Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Shambulio la Dar, Nairobi lilivyomuibua Osama na kuleta hofu ya usalama

10589 Pic+ubalozi TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya leo unaadhimisha miaka 20 tangu kufanyika mashambulizi ya kigaidi yaliyobadili hali ya usalama wa dunia.

Mashambulizi hayo yaliyofanyika kwa tofauti ya dakika chache kati ya ubalozi ulioko Dar es Salaam na ule wa Nairobi, ndiyo yaliyomtambulisha kwa mara ya kwanza kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Qaida, Osama bin Laden.

Kabla ya tukio hilo ni watu wachache mno waliokuwa wakimjua Osama na washirika wake likiwamo kundi la kigaidi la Al Qaeda.

Zaidi ya watu 250 walipoteza maisha hayo, baadhi ya Watanzania walionusurika wanasema ingawa kumekuwa na jitihada za kukabiliana na vitendo vya kigaidi, lakini wanasisitiza kuwa dunia si sehemu salama tena. Wanasema mashambulizi hayo yaliyofanywa Agosti 7, 1998 yameacha alama isiyofutika mioyoni mwao, yanaelezea ukatili uliojificha mioyoni mwa baadhi ya binadamu wanaodiriki kutoa uhai wa wenzao wasiokuwa na hatia.

Baadhi yao mashambulizi hayo yameendelea kuwaweka katika hofu, wanasema tukio hilo lililotokea wakati wa utawala wa Rais Bill Clinton limeacha mtihani mkubwa duniani.

Wachunguzi wa mambo wanasema mashambulizi hayo ndiyo yaliyotoa tafsiri ya upande wa pili kuhusu usalama wa dunia na hata kuwekwa kile kinachoitwa ‘umulikaji’ wenye dhana ya kutaka kubaini na kukabili uovu.

Ingawa tangu awali suala la ulinzi lilipewa umuhimu mkubwa kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo Ikulu, ndani ya ndege na hata kwenye makazi ya viongozi wakubwa wa kitaifa, lakini baada ya mashambulizi ya Dar na Nairobi, kipengele hicho kimebadilika.

Ugaidi huo ndio ulioipeleka mbio dunia na kuifanya itafakari upya kuhusu mwenendo wake. Dunia ilianza kujifunza umuhimu wa kuimarisha ulinzi na upekuzi katika maeneo mbalimbaliikiwamo sehemu yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na hata kuongeza dhana ya kuwatilia shaka watu wanaodhaniwa ni wenye itikadi kali.

Akikumbuka alivyompoteza baba yake mzazi aliyeuawa kwenye shambulizi la Dar, Hussein Ramadhani Mahundi anasema dunia iko njia panda huku mataifa makubwa yakiendelea kukuna vichwa kutafuta njia bora ya kuukabili ugaidi.

Anasema tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma sasa dunia si sehemu salama ya kuishi kutokana na kuongezeka wimbi la vitendo vya kigaidi. Anasema kwa mazingira ya sasa huwezi kujua saa wala dakika ukayopokonywa uhai kutokana kuongezeka vitendo vya kigaidi. “Mimi naweza kusema sasa tunatembea na kifo mkononi kwani bomu halichagui mtu wa aina gani... awe Mwafrika, Mzungu au mtu wa kabila gani. Yaani duniani hakuna amani tena Uchina, Urusi na hata Marekani wanaendelea kukabiliana na hali hii, jumuiya ya kimataifa iendelee kushirikiana katika hili, “ anasema.

Anasema kifo cha mzazi wake aliyekuwa mfanyakazi katika ubalozi wakati shambulizi likitokea kiliwaacha njia panda kwani ndiye aliyekuwa tegemeo la familia yao.

Anasema wakati wa shambulizi hilo yeye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Makongo na siku hiyo alikuwa ameitwa na mzazi wake huyo aende ubalozini kwa ajili ya kuchukua fedha ili akalipe ada.

Anasimulia kuwa wakati akiwa shuleni alisikia kishindo kikubwa cha mlipuko na kwa vile walikuwa katika eneo la jeshi askari walichukua jukumu la kuwatuliza na kuwakusanya eneo moja kuwataka wasikurupuke kwa jambo lolote. Baada ya hali kutuliwa waliruhusiwa kuondoa shuleni hapo.

“Baadaye tukaambiwa ubalozi wa Marekani umelipuliwa nami mara moja kitu kikanichoma moyoni nikahisi lazima mzazi wangu atakuwa amepatwa na jambo. Nilipofika nyumbani nikaelekea moja kwa moja Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, baada ya kuzunguka baadaye nikapelekwa chumba cha kuhifadhia maiti nilikomkuta mzee wangu.

“Nashukuru Mungu nilinusurika maana siku ya tukio mzee aliniita niende kazini kwake nikachue hela lakini sijui niseme bahati mbaya au nzuri shule walininyima ruhusa ndiyo salama yangu,” anasema.

Anasema kwa hali kama hiyo, ugaidi ni suala linapopaswa kupigwa vita na kila mmoja kwa sababu linawatia matatizoni watu wasiokuwa na hatia.

Shambulizi hilo pia ndilo lililomwacha, Christant Hiza Nyange katika maisha ya hofu hadi leo. Nyange bado anafanya kazi ubalozi wa Marekani nchini.

“Hofu mpaka leo bado ipo kwani nikisikia kitu kama mlipuko yaani naweza kushtuka...unaona...maana hata nikiendesha gari likipata basti nashtuka,” anasema Hiza akikumbuka jinsi alivyonusurika kwenye tukio hilo na jinsi lilivyoathiri maisha yake ya baadaye.

Mlipuko Ubalozini Dar

Hiza anakumbuka mlipuko ulipotokea alikuwa amesimama eneo linalotumika kuegeshea magari na baada ya shambulizi hilo hakuna anachoweza kukikumbuka kwa ufasaha, alishtukia yupo Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Ilikuwa siku nzito, tukio kama hili lilivyotokea mimi sikuelewa ni nini, nilisikia tu mlipuko halafu nikarushwa juu nilipofika chini nikaona kama niko kwenye ndoto lakini baadaye nikaona mtu ananishika kuninyanyua, yule mtu alikuwa na damu kifuani nafikiri alikuwa ametoka kuwasaidia wengine... sasa nikawa namkimbia, nilipomkimbia huku magari yanawaka moto yule jamaa ikabidi anikate, wanasema alinipiga ngwala na akanigandamizia kwa chini,” anasema Hiza

Baada ya purukushani hizo hakutambua kilichoendelea, alizinduka akiwa Muhimbili huku pembeni akiwaona pia wafanyakazi wenzake wakiwa na damu na wengine wamefungwa bendeji.

“Nilikuwa siwezi kuongea vizuri tena nilikuwa nasikia kwa shida, wakati nazinduka niliona nimezungukwa na askari wakinihoji kuhusu tukio lile lakini sikuweza kusema mengi kwa vile nilishindwa kuongea na hata askari wenyewe walionionea huruma,” anasema.

Hadi leo anashindwa kuelewa kilicho nyuma ya waliotekeleza shambulizi hilo lililoishtua dunia kwa jinsi lilivyoratibiwa kwa wakati mmoja katika ubalozi wa Dar na ule wa Nairobi.

Shambulizi hilo lilituma ujumbe mpya kwa viongozi wa dunia kuwa magaidi walikuwa na uwezo wa kuvuruga mfumo wa amani ya dunia na hata kuibua hofu.

Tangu wakati huo jina la Osama bin Laden lilianza kutamkwa rasmi vichwani mwa watu wengi na jina hilo lilipata umaarufu mkubwa zaidi wakati wa shambulio jingine la Septemba 11, 2001.

Ingawa rais wa Marekani wakati huo George W.Bush aliahidi kumnasa Osama akiwa hai au mfu, lakini gaidi huyo aliendelea kuisumbua dunia akishirikiana na makundi mengine ya kigaidi barani Afrika na Asia kuratibu mashambulizi.

Kundi hilo liliendelea kufanya mashambulizi maeneo mbalimbali duniani ikiwamo yale yaliyotokea Mashariki ya Kati, Bali, Madrid, London na Paris.

Wakati Bush akishindwa kumpata Osam akiwa hai au mfu, utawala wa Barack Obama ulifanikiwa kumuua Osama Mei 2, 2011 katika mji wa Abbottabad nchini Pakistan.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, mtaalamu wa masuala ya kukabiliana na ugaidi wa taasisi ya Brookings, Daniel Byman anasema Marekani ilishindwa kuchanga vyema karata zake na hata operesheni yake iliyoendesha huko Sudan na Afghanistan baada ya mashambulizi hayo haikuzaa matunda.

Anasema kushindwa kupanga mikakati mizuri dhidi ya Al Qaida, kulifanya kundi hilo kujipanua zaidi nchini Afghanistan kutokana na ushirika wake na uliokuwa utawala wa Taliban.

Mjini Dar es Salaam baadhi ya wafanyakazi walionusurika katika shambulizi hilo wanasema miongoni mwa vitu ambavyo havitasahaulika maisha mwao ni pamoja na tukio hilo.

Monica Kapilima ni mmoja wa walionusurika na ambaye bado ni mfanyakazi ubalozini hapo anasema kwamba alinusurika wakati shambulizi likifanyika kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.

“Kazi yangu ilikuwa kuratibu na kuandaa safari, nilikuwa nimekwenda kwa wakala kufuatilia tiketi ya ndege nikiwa kule nilisikia kishindo baadaye tukaambiwa ubalozi wa Marekani umeshambuliwa na baadaye tukarejea ubalozini.”

Anasema baadaye wafanyakazi wote waliamuliwa kwenda kujihifadhi nyumbani kwa balozi na kisha kuanza kuwasiliana na watu mbalimbali wakitambuana kama walinusurika na tukio hilo au la.

“Baada ya wiki moja hivi ndiyo wafanyakazi tulianza kukutana na kutambuana kama mtu fulani alikuwa amepoteza maisha au kujeruhiwa na yuko wapi na mambo yanayofanana na hayo,”.

Columnist: mwananchi.co.tz