Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Siasa zetu zilenge kuujenga uchumi wa nchi ya tanzania

9533 Pic+siasa TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tunaweza kusema kwamba ni bahati mbaya taifa letu liliingia kwenye mfumo wa siasa wa vyama vingi kabla ya kukubaliana vipaumbele vya taifa letu. Kwamba tunaweza kutofautiana kwa mawazo, itikadi na sera lakini kuna tunu za taifa ambazo ni lazima kushikamana kuzilinda na kuzitetea kwa nguvu zote hadi uhai wetu.

Bahati mbaya hii imezalisha mawazo ya kuvitukuza vyama vya siasa kuliko “utaifa” wetu. Imezalisha ushabiki, mahaba, mipasho, vijembe na ubaguzi. Na watu wanaweka nguvu kubwa kuvijenga na kuvilinda vyama vyao vya siasa zaidi wanavyolijenga taifa lao au zaidi wanavyoujenga uchumi wa taifa letu.

Kujenga uchumi ni kazi ya kila Mtanzania. Kujenga uchumi ni kazi ya pamoja, panahitajika mchango wa kila mmoja katika kuujenga uchumi wa taifa letu. Uchumi imara ni nguzo ya taifa, uchumi imara unatufanya kuwa huru zaidi na kujiamini; uchumi imara utawafukuza maadui zetu wakubwa: Ujinga, magonjwa na umaskini. Na kujenga uchumi imara kwenye dunia ya leo, dunia ya utandawazi, dunia ya ubabe ni lazima kuwa wapole kama njiwa, lakini wajanja kama nyoka. Hapa muhimu ni lazima kutambua kwamba upole huu wa njiwa na ujanja huu wa nyoka ni lazima uwe ni wa wote, si wa mtu mmojammoja.

Njiwa, anachukuliwa kama ishara ya upole, amani na upendo. Kuna utamaduni wa kuwaachia njiwa kuruka wakati wa tukio la amani au ushindi. Wakristo wanaamini Roho Mtakatifu anashuka katika umbo la njiwa. Nyoka ni mjanja na hatari. Wakati mwingine anaonekana kuwa na akili hata ya kumzidi binadamu, Tunakumbuka simulizi ya jinsi nyoka alivyowadanganya Adam na Hawa.

Dunia ni kijiji kimoja

Ni kweli kwamba dunia sasa hivi imekuwa kijiji kimoja? Kwa vigezo gani? Lakini basi, hakuna mwenye uwezo wa kupinga jambo hili sasa hivi, utaitwa kichaa. Tukubaliane kwamba dunia ni kijiji kimoja, kijiji ambacho wajanja wanaishi kwa anasa na wapole wanauzwa mnadani kama njiwa! La msingi, ili tuweze kuishi kwenye kijiji hiki ambacho kinaelekea kuwa pango la wanyang’anyi, ni lazima kuishi kwa ujanja. Kama hatuna nguvu ya kuukataa Utandawzi, hatuna nguvu ya kuikataa IMF na Benki ya dunia, basi tuume na kuvuvia; tuwe wapole kama njiwa na kuwa wajanja kama nyoka. Kinyume na hapo kile kitendawili cha uchumi kukua na umasikini kuongezeka kwa kasi ya kutisha hakitateguliwa milele!

Miaka mitatu iliyopita, nilimtembelea mkulima mmoja katika kijiji cha Nyamigere-Biharamulo. Mkulima huyu alikuwa anafanya biashara ya kununua na kuuza mtama. Nilipoingia nyumbani kwake nilimkuta anakazana kusugua kopo la ujazo wa kilo mbili ili kuondoa maandishi yaliyokuwa kwenye kopo hilo, Yakiwa na maandishi wateja wangu watatofautisha kopo la kuuzia na kununulia, alinielezea mkulima huyo. Alikuwa na makopo mawili yaliyoonekana kulingana lakini yalikuwa tofauti. La kununulia lilikuwa na ujazo wa kilo tatu, lakini yeye anaponunua kwa mteja kopo hilo linakuwa la kilo mbili! Kopo la pili ambalo lilikuwa la kuuzia, lilikuwa na kilo mbili pungufu kidogo. Bei anayonunulia kilo mbili ambazo ni “tatu” ni ile ile anayouzia kilo “mbili” ambazo kusema ukweli zinakuwa zinapungua. Mkulima huyo alinielezea kwamba huo ni ujanja wa kupata faida. Bila ujanja huo hawezi kupata faida katika biashara ya kuuza mtama!

Ujanja kwenye vipimo

Wale wanaonunua mazao vijijini, mfano kahawa, mahindi na maharagwe. Debe lao moja unaweza kujaza madebe matatu ya kawaida! Madebe haya yana jina la “Balimanyaila”, ikiwa na maana ya “Itawachukua muda kugundua ujanja wetu”. Kuna watu waliotajirika na kuendelea, na bado wanaendelea kutajirika kwa kutumia mfumo huu wa “Balimanyaila”.

Hata ukiingia kwenye Benki zetu, utakuta bei tofauti za kuuza na kununua pesa za kigeni. Mfano dola ni ile ile, lakini thamani yake ya kununulia inatofautiana na ile kuuzia. Kwenye benki ile ile na wakati ule ule! Wataalamu wa uchumi wana lugha ya kuelezea muujiza huu! Ni ujanja wa kutaka kupata faida. Si kitu kibaya kupata faida, ila faida ni lazima iwe pande zote mbili; au kwa maana nyingine, ujanja ni lazima uwe pande zote mbili – kinyume na hapo faida inazaa ziada: Ziada inaleta kishawishi cha kutaka ZIADA zaidi: ZIADA zaidi ni hatari! Inazaa Unyang’anyi. Aliyenacho anataka awe na zaidi na anajitahidi kuunda mifumo ya kulinda njia zake za kuleta ziada; yuko tayari kulinda njia zake kwa gharama yoyote ile! Ikifikia hapo, huwezi kukwepa vita!

Hivyo ni muhimu kupanga upole na ujanja wa taifa. Ni muhimu kuujenga uchumi wa taifa letu kwa pamoja, pamoja na tofauti zeuti za kiitikadi, kisera na mahaba ya vyama vya siasa, ni muhimu na lazima kulinda kwa ghrama yoyote uchumi wa taifa letu ambao kwa vigezo vyote ni tunu ya kutulinda sisi na vizazi vyetu. Nchi zote ziliizoendelea zinahakikisha upole huu na ujanja huu unafanyika kwa pamoja na lengo moja.

Nyerere na IMF

Wale ninaolingana nao na wale wanaonizidi umri, wanakumbuka vizuri mapambano ya Mwalimu Nyerere na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Mwalimu, alikuwa anakataa sharti la IMF, la kushusha thamani ya shilingi ya Kitanzania. Aliujua ujanja na upole wa IMF. Wataalamu wetu wa Uchumi wa enzi hizo, walimshauri kukubaliana na masharti ya IMF.

Mwalimu, alikataa katika hotuba yake kwa taifa alitetea msimamo wake kwa kuwalinganisha wataalamu wa uchumi na waganga wa kienyeji, alisema, waganga wa kienyeji wana uwezo wa kutibu, dawa zao zinafanya kazi, lakini ili uwaone kuwa ni wa muhimu na wana uwezo wa kufanya miujiza wanavaa vitu vya ajabu kichwani, wanazungumza lugha isiyojulikana na kutengeneza mazingira yanayowazunguka yaonekana ya kutisha, wakati mbwembwe zote hizo hazina uhusiano wowote na dawa ya kutibu magonjwa, wanaweza kukutibu bila mbwembwe hizo!

Mwalimu, aliamini kwamba uchumi, unaweza kuelezeka kwa lugha ya kawaida ambayo kila Mtanzania anaweza kuilewa. Kwa maoni ya Mwalimu, mbwembwe zote zinazoufunika uchumi, IMF, Benki ya Dunia na Utandawazi ni ujanja tu kama ule wa waganga wa kienyeji.

Kinachofanyika, ambacho ni lazima kila mtu anayeishi katika dunia hii kukizingatia ni ule msemo tunaousoma kwenye misahafu, kuweni wapole kama njiwa na kuwa wajanja kama nyoka!

Katika lugha ya kawaida uchumi ni sayansi ya kuzalisha, kusambaza (kuuza na kununua) na kutumia mali. Neno la kuleta utata kidogo katika ufafanuzi huu ni sayansi. Kwa lugha ya kawaida tunaweza kuilezea sayansi ni elimu inayotokana na uchunguzi, majaribio, vipimo na kuthibitishwa kwa muda uliopo. Tukizingatia kwamba elimu ni mafunzo, masomo au ujuzi fulani; maarifa au hekima!

Katika maisha ya kila siku tunazalisha, tunasambaza na kutumia mali. Hakuna mtu anayeweza kuzalisha kila kitu na kujitosheleza. Katika hili mtu anamhitaji mtu, kijiji kinahitaji kijiji, wilaya inahitaji wilaya, mkoa unahitaji mkoa na nchi inahitaji nchi. Na katika mchakato huu mzima tunatafuta faida na ziada. Mjanja zaidi anapata faida kubwa ninasema ujanja, maana katika kuuza na kununua hakuna ugomvi, hakuna anayemvamia mwenzake na kumnyang’anya mali yake kwa nguvu. Kinachotumika ni upole wa njiwa na ujanja wa nyoka.

Wale wanaonunua mazao vijijini, mfano kahawa, mahindi na maharagwe. Debe lao moja unaweza kujaza madebe matatu ya kawaida. Madebe haya yana jina la “Balimanyaila”, ikiwa na maana ya “Itawachukua muda kugundua ujanja wetu”. Kuna watu waliotajirika na kuendelea na bado wanaendelea kutajirika kwa kutumia mfumo huu wa “Balimanyaila”.

Mwalimu Nyerere alikuwa anakataa kushusha thamani ya shilingi kwa kukwepa ujanja wa “Balimanyaila”. Mashirika kama IMF na Benki ya Dunia ni mtindo ule ule wa “Balimayaila”. Jambo linalosikitisha na ndicho kichocheo cha kuandika makala haya, Hata wataalamu wa uchumi wa Taifa letu, hawakumwelewa Mwalimu.

Wachumi wako wapi? Leo hii mtu anaweza kujiuliza wachumi wetu wako wapi? Kwanini wasibuni mbinu za kuliokoa taifa letu? Kwanini wasitufundishe kuwa wapole kama njiwa na kuwa wajanja kama nyoka? Na wakasisitiza kwamba hili ni letu sote kwa maana vyama vyote vya siasa na hata wale ambao hawana vyama vya siasa. Uchumi ni lazima ujengwe na watu wote.

Sayansi ya kuzalisha, kusambaza na kutumia mali ina wataalamu. Tanzania ilishakuwa na mchumi anayeheshimika dunia nzima. Ni imani yangu kwamba hata sasa hivi tuna wachumi wanaoheshimika na wenye uwezo mkubwa. Kama kweli hawa wamesoma na kupata elimu ni lazima watusaidie kubuni njia za “Balimanyaila”. Watafute ujanja wa kutembea na mashirika kama IMF na Benki ya dunia tuipokee misaada lakini kwa ujanja wa kitaalamu tutumie misaada hiyo kutengeneza mfumo wetu wa kuzalisha, kusambaza na kutumia mali.

Wachumi wetu wamezama kwenye vitabu na utafiti. Kazi kubwa wanayoifanya ni ile ya kuendelea kuyanufaisha mashirika ya IMF na Benki ya Dunia. Sasa wakati umefika wa wachumi wetu kuzama kwenye vitabu na kufanya utafiti wakilenga kulisaidia taifa letu kuendeleza uchumi wetu. Na kwa bahati nzuri Rais John Magufuli amewaingiza wasomi hawa kwa wingi kwenye Serikali. Watumie nafasi hii kubadiilisha mawazo ya Watanzania, wasifanye makosa yaleyale ya kuvaa sare za chama na kuimba wimbo ule ule. Mashirika ya kimataifa hayawezi kutusaidia kama yameshindwa kwingineko itakuwa Tanzania? Miaka kumi iliyo mbele yetu ukiangalia vizuri yale yanatokea katika mfumo wetu wa uchumi tutashuhudia kukwama kiuchumi kama nchi zote zilizokumbatia masharti ya IMF. Wakati ni huu vinginevyo kizazi kijacho kitaifukua mifupa yetu na kuichoma moto kwa hasira.

Padre Privatus Karugendo.

+255754633122

[email protected]

Columnist: mwananchi.co.tz