Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sifa nne za shule bora kwa mwanao

11162 SIFA+PIC.png TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukiuliza swali shule nzuri ni ipi kuna uwezekano mkubwa ukajibiwa haraka haraka kuwa ni uzuri wa majengo, mandhari mazuri kama vile kuwapo kwa maua mazuri na mengineyo.

Hata hivyo, je kweli shule nzuri ni majengo yenye rangi nzuri, vioo, maua au kuna zaidi?

Kamusi ya Kiswahili iliyotolewa na TUKI 2005, inaainisha kuwa shule ni mahali ambapo mchakato mzima wa kutoa maarifa unaendeshwa.

Ni mahali ambapo elimu inarithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine kupitia mbinu na mafunzo maalumu.

Kwa hiyo, ili sehemu yoyote iitwe shule inabidi kuwe na mchakato wa mafunzo yenye kuwapatia wanaojifunza maarifa waliyoyalenga.

Bila kuwa na mchakato huu, eneo hilo halistahili kuitwa shule hata kama mandhari yake yatakuwa ya kuvutia namna gani.

Ndiyo maana kuna majengo mengi ya kifahari lakini hayaitwi shule. Na wanafunzi hawaendi katika majengo hayo, maana siyo shule.

Nini kinafanya jengo kuwa shule?

Watu wengi waliofanya utafiti katika mataifa mbalimbali, wanakubaliana kuwa shule nzuri inapimwa kwa kuangalia kiwango cha utoaji wa maarifa na stadi za maisha.

Maarifa na stadi hizo ndio malengo ya elimu na kiini cha mchakato mzima wa kujifunza na kufundisha.

Wazazi na jamii huwapeleka watoto shule wakitaraji kuwa watapata uwezo unaotokana na maarifa watakayoyapata kutoka shuleni. Si rahisi kama kuna wazazi wanaopeleka watoto shule ili wakashuhudie uzuri wa mandhari ya shule. Matarajio yao ni kuwa watapata uwezo utakaowafanya wakabili changamoto za maisha na kutatua matatizo yanayowazunguka.

Malengo haya ndiyo yanayowafanya wazazi kukwepa kupeleka watoto kwenye maghorofa makubwa na majengo ya kisasa yasiyoitwa shule. Hii ni kwa vile huko hakuna mchakato wa kujifunza ingawa majengo yanavutia.

Sifa za shule nzuri

Kama kitu kinachoifanya sehemu iitwe shule ni mchakato mzima wa kujifunza, basi shule nzuri tunaitambua kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

Kwanza, kuwepo na walimu wa kutosha na wenye taaluma na utaalamu katika mbinu za ufundishaji. Walimu wanaojua saikolojia ya utambuzi wa uwezo wa watoto. Walimu wanaojua mbinu shirikishi zinazotambua uwezo wa watoto.

Hii itawachochea watoto kuwasikiliza na kupata maarifa na muda zaidi wa kuonyesha uwezo na fikra zao.

Inabidi kuwe na walimu wanaopenda kazi yao, wanaojituma na kujiheshimu; wanaofikiri zaidi mbinu za kuboresha kazi zao na kujiboresha wenyewe.

Inabidi wawepo walimu wanaopenda kujiendeleza kitaaluma na wanaoonyesha juhudi za kujua yanayotokea katika jamii yetu na kwingineko ili kuyatumia..

Inabidi wawepo walimu wasio na chuki wala visasi kwa wanafunzi; wanaojua madhara ya uadui kati ya mwalimu na mwanafunzi ili kujenga mazingira salama kwa watoto.

Shule nzuri ni ile inayoamsha vipaji na ubunifu kwa watoto kwa kuwapa vichocheo vya ubunifu. Huwatembeza watoto katika maeneo yenye vitu halisi kama vile milima, maeneo ya kihistoria na mengineyo, ili wakazie maarifa kwa kuona vitu halisi.

Pili, ni shule yenye vifaa vya kufundishia na kujifunzia kama vile vitabu, ramani, maumbo mifano, maktaba yenye vifaa. Pia viwanja vya michezo na maeneo au vifaa vinayowasaidia watu wenye ulemavu kupita na kufanya kazi zao kiurahisi.. Je shule zetu zina vifaa hivyo ili tuziite nzuri?

Tatu, shule nzuri ni ile yenye uongozi thabiti, unaobuni mbinu mpya za kuboresha uhusianao wa walimu na wanafunzi kila siku. Pia, kuwe na uongozi unaothamini taaluma na kuweka kipaumbele taaluma ya watoto kuliko miradi, tafrija na semina zinazopoteza muda mwingi.

Nne, ni shule yenye utamaduni shirikishi ambapo wazazi, walimu na wanafunzi wanashirikiana katika mchakato mzima wa kuboresha elimu kwa watoto.

Bodi za shule, kamati za shule na sikukuu za wazazi zinafanyika ili kupeana mawazo mapya yatakayoboresha utendaji shuleni. Je, ni shule ngapi hapa kwetu zina utamaduni shirikishi unaowaweka wazazi, walezi na walimu pamoja?

Kuitambua shule nzuri kwa kuangalia uzuri wa majengo au wingi wa watoto darasani ni mtazamo hasi. Hili ni tatizo kwa wazazi na walezi wengi ambao aghalabu hutafuta shule kwa kuzingatia wingi wa watoto, magari mazuri yanayowapeleka shule, ubora wa majengo au mandhari ya shule. Haya ni muhimu, lakini bila elimu ni kazi bure.

Wazee wetu walisomea chini ya miembe miaka ya nyuma, lakini ni wabunifu na watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri na jamii inafaidika nao.

Lakini hivi sasa watoto wanahitimu kwenye shule kubwa za kifahari na kujiunga na makundi mabaya au kuwa tegemezi katika familia. Mzazi gani anapenda kuona mtoto wake anahitimu kichwani hana kitu japo amesoma shule yenye mandhari nzuri?

Si vyema kuendelea na mtazamo hasi wa kuchukulia shule nzuri kwa kuangalia ubora wa majengo tu au wingi wa watoto walioandikishwa.

Columnist: mwananchi.co.tz