Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Si jambo rahisi kupata mageuzi ya maana bila demokrasia, maelewano ya kitaifa

9263 Pic+democrasia

Wed, 1 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya vyama vya ukombozi vya Afrika – kikiwamo Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kuvifanya vyama hivyo kuendelea kuwa na mvuto kwa wananchi unaweza kuwa mgumu kwa mazingira ya kisiasa yaliopo nchini.

Mwishoni mwa mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa muda wa siku mbili hivi karibuni, CPC na vyama vya ukombozi vya Afrika vilikubaliana katika maazimio manne yanayolenga kuimarisha juhudi za vyama hivyo katika kuwaletea wananchi wao maendeleo ya kweli.

Maazimio hayo yalitolewa baada ya kugundulika kwamba kwa takribani nusu karne ambapo vyama vya ukombozi vimekuwapo madarakani vimeshindwa kuboresha maisha ya watu wao na hivyo kushindwa kukidhi mategemeo ya wengi tangu uhuru.

Mkutano wa mwaka huu kati ya vyama hivyo umetanguliwa na ule uliofanyika Beijing mwaka jana ambapo viongozi na mashirika ya kisiasa takribani 300 kutoka duniani kote yalikutana kujadili umuhimu wa kushirikiana katika kujenga dunia iliyo bora zaidi.

Maazimio ya mkutano

Miongoni mwa maazimio yaliofikiwa katika mkutano wa Dar es Salaam ni pamoja na uhitaji wa vyama vya siasa kuimarisha juhudi katika kubuni njia za kuwaletea watu wao maendeleo, zinazoendana na mazingira halisi ya nchi zao.

Pili ni umuhimu wa vyama vya siasa kutoa mchango wao kikamilifu kama nyenzo kuu za kujiletea maendeleo ya kitaifa.

Tatu vyama hivyo vilikubaliana kuweka mifano mizuri katika suala zima la mahusiano ya chama na chama yaliyojikita katika misingi ya kujifunza na kunufaika kwa pamoja. Na azimio la nne lilihusu kukuza mahusiano kati ya China na Afrika.

Katika mada yake wakati wa uhitimishaji wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alivikosoa vikali vyama vya kimapinduzi kwa kushindwa kufanya kazi kama hazina ya maarifa na msingi wa fikra za kimapinduzi.

Msomi huyo ambaye aliwahi kuwa mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alibainisha kuwa kwa miaka mingi vyama vya siasa vya Afrika vimekuwa vikifanya kazi kama “mitambo ya kutafutia kura” kwa gharama ya wananchi wa kawaida.

Maoni ya Dk Bashiru yaliakisi maoni ya wasomi na viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ambao hawakusita kuelezea kutokuridhishwa kwao na kushindwa kwa vyama vya ukombozi kutimiza mategemeo waliokuwa nayo wananchi wakati wa kupata uhuru.

Wanavyosema wachambuzi

Hapa nchini, wachambuzi mbalimbali wa masuala ya siasa na utawala wametanabahisha kuwa ili CCM, kama chama kikongwe cha ukombozi barani Afrika, iweze kuyatekeleza maazimio yaliyofikiwa, ni lazima ifanye mageuzi ya msingi katika nyanja mbalimbali.

Profesa Gaudence Mpangala, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), anasema kwamba China, ukilinganisha na Tanzania, ina mazingira tofauti ya kiuchumi na kisiasa ambayo CPC iliamua kuyafuata na hivyo itakuwa ngumu kutekeleza maazimio hayo kwa kuitumia China kama mfano.

Wakati China haikuiacha misingi yake ya kijamaa badala yake iliimarisha ili iendane na mazingira na mahitaji mapya ya wakati, “Tanzania ilitupilia mbali itikadi yake ya ujamaa na kujitegemea na kwa kasi ikajiunga na kiwewe cha uliberali mamboleo (itikadi inayopendelea soko huria na ushindani wa kisiasa,)” amesema Profesa Mpangala.

Sera za kiliberali mamboleo zilizoanzishwa rasmi nchini katika kipindi cha miaka ya 1980 zilileta ushindani katika siasa na nyanja za kiuchumi. “(Tanzania) ikaacha siasa za majadiliano za mfumo wa chama kimoja na kukaribisha siasa za ushindani wa kukata na shoka za mfumo wa vyama vingi.

“Mabadiliko yoyote yanayokusudiwa kuletwa ni lazima yajengeke katika misingi ya majadiliano na maelewano kati ya vyama vya siasa na asasi za kiraia, ambayo kwa sasa siyaoni yakifanyika.

“(Kwa hapa Tanzania) maelewano ni ya muhimu sana pamoja na uwepo wa dira imara ya kitaifa ambayo kila chama cha siasa kinachopata nafasi ya kuunda serikali kinaweza kuifuata,” anasema Profesa Mpangala.

Harakaharaka akatolea mfano wa Azimio la Arusha, ambalo limeuawa na kupelekea kuzaliwa kwa Azimio la Zanzibar, tukio ambalo limeicha nchi “ikienenda bila ya kuwa na mwelekeo wowote wa kitaifa.”

“Sitaki kupendekeza turudi kwenye mfumo wa chama kimoja,” anatahadharisha Profesa Mpangala. “Tunaweza kutumia mfumo huuhuu wa vyama vingi lakini uliojengwa katika misingi ya haki, nafasi sawa, kuvumiliana na kuheshimiana kati ya vyama vya siasa.”

Richard Mbunda, mhadhiri wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anakubaliana na Profesa Mpangala kwamba kuendesha mabadiliko yoyote ya dhati nchini hakutawezekana bila ya uwepo wa nia ya dhati ya kuaminiana na utayari thabiti wa mfumo wa vyama vingi.

Anaamini kwamba itakuwa ngumu kuwaletea watu maendeleo wanayoyataka katika nchi endapo chama kinachounda serikali kitashindwa kutambua mchango unaotolewa na vyama vya upinzani na wachambuzi wengine huru.

“CCM imeshindwa kutambua mchango wa wenzao kutoka upinzani,” anabainisha Mbunda akiongeza kuwa chini ya uongozi uliopo, vyama vya upinzani vinaonekana si vya kizalendo na hivyo hawana mamlaka ya kuzungumzia uendeshaji wa masuala ya nchi.

Ushauri kwa CCM

Kwa upande wake, mhadhiri wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Hamad Salim anashauri kwamba kama kweli CCM imedhamiria kuleta mabadiliko nchini basi ni lazima ikae chini na kutafakari ni nini haswa kilisababisha kufeli ambako katibu wake mkuu leo anakiri.

“Pia, lazima iendeshe vita visivyokwisha dhidi ya mabepari uchwara ambao hukitumia chama kwa maslahi yao binafsi,” amesema. “Kuna ulazima pia wa kukirejesha chama kwa wamiliki wake halali, watu.”

Dk Hamad, ambaye hata hivyo amepongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na mwenyekiti wa CCM Rais John Magufuli, anasema kufeli kwa vyama vya ukombozi vya Afrika katika kuwaletea watu wao maendeleo ndio bei inayopaswa kulipwa na vyama vinavyokiuka misingi ya uanzishwaji wake.

“Vimeacha kuwa vyama vya watu na kuwa vyama vya wasomi. Ni kujipumbaza kufikiri kwamba unaweza kuleta maendeleo ya watu nchini katika mazingira ya sasa ambapo kazi ya kusimamia uletaji wa maendeleo hayo ipo mikononi mwa watu binafsi badala ya taasisi.”

Dk Bashiru, hata hivyo anaahidi kuwa CCM itakwenda kutekeleza mageuzi yanayokusudia na anaamini ya kwamba mageuzi hayo yatasaidia kumkomboa mtu maskini. Yeye anaamini kwamba vita dhidi ya ukoloni haijaisha kwani kazi inayoikabili Afrika kwa sasa ni kupiga vita aina zote za unyonyaji.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na utawala bora barani Afrika wanakubaliana kwamba juhudi yoyote ya kufanya mageuzi ya kweli katika nchi zitafeli kama hakutakuwa na mijadala mipana kuhusu masuala nyeti ya demokrasi.

Demokrasia Afrika

Hata hivyo, barani Afrika kote kunaonyesha kusuasua kwa kasi ya ukuaji wa demokrasia na kumekuwa na wimbi la ukandamizaji wa haki za kiraia hali ambayo inaendelea kuchochea migogoro barani humo na kurudisha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo.

“Badala ya kuongoza vizuri, wanasiasa wako makini katika kuiba fedha ili watoe rushwa na kuiba kura ili warudi tena madarakani,” jarida maarufu la The Economist liliwahi kubainisha mwaka 2016. “Kasi ya ustawi wa demokrasia ni ndogo sana barani Afrika.”

Hivi karibuni, Rais mstaafu wa Marekani, Baraka Obama alikuwa na wasiwasi huo.

“Demokrasia inamaanisha kuwa karibu na kuguswa na maisha kama watu wanavyoyaishi katika jamii zetu, na hicho ndicho tunachopaswa kutegemea kutoka kwa viongozi wetu,” alisema Obama katika hotuba yake ya kuadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Nelson Mandela nchini Afrika Kusini.

“….na hii inatokana na kuandaa viongozi kutoka mashinani ambao wanaweza kusaidia kuleta mabadiliko na kuyatekeleza na ambao wanaweza kuwakabili viongozi waliojifungia kwenye majumba mazuri kuwa kujifungia huko hakusaidii kitu chochote katika jamii.”

Columnist: mwananchi.co.tz