Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Siasa za chuki, ghiliba ubatili mtupu karne ya 21

64547 Siasa+pic

Thu, 27 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unaweza ukasema kuwa ni ujuha na upofu wa kisiasa kwa baadhi ya watu kuendelea kuamini katika siasa za chuki na ghiliba ndani ya karne hii ya 21. Haya mambo hayana mashiko katika ustawi wa maendeleo ya watu na taifa lao.

Siasa za chuki na ghiliba zimepitwa na wakati ndani ya Afrika na ulimwenguni kote. Hazifai kusikika wala kuwepo ndani ya karne hii.

Siasa za namna hii huzalisha ukosefu wa utengamano na maelewano na hupumbaza fikra za uzalendo na kuzalisha itikadi kali na chonganishi kati ya mtu na mtu na kabila kwa kabila.

Historia ya kisiasa inatukumbusha miaka ya 1980, siasa za chuki zilivyoweka alama isiyofutika nchini Sierra Leone na Liberia (1989-1996, 1999-2003) kutokana na siasa zao za uchuki na ghiliba zilizowagonganisha watu wa mataifa haya na kuleta machafuko ya umwagaji damu.

Hakuna siri kwamba siasa za namna hii hazijengi zaidi ya kubomoa utaifa na undugu, pia hupalilia uhasama, uasi, na kuibua visasi baina ya mtu na mtu na chama na chama.

Yaliyotokea Rwanda na Burundi si kwamba ni mipango ya Mungu, hapana ni hila za watu wachache waliojenga chuki za kisiasa na matokeo yake yakatokea mauaji ya kikatili.

Pia Soma

Pamoja na ubaya wake, siasa za chuki na ghiliba kwa sasa ziko wazi na zinaanza kumea kwa kasi ya ajabu ndani ya jamii zetu za Kiafrika na Tanzania ikiwa miongoni mwake.

Ni bahati mbaya siasa na namna hiyo zimeanza hata kwa vijana wanaotegemewa na taifa katika ustawi wake. Kundi la vijana likitumia mitandao ya kijamii, unaona jinsi linavyoweza kuleta madhara katika siasa zetu.

Tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020 mambo ya ajabu yameanza kujionyesha hususani kwenye mitandao ya kijamii ambayo inatumika kutengeneza propaganda za chuki dhidi ya baadhi ya watu, jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani ya nchi.

Vijana wameanza kuwanadi watu wao na kuwabeza wengine kwa tofauti za dini na makabila yao.

Aidha, lugha zinazotumika katika kujenga hoja ni zile zisizokuwa na staha. Vijana wanakwama kwenye uvumilivu wa ujengaji wa hoja wanasahau kanuni kwamba hoja hujibiwa kwa hoja na si kwa kutumia lugha ya matusi kama mbadala wa kujibu hoja, huo ni udhaifu wa kiitikadi katika kujibu hoja za msingi.

Kwa nyakati tofauti, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amekuwa akiongelea chuo cha chama kitakachowanoa makada wa chama hicho, hatua ambayo kwa jinsi hali ilivyo ni ya muhimu mno.

Vijana wote wanastahili kupikwa kisiasa bila kujali itikadi za vyama vyao kwa sababu hoja zinazojengwa mitandaoni na vijiweni ni za chuki na ghiliba na zenye ukosefu wa maadili na malezi ya kisiasa.

Tusipofanya hivyo tukaendelea na siasa za chuki na ghiliba tuna hasara kubwa katika siku za usoni.

Pia, siasa za chuki na ghiliba zinatanuka katika siasa za upinzani. Tanzania iliridhia mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1992. Lakini kwa sasa upinzani unalalamika kuonewa na Serikali, jambo ambalo limezaa chuki na visasi miongoni mwa wafuasi wake.

Tunashuhudia mnyukano mkali kati ya wafuasi wa upinzani na CCM, makundi haya mawili yanashambuliana kwa vijembe, matusi na kejeli. Inawezekana suala hili likaonekana ni dogo na la kawaida lakini si kweli, chuki hizi badaye zinaweza kuwa kidonda kisichokuwa na tiba.

Ili kupata suluhisho la kudumu ni lazima tuwe na siasa zenye fursa sawa kwa vyama vyote.

Ni wajibu wa kila mtu kusimama na kupinga hila na chuki zinazoweza kutufarakanisha na kutuingiza kwenye machafuko hasa ubaguzi na uonevu.

Pia, ziwepo siasa zinazotoa uhuru wa kutoa maoni kulingana na Katiba yetu (ibara ya 18), hivyo vijana wakajenga desturi na utamaduni wa kutumia uhuru wao kikatiba kujenga hoja na kukosoa kwa misingi huku wakilinda uhuru wa watu wengine.

Columnist: mwananchi.co.tz