Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Shurutishi au shirikishi?

49635 SHURUTI+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya kuona kwamba kuna msukumo tena wa kujadili masuala ya elimu, ebu niwape barua iliyoandikwa na rafiki yangu mwalimu.

Makengeza, shule bwana. Naona kuna mitindo miwili tu. Shurutishi na shirikishi.

Hebu nifafanue. Bado nakumbuka nilipokwenda kujiunga na shule kwa mara ya kwanza kama mwalimu. Hata kabla sijaenda, watu wakanipa pole maana shule ile ilifahamika kutokana na ukali wa mwalimu mkuu wake.

‘Yaani Bwana, yule mwalimu hamwogopi mtu. Anaweza kukuchapa viboko hata wewe na asipokupenda, unarudishwa wizarani moja kwa moja na bonge la barua ya kuonyesha usivyofaa. Nakujua na ukorofi wako kwa hiyo ujue kwamba huu ukorofi lazima uufiche chini ya manyasi kabisa maana utaumbuka, utakuja kukosa kazi.’

Kwa kweli niliona jamaa anatia chumvi hadi giligilani na pilipili kichaa.’

‘Haiwezekani Bwana. Kuna sheria ya elimu. Kuna kanuni. Hata kupiga, haruhusiwi kupiga hovyo.’

‘Ohoo! Hebu waulize wanafunzi. Wengine wana makovu hadi leo. Nakwambia, kimbelembele chako kitakuponza.’

Hapo ilibidi nichukue tahadhari kidogo, angalau nisiseme hadi niwe nimesoma vizuri hali ilivyo. Mmmh na hali yenyewe. Kweli mwalimu mkuu alitembeza viboko hadi alisababisha miti yote ikatwe apate fimbo za kutosha.

Upande wa wanafunzi usiseme. Wapo waliogopa fimbo zake hivyo wakajitahidi wasionekane kabisa. Wengine walimwomba Mungu wawe wafupi zaidi. Lakini wanafunzi wengi wakawa sugu, hawakujali fimbo za mwalimu. Wengine walifukuzwa shule lakini waliondoka huku wakiimba ‘aheri kufukuzwa jama, aheri kufukuzwa.’

Upande wa walimu mambo yalikuwa magumu zaidi. Sijui ni kwa sababu walikuwa na familia au waliogopa kupoteza kazi tu lakini walinywea. Hata mahali ambapo ilikuwa dhahiri mwalimu mkuu amekosea, waliishia kumsifia tu. Hakuna aliyethubutu kumwambia ukweli.

Na waliungwa mkono wa kundi la wanafunzi ambao walipewa jina la ‘wapuksi’, yaani wapambe nuksi maana kazi yao ilikuwa ni kuimba sifa za mwalimu mkuu kila kona … na kutoa taarifa kwake iwapo mwanafunzi yeyote alionesha kukereka na hali ilivyo.

Katika hali hii, unaweza kutabiri matokeo ya mitihani ilikuwaje. Wachache walifaulu lakini walio wengi walikula ile sifuri. Kwa mawazo ya mwalimu mkuu, tatizo lilikuwa kwa wanafunzi, wavivu, hawataki kusoma na wakorofi. Lakini mimi nikabaki najiuliza wapo wanafunzi hawafaulu kwa sababu hawasomi au hawasomi kwa sababu wanajua hawatafaulu. Wanapoteza muda tu.

Na matatizo haya yaliingia kila sehemu. Shamba la shule hovyo, miradi fedha hatujui zinaenda wapi, huko jikoni usiseme kabisa. Ndipo hapo, baada ya kusoma mazingira vizuri, nikabaki najiuliza nifanye nini.

Hapo Mungu akaniona. Siku moja nilisimama na kumwambia mwalimu mkuu amekosea. Wacha ajaribu kunifukuza na fimbo yake. Akaniandikia barua ya kunirudisha wizarani moja kwa moja. Wakati natafakari niweke wapi mizigo yangu, mwalimu mwenzangu akaja akiimba kwa sauti kubwa.

‘Anatoka. Anatoka.’

Kuniona mimi akanikumbatia kwa furaha.

‘Usifunge mizigo tena. Anaondoka.’

Na kweli. Akaja mwalimu mkuu mwingine. Sote tulimwangalia kuona atakuwaje. Hakukuwa na dalili ya fimbo … duh! Wiki ya kwanza, akakaa na walimu muda mrefu kuwauliza kulikoni, wafanyeje kuboresha shule. Hakukomea hapo. Alitembelea kila darasa na kuwaomba wanafunzi waandike insha juu ya shule ninayoipenda. Baada ya kukusanya yote hayo, akasoma na kuweka pamoja mapendekezo yanayofanana. Ungeshangaa makengeza. Mambo mengi, ukiacha viboko na ukali, yalifanana kabisa na yale ya aliyeondoka. Hayakuwa mambo mabaya, bali namna ya kuleta mambo hayo, matumizi ya nguvu, kushurutisha na kutisha badala ya kushirikisha, hayo ndiyo yaliyoleta ukakasi. Pamoja na kufanya maamuzi tata kwa kuwa hakutaka kusikiliza cha mtu na hakuna mtu aliyetaka kumwambia ili afokewe.

Basi baada ya hapo, wacha walimu wafundishe kwa nguvu. Kumbe wengi walipenda kufundisha lakini mbele ya ukali ule, waliacha kuwajibika. Walipopewa nafasi ya kuonesha vipaji na uwezo wao, walifurahi. Sisi walimu tulianza kushindana kufundisha wanafunzi vizuri. Wengine waliozoea mtindo wa zamani walianza kuimba sifa za mwalimu mkuu.

Wacha nicheke. Yule walimsifia kwa ukali wake, sasa huyu wanamsifia kwa ushirikishaji wake. Wapi na wapi! Lakini mwalimu mkuu hakutaka kabisa sifa. Hata kwenye nyimbo za mahafali, akakataa wimbo wa kumsifu yeye na kusema wote wanastahili kupewa sifa.

Kutokana na hayo, hata wanafunzi sugu wakabadilika. Mwanzoni walitia shaka sana, wakaona huyu anadanganya tu. Lakini alivyoendelea kuwashawishi washiriki, na kuwasikiliza kwelikweli badala ya kuwatisha, sugu zikatoweka na walio wengi walianza kusoma vizuri.

Kilichonifurahisha mimi, Makengeza ni kwamba alipenda kumwachia kila mtu nafasi yake ya kuwajibika, kimasomo, kimiradi, kinidhamu na kadhalika. Akatusoma na kutupa kila mmoja nafasi yake ya kutumia vipaji vyetu.

Alipoona tumeteteleka, akatuita na kujadiliana nasi kulikoni. Hakutuingilia katika kazi yetu, ingawa alitusimamia vizuri sana. Kutokana na hayo, hakuna aliyeweza kukwepa wajibu wake na tulianza kujiamini kwamba tunaweza sisi pia, hatuna haja ya kumtegemea mwingine.

Naam twaib. Matokeo ya mitihani yalipotoka watu wakastaajabu. Badala ya kushika mkia wilayani tulikuwa juu kabisa. Wacha mwalimu mkuu afanye sherehe na kutupongeza sote. Toka siku ile, tulio wengi hatukutaka kuhama kabisa.

Hata wanafunzi walisikitika kuondoka maana wao nao walifurahia nafasi ya kusema kwa uwazi na kuwajibika katika maeneo yao. Huko nyuma tulimwachia mtu mmoja aendeshe shule, lakini sasa sote tuliendesha shule kwa pamoja.

Hii si ndiyo njia bora ya elimu na hata maisha kwa ujumla.



Columnist: mwananchi.co.tz