Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Siku 66 za Dk Magufuli, 299 za Samia

Magufuliiiiiiipiccc Data Hayati Dk. John Magufuli

Thu, 16 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mwaka huu (2021), siku zake ni 365. Dk John Magufuli alitangazwa kuwa amefariki dunia Machi 17. Kutoka Januari Mosi mpaka Machi 17 ni siku 66.

Machi 17, Samia Suluhu Hassan alishika mpini wa kuliongoza taifa kama kaimu Rais. Kisha, Machi 19, Samia alikula kiapo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Fanya mgawanyo, katika siku 66 za mwaka huu, nchi ilikuwa chini ya uongozi wa Dk Magufuli. Kutoka Machi 17 mpaka Desemba 31, mwaka 2021 utakapokuwa unaondoka, kama kila kitu kitakwenda sawa, nchi itakuwa mikononi mwa Samia.

Hivyo, mwaka 2021 una ladha mbili tofauti za uongozi. Siku 66 za Magufuli na 299 za Samia. Na katika kipindi hiki tukielekea ukingoni mwa mwaka huu, si vibaya kuchambua ladha tofauti za uongozi.

Siku Rais Samia alipomsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya alitoa sababu kwamba alimuondoa kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma nyingi zinazomkabili.

Sabaya alianza kulalamikiwa tangu kipindi cha Magufuli lakini hakuchukuliwa hatua yoyote. Hivyo, hapa mapema kabisa taifa lilionja ladha tofauti ya kiuongozi kutoka alipoishia Magufuli.

Advertisement Uamuzi wa Rais Samia kuhusu Sabaya ulivutia hisia za wengi. Sabaya, anayetumikia kifungo cha miaka 30 hivi sasa, alikuwa na tuhuma nyingi. Malalamiko dhidi yake yalitolewa kila upande. Wanasiasa, wafanyabiashara hadi wakulima. Hata hivyo, ilionekana ilikuwa vigumu mno haki kutendeka dhidi yake kipindi cha Magufuli.

Mpaka hapo, Rais Samia akawa amechora alama ya kwamba yeye anasikiliza sauti za watu anaowaongoza. Sabaya ameshahukumiwa kifungo jela na bado ana kesi nyingine za ujambazi, utakatishaji fedha na kumiliki genge la uhalifu.

Mashehe 36 wa Uamsho walikuwa mahabusu kwa takriban miaka nane. Mashitaka yaliyokuwa yakiwakabili ni kujihusisha na vitendo vya ugaidi. Mengi yalielezwa kuhusu mashehe hao. Hoja kubwa ilijengwa nyuma ya viulizo; mbona kesi yao haisomwi? Kwa nini hawahukumiwi kama kweli mashtaka yapo?

Kwa waliopata kuwashuhudia mashehe hao wakipelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam walijionea namna ambavyo waliwekwa kwenye kundi hatari mno.

Ulinzi dhidi yao ulikuwa mkubwa na wa kuogofya. Zaidi, hawakutakiwa kutetewa. Watu waliojitokeza kutaka mashehe wa Uamsho watendewe haki, walipitia wakati mgumu.

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, mwaka 2017 alijaribu kuwasemea, akakutana na changamoto ya kuitwa polisi, akahojiwa.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Imamu Bukhary, Shehe Khalifa Khamis aliunga mkono kauli ya Lowassa, kuhusu mashehe wa Uamsho kutendewa haki. Sheikh Khalifa alikamatwa na polisi.

Zilipita nyakati kuonekana unawahurumia mashehe wa Uamsho ilikuwa jinai kubwa. Rais Samia, ndani ya siku zake 100, alithubutu kusikiliza kilio cha mashehe hao. Waliachiwa huru.

Rais Samia aliweka alama kubwa kwamba yeye siyo tu kiongozi mwenye usikivu, vilevile uongozi wake ni wenye kuheshimu utu.

Siku za mwanzo za Rais Samia ofisini, alionya kuwa hataki kodi za dhuluma. Alitoa kauli hiyo kufuatia malalamiko ya muda mrefu kwamba wafanyabiashara walikuwa wakibambikiziwa malimbikizo ya kodi na kupewa kesi za uhujumu uchumi. Rais Samia alitaka wafanyabiashara wasidhulumiwe, badala yake Wizara ya Fedha ilipaswa kutengeneza vyanzo zaidi vya mapato.

Hapa Rais Samia alithibitisha kuwa yeye ni msikivu, anayefuatilia malalamiko ya wananchi na kuyafanyia kazi. Huwezi kuwa kiongozi mzuri kama huachi masikio yako wazi ili ujue wananchi unaowaongoza wanazungumza nini.

Muhimu ni kuchuja unayoyasikia, yale yenye ukweli unayafanyia kazi, ya uzushi unayazingatia kwa namna ya kuhakikisha hayakuyumbishi.

Rais Samia hakuishia tu kusema hataki kodi za dhuluma, bali pia alienda mbele zaidi na kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuta kesi zote za kubambikia watu. Kutokana na msimamo wa Rais Samia, Takukuru walifuta kesi 47 za ubambikiaji.

Kisha, Rais Samia akataka polisi nao wafute kesi za ubambikiaji.

Kutoka alipotoa kauli hiyo, taifa limeshuhudia watu wakitolewa mfululizo. Sababu kubwa inayotolewa ni moja; Ofisi ya Mwendesha Mashitaka haina nia ya kuendelea na kesi. Hizi ni alama za uongozi wenye kuheshimu haki za binadamu, ambazo Rais Samia ameziweka kwenye siku zake zinazoelekea kutimia 299 katika siku 365 za mwaka huu.

Katika hotuba yake ya kwanza bungeni, Rais Samia alilitaka Bunge kufanya kazi yake ipasavyo. Aliomba wabunge wakosoe serikali anayoiongoza. Ni kipimo kingine kuwa hataki mapambio, bali yupo tayari kusikiliza ukweli. Kiongozi asiye msikivu hawezi kuruhusu kukosolewa.

Siku hiyohiyo alipokuwa anahutubia Bunge, Rais Samia alitaka watu wanaotangaza kuwa mtangulizi wake, Dk Magufuli aliuawa, wajitokeze na watoe ushahidi. Hapo alikuwa anajibu maneno yaliyokuwa yanasambazwa mtandaoni na baadhi ya watu kwamba Dk Magufuli aliuawa. Tuhuma hizo zilitaja mpaka majina ya waliowatuhumu kufanya mauaji.

Rais Samia alionya kuwa waliokuwa wanasambaza uzushi wa kuuawa Dk Magufuli, wasijidanganye kwamba wasingepatikana. Na kweli, baada ya kauli yake kumekuwa na utulivu. Akaunti za mitandao ya kijamii zilizokuwa zikitumika kufanya uenezi huo, siku hizi zipo kimya. Rais Samia hapa alizidi kuthibitisha kwamba anasikiliza yanayozungumzwa.

Rais Samia hataki Bunge lijadili mambo yasiyo na tija. Kuonesha kuwa anafuatilia mijadala ndani ya Bunge na hakupendezwa jinsi wabunge walivyokuwa wanalinganisha uongozi wake na ule wa mtangulizi wake, Dk Magufuli, alipata kuwaambia waziwazi kwamba walikuwa “wakidemka”. Alisema, wabunge walikuwa wakicheza ngoma za mitandaoni badala ya kufanya kazi yao.

Ni kwamba, Rais Samia alikuwa akifuatilia mitandao ya kijamii, kile kilichokuwa kikijadiliwa mtandaoni, kuwalinganisha Rais Samia na Magufuli, ndicho hicho kilichokuwa kinachukua nafasi kubwa.

Rais Samia aliwataka wabunge kuacha kudemka kwa ngoma iliyopigwa mitandaoni. Maana ni kweli, kilichokuwa kinaendelea mitandaoni, ndicho kilichochukua nafasi kubwa bungeni.

Kama Rais Samia asingekuwa mfuatiliaji na msikivu mtandaoni, hivyo kuunganisha na hoja za wabunge, asingekosoa kuwa wabunge walikuwa wanademka. Unapojadili hoja hii bila shaka unakuwa huwezi kupinga unapoambiwa kuwa Rais Samia ni mfuatiliaji, vilevile msikivu.

Katika siku zinazoelekea kutimia 299 za urais wa Samia, huwezi kusahau jinsi vyombo vya habari vinavyopumua. Siyo kwa mazingira aliyoyatengeneza, bali kwa tamko alilolitoa.

Rais Samia aliagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa viachiwe huru. Kauli hiyo haikuashiria chochote, zaidi ya kuonesha kuwa alitaka vyombo vya habari vifanye kazi yake na visibughudhiwe.

Ni siku 299 za usikivu na utu, lakini pia za ufunguzi kitaifa. Mengi yaliyokuwa yamefungwa awali, kwa sasa yamefunguliwa. Ni alama pia ya usikivu, huwezi kutambua kilichokuwa kimefungwa kama husikilizi. Upo uponyaji mkubwa unaonekana kipindi hiki.

Katika kila uamuzi ambao Rais Samia ameufanya ndani ya siku 299, utapata jawabu moja kati ya matatu; utamuona ni msikivu, ana utu, au anaiponya nchi. Hii ndiyo sababu asilimia kubwa ya watoa maoni wamekuwa wakitamka dhahiri kwamba kipindi hiki Watanzania wana furaha. Si uongo, na haihitaji utafiti mkubwa. Furaha ya Watanzania ipo dhahiri katika miezi tisa ya uongozi wa Rais Samia.

Rais Samia pia hafanyi kazi kwa kuendeshwa na presha za watu. Anasikiliza kisha anajiridhisha. Wapo wengi wameshutumiwa na wanaendelea kulalamikiwa kwenye Serikali anayoiongoza. Hata hivyo, hajawaweka kando. Yupo nao.

Waliokutana na rungu lake ni wale waliofanya makosa katika uongozi wake au alishajiridhisha.

Mara nyingi Rais Samia amekuwa na mtindo wa uongozi wa kuhamisha kuliko kutupa pembeni.

Anzia Dk Bashiru Ally, aliyemtoa kwenye ukatibu mkuu kiongozi hadi ubunge, ndivyo na wengine walivyopangiwa majukumu mengine. Ni wachache mno waliotemwa jumla. Rais Samia anasikiliza na anaponya kwa kutanguliza utu mbele.

Miezi 12 ya mwaka 2021, mitatu isiyotimia chini ya Magufuli, ina ladha ya miaka mitano kuanzia Novemba 5, 2015. Halafu tisa iliyotimia na kuzidi chini ya Samia, kama Mungu ataendelea kumruzuku afya, uhai na kumkinga na mitihani, nchi ipo tofauti.

Uhusiano wa kimataifa unastawi sasa. Si kama siku 66 za awali mwaka huu ambazo hazitofautiani na miaka mitano ya Magufuli.

Columnist: www.mwananchi.co.tz