Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sheria, kanuni za wanyamapori mfumo wa jeshi usu zaandaliwa

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Wizara ya Maliasili na Utalii ipo kwenye hatua za mwisho za kuandaa sheria na kanuni za kuwezesha sekta ya wanyamapori na misitu inakuwa na mfumo wa jeshi usu badala ya uendeshaji wa kiraia.

Akizungumza juzi kwenye mahafali ya 53 ya uhifadhi wanyamapori na kuadhimisha miaka 52 ya Taasisi ya Wanyamapori Pasiansi, waziri wa wizara hiyo, Dk Hamisi Kigwangalla alisema lengo la kuandaa sheria hiyo ni kukabiliana na ujangili, biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya misitu.

“Serikali imedhamiria na imejipanga kuhakikisha inadhibiti matumizi haramu ya maliasili, ikiwamo uingizwaji wa mifugo kwenye maeneo yote ya hifadhi yanayohifadhiwa kisheria,” alisema Dk Kigwangalla.

Pia, alisema tafiti zinaonyesha hali ya hifadhi na mazingira Afrika inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo za kisiasa, kiuchumi, ukuaji wa teknolojia, mabadiliko ya tabia nchi na ujangili.

Alisema Serikali inaendelea kupambana na changamoto hizo ili kuhakikisha wanyama wanakuwa salama ndani na nje ya maeneo ya hifadhi.

Akizungumzia tatizo la ajira na umri wa kuajiriwa kwa wahitimu hao, Dk Kingwangalla alisema atawasiliana na mamlaka za ajira ili kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwa mahitaji ya askari hifadhini ni makubwa.

Awali, Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori Pasiansi, Lowaeli Damalu alisema askari 425 wamehitimu shahada na stashahada ya uhifadhi wa wanyamapori.

Pia, wamo wahitimu wa kozi ya usimamizi wa sheria za wanyamapori na misitu iliyoanza Agosti 21, 2017.

Alisema askari hao walianza mafunzo wakiwa 441 lakini 16 walishindwa kuhitimu na tisa waliacha masomo kutokana na ugonjwa, masuala ya kifamilia na mmoja alifariki dunia.

Alisema saba walifukuzwa baada ya kubainika wanatumia dawa za kulevya ikiwamo bangi, pombe na wengine utoro na ujauzito.

Mhitimu Majaliwa Rashidi alisema changamoto zinazowakabili ni kukosekana ajira.

Naibu katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Aloyce Nzuki alisema tangu chuo kianzishwe askari 4,961 wamehitimu na kati yao asilimia 80 wanafanya kazi katika maeneo mbalimbali ya hifadhi.

Columnist: mwananchi.co.tz