.

Anasema pia wale wanaofuata mtindo mzuri wa maisha, nao wana nafasi nzuri ya kuishi muda mrefu.

Anasema huenda Jenerali Musuguri ameishi umri mrefu kwa kuwa na mtindo mzuri wa maisha na kulingana na hadhi yake atakuwa anafanya uchunguzi wa afya yake mara kwa mara.

“Mtu akiwa na utamaduni wa kufanya check up (uchunguzi wa afya) mara kwa mara anakua katika nafasi nzuri ya kuchukua hadhari ya magonjwa kwa sababu kama itafahamika ana magonjwa hutibiwa katika hatua za awali,” anasema daktari huyo wa binadamu.

Anatoa mfano kuwa watu wengi wa Japan wanaishi umri mrefu kwa kuwa wanazingatia mwenendo mzuri na kanuni za maisha pamoja na kula vyakula ambavyo ni rafiki kwa mwili.

Anasema ili mtu aishi muda mrefu ni lazima awe na afya bora ya mwili kwa jumla, hivyo kuwa huru na magonjwa mbalimbali.

Anasema afya bora inatokana na mwenendo mzuri wa maisha ya kila siku ikiwamo kula vyakula bora pamoja na matunda na mboga za majani na kufanya mazoezi.

“Ulaji holela unachangia mtu kuwa na afya mbovu. Watu wanapaswa kuepuka matumizi ya tumbaku, pombe kupita kiasi na kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi,” anasema Dk Shita.

Dk Shita anasema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wanaofanya mazoezi mepesi kama kutembea, kuruka kamba nao wanaweza kuishi maisha marefu. Pia wanaotumia vyakula vya asili kama mboga za majani, dagaa na kutumia kiasi kidogo cha sukari.

“Watu wanashauriwa kuepuka kutumia vyakula vya kusindika pamoja na kula nyama nyekundu ili kujiepusha na maradhi,” anasema.

Anasema kwa ujumla ili mtu awe na afya njema anatakiwa kufuata mitindo mizuri ya maisha ikiwa ni pamoja na kujiepusha na ulaji holela, kupunguza mafuta, wanga na sukari.

“Pia chumvi ya mezani nayo si nzuri, watu wajiepushe na matumizi ya tumbaku kwani wanachangia aina mbalimbali za ugonjwa wa saratani pamoja na vyakula vya kusindika ambayo huwa na mafuta mengi,” anasema.

Anahimiza watu kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi mepesi ya mara kwa mara, ili kuepuka na kusema angalau kwa siku mtu atembee umbali wa kilomita mbili.

Anasema pia mtu anaweza kutembea kwa muda wa kuanzia nusu saa hadi saa nzima kwa siku tano za juma.

Shirika la Afya Duniani

Shirika la Afya Dunia (WHO) limesema kuwa umri wa kuishi kote duniani umeongezeka tangu mwaka 2000.

Ripoti ya Shirika hilo kuhusiana na takwimu za afya zinaonyesha kuwa wastani wa maisha ya binadamu umeongezeka kwa miaka 5.5 kati ya mwaka 2000 hadi 2016.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wastani wa umri wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 66.5 mpaka miaka 72.

Shirika hilo linasema wanawake wa Japan na wanaume wa Uswisi ndio wanaoishi muda mrefu zaidi kwa wastani wa miaka 86 na 81, huku Sierra Leone ikitajwa wanaume na wanawake ndio wenye maisha mafupi ya miaka 50.

WHO imeongeza kuwa ongezeko hilo la miaka mitano linatosha kubadili hali iliyoshuhudiwa katika miaka ya 1990 Afrika ya kupungua umri wa kuishi kutokana na Ukimwi na kwa Ulaya Mashariki kutokana na kusambaratika kwa muungano wa Soviet.

Shirika hilo linasema mabadiliko makubwa ya kuishi yako Afrika ambako sasa watu wanatarajiwa kuishi kwa wastani wa miaka tisa zaidi sababu zikiwa ni kuimarika kwa afya ya watoto, kudhibiti malaria na ongezeko la fursa ya kupata dawa za kurefusha maisha kwa wanaoishi na Ukimwi.

Hata hivyo, limesema wanawake bado wanawashinda wanaume kwa kuishi muda mrefu zaidi wastani ukiwa miaka minne na nusu zaidi baada ya kufikisha umri wa miaka 73.

Columnist: mwananchi.co.tz