Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Serikali za mitaa: Historia na chimbuko lake tangu ukoloni

14387 Pic+mitaa TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika makala iliyopita nilijaribu kuelezea uhusiano uliopo katika ya serikali za mitaa na Serikali kuu. Leo nijaribu kuelezea kwa undani kidogo historia na chimbuko la serikali za mitaa.

Ni muhimu kurudia historia ya taifa letu, ili hata kama watu wakifanya makosa, kama haya tunayoyashuhudia ya madiwani kuhama vyama vya siasa na kutulazimisha kurudia uchaguzi kwa gharama kubwa, wakati asilimia kubwa ya Watanzania hawana maji na huduma nyingine za kijamii, isiwe ni bahati mbaya; mtu afanye makosa akifahamu. Inawezekana wengine hawafahamu vizuri maana ya serikali za mitaa na chimbuko lake.

Historia na chimbuko la serikali za mitaa katika taifa letu Tanzania, inafafanuliwa katika vipengelee vitatu. Vipengele hivi ni: serikali za mitaa kabla na wakati wa ukoloni; serikali za mitaa tangu ukoloni hadi mwaka 1972 na urejeshwaji wa serikali za mitaa za kidemokrasia.

Wataalamu wengi wanakubaliana kwamba serikali za mitaa ni chombo cha utawala wa umma, kilichopewa madaraka ya kuamua na kuendesha shughuli za umma katika sehemu ndogo ya nchi au taifa. Na katika utaratibu au mfumo wa Serikali, chombo hiki huwa ni cha utawala katika ngazi ya chini, baada ya ile ya mkoa na Taifa.

Hivyo tukiangalia nyuma, kabla na wakati wa ukoloni, tutaona kwamba hapo awali makabila na koo mbalimbali zilikuwa zikijitawala zenyewe. Zilikuwa na mfumo unaofanana na serikali za mitaa.

Tukifuata maana serikali za mitaa kama inavyotolewa na wataalamu, basi mfumo huu ulikuwapo hata enzi za mababu zetu, hata kabla ya ukoloni.

Koo au makabila hayo yalikuwa yakiongozwa na wazee waliotambuliwa na kuheshimiwa. Viongozi hao walikuwa wakisaidiwa na mabaraza ya wazee katika uendeshaji wa shughuli za ukoo au kabila husika. Mabaraza haya yalikuwa muhimu katika utoaji wa maamuzi mazito yahusuyo jamii zao kama vile njaa, maradhi au hata vita kutoka ukoo au kabila jingine.

Hivyo kwa namna fulani, tangu enzi ya zama, mababu zetu walikuwa na aina ya utawala ambao kwa kiasi ulikuwa unafanana na wa sasa kwa msingi wa utawala katika ngazi za chini. Tofauti ni kwamba wakati ule viongozi wa chini hawakuchaguliwa kwa kufuata demokrasia na kuzingatia jinsia. Kulikuwa na namna yao ya kuchaguliwa kufuatana na sifa za jamii husika na viongozi hao walisikilizwa na kuheshimiwa.

Wakoloni wa kwanza kufanya maskani yao hapa, yaani Wajerumani na Waarabu walikuta utawala wa kichifu, ambao ulikuwa unatawala kwenye ngazi za chini kama zilivyo serikali za mitaa, lakini wao hawakutaka kuutambua. Katika kipindi cha utawala wa Mjerumani viongozi hao wa makabila mbalimbali hawakutambuliwa rasmi.

Badala yake Mjerumani aliwateua watu wake walioitwa maakida kuwa mawakala wake katika utawala wa chini. Mfumo huu uliwaletea matatizo makubwa Wajerumani. Mifano ni vita kati ya Wajerumani na Wahehe walioongozwa na Chifu wao Mkwawa au vile vita vya Pangani vilivyoongozwa na Abushiri.

Historia inatwambia kwamba Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia, mwaka 1914-1918, vilimng’oa Mjerumani nchini Tanganyika. Badala yake Mwingereza, aliingia kuitawala Tanganyika akiwa na mfumo wake wa utawala.

Tofauti na Mjerumani, Mwingereza aliwatambua machifu wa jadi wa makabila mbalimbali na pale ambapo hawakuwapo, aliwaweka. Gavana Donald Cameron, aliyetawala Tanganyika kati ya mwaka 1925 na 1931, alipitisha sheria ya Mamlaka ya Wenyeji (sura ya 72) ya 1926. Huu ulikuwa mwanzo wa kuhalalishwa rasmi kwa serikali za mitaa chini ya serikali ya kikoloni na hii ndiyo ilikuwa chimbuko la serikali za mitaa za sasa nchini.

Gavana, huyu alikuwa na uzoefu wa Nigeria alikofanya kazi kabla ya kuja Tanganyika. Uzoefu huu ulimfanya kuwakubali machifu na sehemu ambazo hazikuwa na machifu aliwaweka. Gavana huyu aliamini kwamba wananchi wangalitekeleza kwa hiari zaidi amri za Serikali yake pale zilipokuwa zikitolewa na machifu wao. Utaratibu huu wa mamlaka za wenyeji uliendelea hadi mwishoni mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, mwaka 1939-1945.

Marekebisho ya sheria

Sheria ya Mamlaka ya Wenyeji ya mwaka 1926, ilifanyiwa marekebisho mwaka 1950. Marekebisho haya yalisababishwa na vuguvugu la kudai Uhuru. Wananchi walitaka kuwa na uhuru zaidi wa kujiamulia mambo yao wenyewe.

Waziri wa makoloni, Arthur Creech Jones alituma waraka kwa magavana wote wa Kiingereza mwaka 1947 akiwataka waanzishe mfumo wa kidemokrasia wa serikali za mitaa katika makoloni yao.

Kufuatana na mabadiliko hayo, machifu waliundiwa mabaraza ya kuwashauri wakuu wa majimbo na wilaya. Mamlaka hizo zilipewa pia kibali cha kutumia mapato yao kwa shughuli za utawala, maendeleo na ustawi wa jamii. Kamati za fedha ziliundwa kusimamia mapato na matumizi kwa niaba ya mamlaka.

Mwaka 1953, serikali ya kikoloni ilifanya mabadiliko mengine katika muundo wa serikali za mitaa. Sheria ya Serikali za Mtiaa (Sura 333) ilipitishwa. Sheria hii ilifuta Mamlaka ya Wenyeji (sura 72) ya 1926. Mwaka huohuo Chuo cha Serikali za Mitaa kilifunguliwa Mzumbe, Morogoro kwa lengo la kuendesha kozi fupi kwa ajili ya machifu, makarani wa mahakama za wenyeji na wajumbe wa mabaraza ya wenyeji.

Pia, sheria hiyo ya mwaka 1953 iliidhinisha Halmashauri za Serikali za Mitaa kuwa na madaraka kamili ya utendaji juu ya watu wote wanaoishi katika maeneo yao bila kujali rangi zao. Ni sheria hiyo ndiyo iliyoanzisha utaratibu wa uchaguzi wa madiwani na halmashauri kuwa na uhuru zaidi wa utendaji.

Hata hivyo, mfumo huu wa kikoloni ulikuwa na kasoro fulani. Utaratibu wa uchaguzi wa madiwani ulikuwa wa kura tatu, yaani kuchagua watu watatu, Mwafrika, Mzungu na Muasia. Utaratibu huu haukutilia maanani wingi wa Waafrika weusi, uliwawezesha Wazungu na Waasia kuwa na idadi ya madiwani sawa na Waafrika. Maana yake ni kwamba Wazungu na Waasia waliweza kuchukua theluthi mbili ya madiwani, ingawaje walikuwa wachache sana kuliko Waafrika.

Mfumo huu ulikuwa na misingi ya ubaguzi wa rangi. Wakoloni, walipendelea mfumo huu ili kulinda utawala wao.

Itaendelea wiki ijayo

Columnist: mwananchi.co.tz