Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Serikali isizidhoofishe halmashauri za wilaya

9527 Pic+serikali TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serikali imekabidhi shughuli za ukusanyaji wa mapato ya maegesho jijini Mwanza kwa Wakala wa usimamizi wa barabara vijijini (Tarura).

Shughuli hizo ambazo kwa sasa zipo kwenye majaribio ya miezi mitatu zitawalazimu madereva kulipa ushuru kwa njia ya mtandao.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Tarura Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Koyoya Fuko, kwa kushirikiana na Kampuni ya NPK Technology ya jijini Dar es Salaam, Tarura itafunga vifaa vya kisasa zikiwemo kamera za CCTV katika mitaa yote ya jiji la Mwanza zitakazonasa na kuratibu shughuli za maegesho na malipo.

Pamoja na malipo ya maegesho, kamera hizo pia zitasaidia masuala ya ulinzi na usalama mitaani kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi mienendo inayotiliwa mashaka yanapobainika mitaani.

Mfumo huo unaofanyiwa majaribio jijini Mwanza kabla ya kuenezwa nchi nzima pia utasaidia kuimarisha usafi mitaani kwa kubaini maeneo ambayo uchafu umerundikana na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

Anasema kupitia mfumo huo, wanatarajia mapato ya ushuru wa maegesho kupanda kutoka Sh500 milioni za sasa hadi kufikia Sh2.5 bilioni kwa mwaka.

Wakati Tarura wakifurahia kupata chanzo kipya cha mapato, Halmashauri zinaendelea kuugulia na msumari wa moto baada ya Serikali kuendelea kuchukua vyanzo vya mapato ambavyo awali vilibuniwa na kukusanywa na halmashauri.

Naibu Meya wa Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha alionyesha wasiwasi kuwa utekelezaji wa mipango licha ya kuongeza makusanyo, lakini unaendelea kuzidhoofisha halmashauri kwa kuzinyang’anya vyanzo vya mapato.

Kilio hicho pia kilitolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga aliyesema sehemu ya fedha zilizotokana na ushuru wa maegesho zilizisaidia halmashauri kuzilipa kampuni yanayofanya usafi mitaani na uamuzi wa kuitwaa unamaanisha halmashauri zianze kujipanga upya.

Akizungumzia utekelezaji wa mpango huo, Fuko anasema mfumo huo utakapoanza kazi, malipo ya maegesho yatafanyika kwa njia ya kielektroniki kwa njia ya mitandao ya simu badala ya mfumo wa sasa wa kutumia mawakala mitaani.

Kwa mtazamo wangu mfumo huo unaweza kuwa mzuri kwa upande mmoja na mwingine ukiumiza kwani kutaondoa tabia za baadhi ya madereva waliokuwa wamezoea kumalizana na wakata ushuru kwa siri. sasa hawatakuwa na njia zaidi ya kulipa ushuru halali.

Lakini pia, kama nilivyoeleza hapo juu, mfumo huo utaendelea kuwa mwiba kwa halmashauri zilizokuwa zinategemea ushuru huo kuongeza mapato ukizingatia kuwa tayari serikali ilishatoa maelekezo ya kufutwa kwa halmashauri itakayoshindwa kufikia asilimia 80 ya makusanyo.

Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), uliofanyika mjini Mpwapwa, mkoani Dodoma 2016.

Kwa sasa halmashauri hizo zitalazimika kutafuta vyanzo vingine vipya ili kuepuka kufutwa.

Ni vema serikali inapofanya maamuzi iangalie matokeo ya pande zote mbili ili kuondoa misuguano na migongano inayoweza kutokea ili kusaidia katika usitawi wa maendeleo ya taifa letu.

Columnist: mwananchi.co.tz