Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Shahidi akiri kuhongwa bia mbili amchague Kihiyo-4

89491 Kihiyopic Shahidi akiri kuhongwa bia mbili amchague Kihiyo-4

Sat, 21 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya kuahirishwa kwa mara nyingine, kesi ya kupinga ushindi wa mbunge wa Jimbo la Temeke katika uchaguzi wa Novemba 1995 iliyofunguliwa na waliokuwa wagombea wa NCCR-Mageuzi ambao ni Richard Tambwe Hiza na wa Chadema, Beatrice Mtui pamoja na wananchi wanne iliendelea tena Aprili 10, 1996.

Siku hiyo, mahakama ilielezwa kuwa wale wote ambao walikuwa hawajui kusoma na kuandika walipigishwa kura kwa mgombea wa CCM, Ramadhani Ally Kihiyo.

Shahidi wa 10 katika kesi hiyo, Kassim Hendelo alidai hayo katika ushahidi wake alioutoa mahakamani hapo siku hiyo mbele ya Jaji Mapigano.

Shahidi huyo ambaye alionekana kuwa kivutio mahakamani hapo kuliko mashahidi wengine wote waliomtangulia kutoa ushahidi wao alisema kwamba alikuwa akiwasaidia watu wasiojua kusoma na kuandika kwa kuwauliza wanataka kumchagua mgombea yupi miongoni mwa wagombea wote, na ndipo yeye akawa anaweka alama ya ‘vema’ kwa mgombea wa CCM bila wapiga kura hao kuelewa kinachoendelea.

Shahidi huyo ambaye wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 1995 na ambao ulirudiwa Novemba 19 mwaka huo alikuwa ‘mpiga debe’ wa mgombea wa CCM, alisema yeye mwenyewe alihusika kuwapigisha kura za kumchagua Kihiyo zaidi ya watu 800 wasiojua kusoma na kuandika bila utashi wao.

Hendelo ambaye wakati anatoa ushahidi huo alikuwa amejiengua CCM na kujiunga na NCCR-Mageuzi, hadi wakati uchaguzi huo unafanyika alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Tawi la Mivinjeni na mjumbe wa mkutano mkuu wa kata ya Kurasini.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa baada ya kufanyika uchaguzi wa awali wa Oktoba 29 uliofutwa ambao ilionekana CCM ilishindwa, wao kama viongozi wa chama hicho walikuwa wakikutana usiku kwenye ofisi ya Tawi la Mivinjeni ili kupanga mikakati ya kushinda.

Katika mkutano huo, Kihiyo alifika mara mbili. Pamoja na mambo mengine walipanga mbinu za kuwasaidia wapiga kura ambao hawajui kusoma na kuandika, kura zao kuziweka kwa mgombea wa CCM. Huo ndio ulikuwa mkakati wao wa awali.

Wakiwa katika vikao hivyo vya faragha, alisema Hendelo, mwenyekiti wa tawi hilo la Mivinjeni aliwaambia wasiwe na shaka kwani kuna Wahindi ambao walikuwa wametoa mamilioni ya pesa, na kwa sababu hiyo “hawatakuwa watu wa njaa njaa.”

Akiulizwa kama wasimamizi wa vituo hawakuwa wakiwakataza kuwasaidia wasiojua kusoma na kuandika, mahojiano kati ya shahidi Hendelo na Wakili Dk Masumbuko Lamwai yalikuwa hivi:

Lamwai: Wasimamizi wa vituo hawakuwa wakiwazuia kuingia ndani ya vituo?

Hendelo: Wasimamizi walikuwa wetu.

Lamwai: Ina maana gani unaposema walikuwa wetu?

Hendelo: Yaani wasimamizi pamoja na Tume ya Uchaguzi walikuwa wanataka sana CCM washinde.

Lamwai: Zaidi yako kulikuwa na watu wengine?

Hendelo: Oh. Wengi, ambao wengine walikuwa wanakaa vichochoroni na kuwaeleza wapiga kura “msimsahau mmachinga”, yaani (Benjamin) Mkapa.

Hendelo alisema usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi wa marudio, yeye alisambaza karatasi za maelezo ya wagombea ambazo alizibandika karibu na vituo vya kupigia kura, na kazi hiyo aliifanya usiku kwa maelekezo ya ofisi ya CCM.

Kisha akaja shahidi wa 11, Henry Kowelo, ambaye alikuwa mratibu wa vituo vya kata ya Kurasini kupitia chama cha NCCR-Mageuzi. Alisema kufuatia kampeni za siri zilizofanywa na CCM, watu walinunuliwa pombe na yeye alipata bia mbili alizokunywa, huku msimamo na ushawishi ukiwa ni kuhakikisha mgombea wa CCM, Kihiyo, anashinda.

Shahidi huyo alisema katika maeneo hayo vituo vingi vya kupigia kura viliwekwa kwenye nyumba za wajumbe wa nyumba kumi na alivitaja vichache kama kwa Mibavu, kwa Njinjo, kwa Bregi na kwa Mbonde.

Mahojiano kati ya shahidi huyo na mwanasheria wa Serikali, Julius Malaba yalikuwa hivi:

Malaba: Ulifika tu na kupewa bia au ilikuwa vipi?

Kowelo: Nilipoingia tu ndani nilikaribishwa na kupewa bia.

Malaba: Ulipopewa nawe ulikunywa bila kuuliza?

Kowelo: Sasa uulize nini na unafahamu hiyo ni bia?

Baada ya kuzuka utata juu ya shahidi wa 12, mahakama ililazimika kuiahirisha kesi hiyo hadi siku iliyofuata. Utata huo uliibuka baada ya kukataliwa kwa shahidi huyo wa 12, Elizabeth Magwaja, ambaye alikataliwa kutoa ushahidi kwa kuwa yeye pia alikuwa ni mlalamikaji wa kwanza katika kesi ya tatu ya kupinga matokeo jimbo hilo.

Baada ya Elizabeth kupanda kizimbani na kula kiapo na kuanza kutoa ushahidi wake, aliulizwa kama alishiriki katika zoezi la upigaji kura lililofanyika Oktoba 29 na kurudiwa Novemba 19. Alisema alishiriki.

Hata hivyo, alipoulizwa juu ya shahada yake aliyotumia kupiga kura, alisema alimpa Dk Masumbuko Lamwai wakati wa kufungua kesi hiyo, kauli ambayo ilimfanya Wakili William Erio aliyekuwa anamtetea Kihiyo kupinga shahidi huyo kuendelea kutoa ushahidi wake baada ya kubainika kuwa hakuwa na shahada.

Hatua hiyo ilikubaliwa na Jaji Dan Mapigano aliyekuwa anaisikiliza kesi hiyo. Jaji huyo alimuuliza wakili Majura Magafu juu ya shahada hiyo, lakini wakili huyo alisema alichoambiwa na Dk Lamwai ni kwamba shahada hizo pamoja na makaratasi mengine yanayohusu kesi hiyo yalipotea.

Wakili Magafu alidai kuwa Dk Lamwai alishaomba Tume ya Uchaguzi ipeleke vifaa vyote vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu mahakamani ili waweze kutafuta uthibitisho kuwa Elizabeth alijiandikisha na kupiga kura.

Lakini hoja hiyo ya Wakili Magafu ilipingwa na mwanasheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Abraham Senguji, ambaye alisema kuwa haiwezekani vifaa vyote vilivyotumika kwenye uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na masanduku 549, vipelekwe mahakamani hapo.

Kutokana na mabishano hayo ya hoja za kisheria miongoni mwa mawakili hao, ilibidi Elizabeth aondoke kizimbani bila kutoa ushahidi wake na jaji akashauri pande zote katika kesi hiyo zikae na kukubaliana namna ya kuweza kuvipata vielelezo hivyo.

Hata hivo, baada ya kukosekana kwa mwafaka miongoni mwao, kesi hiyo ililazimika kuahirishwa na Jaji akaamuru aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, afike mahakamani siku iliyofuata, asimame kizimbani kuhusu kauli alizotoa wakati wa uchaguzi wa marudio.

Ditopile alilazimika kufika mahakamani siku alipotakiwa kufika, ingawa kwa kuchelewa. Hata hivyo, Wakili Lamwai alidai kuwa Ditopile alipopelekewa wito wa mahakama aligoma kuupokea.

Itaendelea kesho...

Columnist: mwananchi.co.tz