Ninaendelea kusisitiza pendekezo langu kwako mwalimu kuwa ukielewa msingi wa tatizo la mwanafunzi wako, unaweza kujenga nidhamu yake bila kulazimika kutumia njia za mkato kama bakora.
Hata mwanafunzi unayemwona ameshindikana, anaweza kujirekebisha ukifahamu namna ya kushugulika naye. Muhimu ni kuwa mvumilivu unapochukua hatua.
Katika makala haya, japo kwa ufupi, ninapendekeza kutafuta ushirikiano wa karibu na wazazi ikiwa unataka kupata matokeo mazuri.
Bila shaka unakumbuka ulifundishwa chuoni kwamba familia ndio kiini kikubwa cha tabia ya mwanafunzi. Mambo anayoyaona mtoto yakifanyika nyumbani yanaathiri kwa kiasi kikubwa namna anavyofikiri na kufanya.
Kama ulisoma somo la unasihi na ushauri, utakumbuka majina ya Alfred Alder na Virgia Satir waliotukumbusha kuwa hatuwezi kutenganisha tabia ya mtoto na hulka za familia yake. Kimsingi, unachokiona kwa mtoto ni dalili tu aina ya maisha anayoishi nyumbani.
Kwa uelewa huo utakubaliana na mimi kwamba mtoto anayekosa nidhamu shuleni ni sawa na mtu anayelia kutafuta msaada. Kutosikia, ukorofi, ujeuri, ni kilio cha kukuambia wewe uliye mwalimu wake kwamba nyumbani kwao mambo hayako shwari.
Kama umefundisha kwa muda, utaelewa namna gani wakati mwingine unaweza kumwadhibu mtoto lakini habadiliki. Unafanya kila jitihada za kumrekebisha lakini mtoto haonekani kukuelewa.
Katika mazingira kama haya, unahitaji kuelewa kwamba tabia hiyo unayojitahidi kuiondoa, imeota mzizi kwenye moyo wa mwanafunzi. Huwezi kuing’oa kwa jitihada zako mwenyewe. Huwezi kuing’oa kwa adhabu kali.
Familia ni sawa na mfumo unaounganisha tabia za watu tofauti lakini zenye kutegemeana. Tabia ya mzazi kwa mfano, inaathiri tabia ya mtoto. Tabia ya mtoto nayo kwa upande mwingine, inaathiri tabia ya mzazi.
Mzazi, mathalani, anaweza kuwa na hulka ya ukali kwa watoto. Kila akirudi nyumbani hawezi kuzungumza kwa amani na familia yake bila kufoka. Watoto wanaokulia kwenye mazingira kama haya wanaweza wasipende tabia hiyo lakini wakajikuta na wao wakiyafanya hayo hayo wasiyoyapenda.
Sababu ni kwamba kinachofanywa na wazazi hugeuka kuwa sheria isiyoandikwa inayoongoza namna watoto wanavyofanya mambo yao. Namna gani azungumze na mtu mzima; nini afanye anapohitaji kitu; jinsi gani atatue migogoro yake pale inapojitokeza, haya ni baadhi ya mambo tunayoweza kuyaita sheria zinazotokana na desturi za familia.
Mwalimu mmoja wa sekondari alinisimulia kisa cha kumwita mzazi wa mtoto aliyekuwa amefanya kosa linalostahili adhabu. Katika hali isiyotarajiwa, mzazi yule alipofika shule alionekana kushangaa inakuwaje mwalimu anamsumbua kijana wake.
Badala ya kushirikiana na mwalimu kushughulikia tatizo la kijana wake, mzazi alikuwa upande wa mwanawe akimshambulia mwalimu aliyekuwa anajaribu kushughulikia tatizo.
Mwalimu alinieleza kwa masikitiko, “Ningefanyaje hapo? Kile nilichofikiri ni kosa, mzazi anaona ni sahihi. Mzazi na mtoto wake hawaelewi kosa liko wapi. Ningechukua hatua gani hapo?”
Huu ni mfano wa namna gani maisha ya mwanafunzi nyumbani yanavyokuwa msingi wa tabia ya mwanafunzi. Unaweza kumlaumu mtoto kwa tabia fulani, lakini kumbe kwa mwanafunzi huyo tabia unayoiona ni sehemu ya maisha yake. Unaweza ukashangaa, mathalani, mtoto hasalimii watu akiwa shuleni. Anakupita kama hakuoni. Lakini kumbe hiyo inaweza kuwa ndiyo hali halisi nyumbani anakotoka.
Anapoamka, hakuna mtu anakumbuka kumsalimia yeyote. Mtoto kama huyu unaweza kumwadhibu lakini usipate matokeo unayoyahitaji kwa sababu hajakuzwa kusalimia.
Wakati mwingine kuna watoto wanakuwa wagomvi shuleni kwa sababu tu mazingira ya nyumbani yanahamasisha ugomvi.
Mara nyingi walimu wamekuwa wepesi kutoa adhabu bila kuwasikiliza wanafunzi. Lakini kama wangejipa muda wa kuwasikiliza, wangegundua kuwa wanafunzi hawa wanaonyesha nidhamu mbaya kwa sababu tu kuna kitu kimekosekana kwenye maisha yao.
Wapo wanafunzi wanaishi kwenye mazingira magumu nyumbani. Fikiria mwanafunzi ambaye wazazi wake wamefarakana. Mwanafunzi huyu anaweza kuwa na uchungu mkubwa ndani yake hata kama anaweza kuonekana akifurahi anapokuwa kwenye mazingira ya shule.
Mara nyingi migogoro ya wazazi huwafanya watoto wajilaumu. Watoto hujisikia hatia kwamba nao kwa namna moja au nyingine wanahusika na matatizo wanayoyaona kwa wazazi wao. Mwanafunzi anayepitia maisha kama haya anaweza kukukosea adabu lakini asielewe anachokifanya.
Kwa upande mwingine, wapo wanafunzi waliokulia kwenye mazingira ya kudekezwa. Wanapokuja shuleni, wanafunzi hawa wanahama na tabia hizo walizotoka nazo nyumbani.
Kama nilivyotangulia kueleza, matatizo mengi ya mwanafunzi yanaanzia kwenye familia walikotoka. Unaposhughulika na mwanafunzi jitahidi kuelewa kuwa yeye ni sehemu ya sheria zisizoandikwa lakini zinazoongoza mambo anayoyafanya.
Katika mazingira kama haya, huwezi kushughulikia suala la nidhamu bila kumshirikisha mzazi. Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa karibu na wazazi wa mtoto kama namna ya kutafuta ufumbuzi utakaokuletea matunda.
Mahali pa kuanzia ni kufanya mazungumzo na wazazi kuhusiana na tabia ya mwanafunzi. Mazungumzo haya yalenge kuelewa mazingira ya kimalezi yaliyopo nyumbani ili uweze kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kumsaidia kijana.
Hakikisha mnazungumza lugha moja na mzazi ili aelewe shida ya mwanawe iko wapi. Mzazi asipoelewa inakuwa vigumu hatua zozote utakazochukua kuleta mabadiliko unayoyatarajia.
Lakini pili, wakati mwingine shida inakuwa ni wazazi wenyewe kukosa mamlaka kwa watoto wao. Chukulia mzazi anayeweza kumwambia jambo mwanawe na asifanye na bado akachukulia kuwa kawaida.
Chukulia mzazi mlevi, mdhalilishaji na mwenye tabia ya ugomvi uliopitiliza.Tabia kama hizi zinaweza kumfanya mzazi ‘akakosa’ mamlaka.
Katika mazingira kama haya ni muhimu kuzungumza kwa kina na wazazi, ili waelewe kwa kiwango gani tabia na mienendo yao inavyofanya kazi ya kumwadabisha mwanafunzi kuwa ngumu.