Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Siasa Afrika Mashariki njiapanda

13760 Pic+afrika TanzaniaWeb

Sat, 25 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati mfumo wa vyama vingi ukikaribia kufikisha miongo mitatu, siasa za nchi za Afrika Mashariki zipo njiapanda huku kila nchi ikiwa katika changamoto zake.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa na jamii waliozungumza na Mwananchi wametaja kuwapo kwa dalili za kurudi nyuma kuelekea demokrasia kutokana na matumizi ya nguvu badala ya ushindani wa hoja.

Wachambuzi hao wametoa maoni hayo wakati mikutano na maandamano kwa vyama vya siasa vikidhibitiwa nchini, viongozi wa upinzani Uganda wakiwa wanafunguliwa mashtaka ya uhaini huku siasa za Kenya zikilenga uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Wakati mwanasiasa mkongwe Njelu Kasaka akisema siasa za ukanda huo zimekuwa zinarudi nyuma na kukumbatia mambo ambayo tayari yamelaaniwa, mwanahabari na mchambuzi wa masuala ya kijamii, Maria Sarungi amesema ni kutokana na nchi hizo kuwa na mifumo dhaifu kuliko viongozi.

Hali ilivyo Tanzania

Suala la kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa na maandamano tangu utawala wa awamu ya tano ulipoingia madarakani, limekuwa changamoto miongoni mwa wanasiasa huku vyama vya Chadema na ACT Wazalendo vikifungua kesi mahakamani kupinga hali hiyo.

Hata hivyo, viongozi wa Serikali na CCM wamekuwa wakisema mikutano haijazuiwa, bali vyama vya siasa vinaruhusiwa kufanya mikutano ya ndani huku wabunge na madiwani wakiruhusiwa kufanya mikutano katika majimbo na kata zao.

Jambo hilo limezidisha kibano kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa, wanaotaka kufanya mikutano na wanachama wao sehemu mbalimbali nchini.

Mbali na vyama vya siasa, changamoto nyingine ni kuzuiwa kuonyeshwa kwa vipindi vya moja kwa moja vya Bunge tangu Februari 2016.

Hofu zaidi ilitanda baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Huduma za Habari; Sheria ya Takwimu za 2016 na Sheria ya Makosa ya Mitandao ya 2015 zinazoweka majaribuni uhuru wa wananchi kutoa maoni yao huku pia vyombo vya habari vikilalamika kubanwa.

Jambo jingine ambalo limetawala siasa za Tanzania ni madiwani zaidi ya 150 na wabunge watano wa upinzani kuhamia chama tawala wakitoa sababu kuwa wanakwenda kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli.

Siasa za Uganda

Mbali na Tanzania, hivi karibuni nchini Uganda ambayo imeongozwa na Yoweri Museveni tangu mwaka 1986, mambo yamepamba moto baada mbunge ambaye pia ni mwanamuziki mashuhuri, Robert Kyagulanyi maarufu ‘Bobi Wine’ kukamatwa akidaiwa kukutwa na silaha kinyume cha sheria.

Kushikiliwa kwa Bobi Wine kumezusha hasira nchini humo na miongoni mwa wasanii maarufu sehemu mbalimbali ulimwenguni wamelaani pia taarifa ya kupigwa vibaya akiwa kizuizini madai ambayo Serikali ya Uganda inakanusha licha ya kuwa alionekana akiwa hawezi kutembea mwenyewe.

Serikali ya Uganda inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka ndani na nje ya nchi hiyo la kumwachia huru mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 36 na kwa siku kadhaa sasa vyombo vya usalama nchini humo vimetumia nguvu kukabiliana na maandamano ya mitaani yaliyotaka kushikiliwa Bobi Wine kufikie mwisho.

Baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya wiki moja, Bobi Wine ambaye pia alidaiwa kupigwa na kujeruhiwa wakati akikamatwa, alifikishwa katika Mahakama ya Kijeshi ambayo ilimfutia mashtaka ya kukutwa na silaha.

Hata hivyo, baada ya kumwachia, alikamatwa tena na kushtakiwa katika mahakama ya kiraia kwa makosa ya uhaini.

Hati ya mashtaka inasema Bobi Wine na wenzake walijaribu kumdhuru Rais Museveni wakati wa mkasa uliotokea siku kadhaa zilizopita ambako msafara wa kiongozi huyo ulishambuliwa kwa mawe.

Hakimu wa mahakama hiyo katika mji wa Kaskazini wa Gulu, ameamuru mbunge huyo aendelee kushikiliwa mahabusu hadi Agosti 30 atakapofikishwa tena mahakamani pamoja na watuhumiwa wengine 34 walioshtakiwa kwa uhaini wiki iliyopita.

Kenya nafuu

Tofauti na Uganda na Tanzania, kwa kiasi fulani siasa za Kenya zimeonekana kulenga zaidi uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 kwa makundi mbalimbali kuanza kujipanga kwa uchaguzi huo.

Jambo ambalo halikutarajiwa na wengi ni mapatano kati ya Rais Uhuru Kenyatta anayetoka Muungano wa Jubilee na kiongozi wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga.

Raila na Kenyatta walikuwa katika msuguano mkali baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2017, licha ya Rais Kenyatta kushinda, alipingwa mahakamani na uchaguzi kuamriwa kurudiwa Oktoba 26.

Hata hivyo, Raila aliyekuwa kiongozi wa muungano wa Nasa alisusia uchaguzi huo na kama hiyo haitoshi aliamua kujiapisha Januari 30 jambo lililozidisha utata zaidi kutokana na viongozi wengine wa juu wa Nasa kutohudhuria ‘hafla’ hiyo hivyo kuonekana kama wamemsaliti.

Hata hivyo, baada ya miezi miwili ya misimamo mikali kutoka kwa chama cha Jubilee na muungano wa Nasa, Rais Kenyatta na Raila walifanya mkutano wa pamoja wa ghafla Machi 5 katika jumba la Harambee, wakikubaliana kuweka tofauti zao kando na kuliunganisha taifa.

Safari hii, viongozi wengine wa juu wa Nasa wakiongozwa na Kalonzo Musyoka walimuona Raila msaliti kwa sababu hakuwashirikisha katika mpango huo.

Lakini pia wadadasi wa masuala ya siasa wanasema, Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto amejikuta kama ametengwa licha ya matamanio yake ya kurithi kiti cha urais mwaka 2022.

Hali ikiwa hivyo, Ruto amejikuta akitajwa kinara wa vitendo vya rushwa nchini humo kutokana na matokeo ya utafiti ya taasisi ya Ipsos Synovate akiwa na asilimia 33 ya Wakenya waliohojiwa, huku yeye mwenyewe akidai kuwa utafiti huo umefadhiliwa na wabaya wake ukilenga uchaguzi wa 2022.

Maoni ya wachambuzi

Akizungumzia matukio ya kisiasa yanayotokea katika nchi za Afrika Mashariki, mwanasiasa mkongwe, Njelu Kasaka alisema siasa za ukanda huu zimekuwa zikirudi nyuma kutoka kwenye demokrasia hadi matumizi ya nguvu.

“Siasa za Afrika Mashariki zinarudi nyuma kwa sababu ya kufanyika kwa mambo ambayo tulikuwa tukiyalaani huko nyuma. Zamani Tanzania ilikuwa ikilaani vitendo vya kibabe vya nchi nyingine, lakini kinachofanyika sasa ndiyo hayo hayo,” alisema Kasaka.

Aliongeza: “Wakati nchi kama Kenya wakitatua matatizo yao kwa mazungumzo, sisi tunafuata nguvu za dola. Wakati tunaingia kwenye mfumo wa vyama vingi, tulikubaliana kubishana kwa hoja, lakini sasa kuna matumizi mengi ya nguvu ya dola kuliko hoja.”

Kasaka aliyekuwa kiongozi wa kundi la G55 lililokuwa likidai Serikali ya Tanganyika mwaka 1993 kabla ya kuvunjwa na Mwalimu Julius Nyerere, aligusia siasa za Uganda akisema zinaathiriwa na uongozi wa muda mrefu.

“Viongozi wakishakaa madarakani kwa muda mrefu wanajisahau, hicho ndicho kinachotokea Uganda,” alisema.

Lakini, Dk Emmanuel Malya wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania alisema kilichotokea Uganda kwa Bobi Wine ni kutokana na mfumo wa siasa wa nchi hiyo unaoruhusu wagombea binafsi.

“Kuna suala la vijana limejitokeza katika siasa za Uganda na pia nchi hiyo inaruhusu wagombea binafsi. Bobi Wine ni mbunge asiye na chama. Amekulia kwenye makazi duni na kwa kuwa ni mwanamuziki anakubalika sana na vijana. Ni tofauti na Tanzania ambapo wagombea huru hawaruhusiwi,” alisema Dk Malya.

Akichambua zaidi siasa za Afrika Mashariki, Maria Sarungi alisema demokrasia kwa nchi hizo inakumbwa na changamoto ya viongozi kutofuata sheria na taratibu zilizopo.

“Hilo linatokana na kile ambacho rais mstaafu wa Marekani, Barrack Obama alikizungumza hivi karibuni japo hakikupokewa vizuri; kuwa na taasisi imara badala ya viongozi imara,” alisema.

Aliongeza, “Katika suala la demokrasia, haki na usawa, endapo kiongozi akipata madaraka kwa haki au kwa kuchaguliwa au hata akipata kwa nguvu, anaingia madarakani akijua nchi ina sheria, Katiba, kanuni na taratibu mbalimbali. Japo zinampa nguvu, sheria hizohizo pia zinadhibiti madaraka yake.”

Alisema suala la viongozi kutofuata sheria limekita mizizi huku Umoja wa Mataifa ukifumbia macho viongozi hao na kusababisha wananchi wasio na uelewa kufanya vurugu.

Columnist: mwananchi.co.tz