Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Shule zetu ni salama kwa watoto?

15584 Pic+shule TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Taifa linaomboleza mtoto mdogo kupoteza maisha kutokana na kipigo shuleni.

Siperius Eradius (13), hayupo tena duniani, nguvu kubwa iliyotumika kumrudi imekatisha uhai wake.

Nani anayejua kama pengine ndani ya mtoto huyu kulikuwa na talanta ambazo pengine zingekuja kulinufaisha Taifa? Je, haiwezekani Taifa limepoteza rais, daktari, mhandisi au mwalimu wa miaka ijayo?

Kifo chake kiturudishe nyuma mwaka 2016, mwanafunzi mwingine mkoani Mbeya alipoponea chupuchupu mikononi mwa walimu damu changa. Alipewa kipigo cha mbwa mwizi. Sebastian Chinguku, hakuonekana kama mwanafunzi mbele ya waliokuwa wakimsulubu, walimu waliuacha ualimu, wakauondoa uanafunzi wa wake na kumgeuza kuwa kibaka.

Hii ni mifano michache kati ya mingi ikiwamo ile isiyoripotiwa. Ni matukio ya ukatili kwa wanafunzi shuleni chini ya jina la kurekebisha nidhamu.

Ushauri na unasihi vimefeli, sasa dawa pekee ya walimu kujenga nidhamu shuleni ni kutumia bakora, ngumi na mateke. Hili ndilo linachagiza swali je, shule zetu ni salama kwa watoto?

Nidhamu na adhabu shuleni

Hakuna elimu pasipo nidhamu. Nidhamu inatajwa kuwa moja ya mihimili muhimu katika mchakato wa ujifunzaji.

Ndio maana wanafunzi wasio na nidhamu aghalabu wanafanya vibaya kwenye taaluma. Lakini swali kuu ni kwa namna gani walimu wanapaswa kuwarudi wanafunzi wasio na nidhamu au wanaobainika kuwa na makosa?

Je, adhabu za kikatili zikiwamo upigaji wa viboko, adhabu za udhalilishaji ni njia bora zaidi ya kushughulika na wanafunzi wakorofi?

Wakili Marietha Mollel anasema hakuna sheria inayozuia mwanafunzi kuchapwa. Hata hivyo, anataja Sheria ya Elimu Tanzania na Sheria na Adhabu ya Viboko ya mwaka 1979 inayomruhusu mwalimu kumchapa mwanafunzi mkononi au kwenye makalio kwa kutumia fimbo isiyo ngumu.

“Sura 353 ya sheria Sheria ya Elimu Tanzania kifungu cha 60(o) inaruhusu adhabu ya viboko shuleni na inampa mamlaka Waziri wa Elimu kutunga kanuni zinazohusu namna ya kutoa adhabu hiyo kwa wanafunzi,” anafafanua.

Anasema hata Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 iko kimya kuhusu adhabu ya viboko ingawa inazuia vitendo vya ukatili kwa mtoto.

Shule zetu ni salama?

Ukitembelea shule zetu hasa za umma, hutokosa kubaini kwamba walimu wengi bado wanatumia fimbo kama adhabu ya kawaida. Fimbo zimekuwa kama utamaduni uliozoeleka katika shule zetu.

Hoja kubwa ya walimu ni mmomonyoko mkubwa wa maadili miongoni mwa wanafunzi, hali inayofanya walimu waamini kuwa nidhamu ya wanafunzi bila viboko ni jambo lisilowezekana.

Pia, walimu wanarusha lawama kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwa wao ndio wanaolea tabia mbovu za wanafunzi. Kwa mfano, walimu wanasema wazazi wengi hawana muda na watoto wao. Kukosa muda si tu kunatoa mwanya kwa watoto kujihusisha na tabia zisizokubalika lakini kunawafanya washindwe kuwarekebisha watoto wao.

Lakini pia kuna tatizo la ushirikiano mdogo baina ya walimu na uongozi wa shule zao katika kusimamia nidhamu ya wanafunzi. Mifano inayotolewa na walimu ni kwamba wakati mwingine bodi za shule zinafumbia macho matatizo ya kinidhamu na hivyo wanafunzi wanakuwa na ujasiri wa kufanya watakavyo wakijua watalindwa hata wanapokuwa wamefanya makosa ya wazi.

Mwalimu mstaafu, Raymond Ichekeleza anasema, ili kuepuka matatizo kama yaliyojitokeza kwenye shule ya Msingi Kibeta ni walimu kuzingatia utaratibu wa kutoa adhabu kwa mwanafunzi.

Anasema kuwa shule nyingi hazitilii maanani matumizi ya kitabu cheusi ambacho ni maalumu kwa wanafunzi wenye makosa ya utovu wa nidhamu na huwa ni doa kwa safari ya mwanafunzi huyo hata baada ya kumaliza shule.

‘’Akionywa mara ya kwanza akaendelea kushindikana anaandikwa kwenye ‘black book’ na adhabu inaandikwa na mara ngapi ameonywa na mtoa adhabu anasaini hilo ni doa la kumuondolea hata sifa ya uongozi’’anasema Ichwekeleza

Adhabu lazima idhalilishe au kuwa ya kikatili?

Ingawa tunaweza kuwalaumu walimu kwa kutoa adhabu ya fimbo kiholela lakini tukumbe walimu hawa wanatoka kwenye jamii inayoamini kuwa fimbo ndiyo namna pekee ya kumrekebisha mtoto.

Jamii inaamini ili adhabu iwe na nguvu ya kumbadilisha mtu, lazima isababishe maumivu makali kwa anayeadhibiwa. Tumejenga dhana potofu kuwa ufanisi wa adhabu ni mpaka anayeadhibiwa alie, aumie na ikiwezekana adhalilike. Hilo halipaswi kuwa lengo la adhabu. Mtu yeyote anapotoa adhabu aelewe kuwa hafanyi hivyo kwa lengo tu la kumaliza hasira zake. Lengo la adhabu linapaswa liwe ni kumwonya anayeadhibiwa kuwa alichokifanya si sahihi.

Mapendekezo

Tunahitaji la kufikiria upya ulazima wa kutumia fimbo kama adhabu kwa wanafunzi. Badala ya kuharakisha matumizi yake hata katika mazingira yasiyo ya lazima, tujenge uhusiano mzuri baina ya mwalimu na mwanafunzi. Ili hili liwezekane, mamlaka za elimu kuanzia ngazi ya mwalimu mkuu, ziwajibike zaidi kuweka mazingira mazuri yanayojenga daraja baina ya walimu na wanafunzi na kusimamia utaratibu wa kutoa adhabu kwa wanafunzi.

Aidha, katika mazingira ambayo ni lazima pengine kutumia fimbo, mwalimu mkuu awajibike kuhakikisha kuwa adhabu hiyo inatolewa kwa minajili ya kumrudi mwanafunzi na sio kumdhalilisha na kumkomoa. Ikiwa itatokea mwalimu ametumia adhabu hiyo kiholela, mwalimu mkuu achukue hatua madhubuti za kumwajibisha na akishindwa kufanya hivyo, awajibishwe.

Wakili Mollel anaongeza pendekezo la kisheria kwa kusema: “Sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 ifanyiwe nyongeza na kuweka kosa la jinai kwa mwalimu akayetumia adhabu ya viboko kinyume na sheria na kanuni za viboko shuleni.”

Kwa upande mwingine, walimu wakumbuke mipaka yao wanapoadhibu wanafunzi. Kuna haja ya kutenganisha adhabu na vitendo vya ukatili kama tulivyotangulia kueleza.

Pia, lipo tatizo la uandaaji wa walimu. Katika vyuo vya ualimu na hata vyuo vikuu vinavyoandaa walimu, masomo ya saikolojia na unasihi yanafundishwa kijuu juu na matokeo yake walimu wanaondoka na maarifa nusu nusu yasiyowasaidia kuelewa namna bora ya kusimamia malezi ya vijana wasumbufu.

Columnist: mwananchi.co.tz