Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Serikali ilimpenda au ilimuogopa Mengi?

55731 MENGI+PIC

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kilio kikubwa cha bilionea Reginald Mengi ni sera za Serikali kiuchumi. Mpaka amefariki dunia, amekuwa kielelezo cha watu wenye uthubutu wa kupinga utaratibu wa Serikali hususan utoaji fursa za uwekezaji.

Mwanzoni mwa miaka ya 1970, Mengi aliporejea nchini akitoka Scotland, alikokwenda kusomea shahada ya uhasibu, alikuta nchi imeshashika usukani katika mfumo wa ujamaa. Na kwa vile ndoto yake ilikuwa biashara, aliona mazingira yalikuwa magumu mno.

Katika kitabu chake, “I Can, I Must, I Will; The Spirit of Success”, kwa maana ya “Naweza, Lazima nifanye, Nitafanikiwa; Nafsi ya Mafanikio”, anasema kuwa nyakati za ujamaa fursa zilikuwa chache na zilitolewa kwa upendeleo kwa Watanzania wenye asili ya Asia.

Anasema Watanzania weusi walidhibitiwa kufanya biashara na kufanikiwa, kwa sababu walihofiwa kama wangekuwa na fedha nyingi basi wangehodhi siasa za nchi kutokana na nguvu kubwa ya kiuchumi ambayo wangekuwa nayo.

Anatolea mfano alipoanzisha kiwanda cha vinywaji baridi cha Bonite Bottlers (Coca Cola), kwamba mwaka 1987, Mwalimu Julius Nyerere alikikosoa kwa maelezo kuwa malighafi zake zilitoka nje, kwamba huo ulikuwa ubepari.

Mengi anasema, kiwanda cha Fahari Bottlers Limited, kilianzishwa mwaka 1983, Nyerere akiwa madarakani, kikawa kinazalisha bidhaa za Pepsi, alikiruhusu kwa sababu kilikuwa cha Watanzania wenye asili ya Asia na hakukikosoa.

Habari zinazohusiana na hii

Ukimsoma Mengi, utaona kwamba matumaini ya kufanikiwa zaidi kibiashara ni baada ya Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi kuingiza sera za ulibelari na kuruhusu kila mtu afanye anachoweza ilimradi asivunje sheria. Hata hivyo, alilalamika kuwa kipindi cha Mwinyi bado Nyerere alikuwa na nguvu sana.

Pia, Mengi aliwahi kuingia kwenye mgogoro na Wilson Masilingi alyekuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa. Sababu ilikuwa ni uwekezaji wa Hoteli ya Kilimanjaro, sasa Hyatt Regency, The Kilimanjaro.

Mengi alitaka kuwa mwekezaji wa hoteli hiyo, lakini alinyimwa, wakapewa wawekezaji kutoka nje. Mengi aliishambulia Serikali kwamba haikuwa ikiwapa kipaumbele wazawa, na ilipendelea zaidi wageni. Haya ni malalamiko ya muda mrefu ya Mengi.

Aliamini kuwa wazawa wanapaswa kupewa kipaumbele katika fursa za uwekezaji ndani ya nchi. Hata pale wazawa wangekuwa na uwezo mdogo, Mengi aliamini kwamba lilikuwa jukumu la Serikali kuwawezesha kufikia viwango vinavyokidhi uwekezaji husika.

Kipindi cha Rais wa nne, Jakaya Kikwete, mara kadhaa Mengi aliingia kwenye mgongano na mawaziri. Zipo nyakati alituhumiwa kuihujumu Serikali ya Kikwete. Aliyekuwa mbunge wa Mkuranga, Adam Malima aliwahi kumsema Mengi kutumia vyombo vyake vya habari kujitangaza kuliko Rais.

Hoja hiyo ya Malima ilisababisha mzozo mkubwa bungeni, huku Mengi akisimama imara kujitetea. Televisheni ya ITV ilirudia taarifa za Mengi na Rais Kikwete kuonyesha kwamba Malima hakusema kweli. Mengi pia alimwandikia barua Spika Samuel Sitta kulalamika. Mwisho Malima aliomba radhi.

Wakati huo pia, ukatokea mzozo kati ya Mengi na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Sophia Simba. Tuhuma zilitolewa na Sophia kuwa Mengi hakuwa mwana CCM na alikuwa anaihujumu Serikali, vilevile alimtuhumu kutaka kuwania urais.

Mengi aliitisha mkutano na vyombo vya habari, akaonesha kadi zake za Tanu kisha ya CCM ya mwaka 1977. Akasema hajawahi kuwa na mpango wa kuwa Rais. Hata hivyo, ilikuwa dhahiri kwamba hakukuwa na kuaminiana kati ya Mengi na mawaziri wa Kikwete.

Uliibuka mvutano mwingine pale Mengi alipoitisha vyombo vya habari na kulalamika kwamba alipewa taarifa kutoka kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri, kwamba kuna waziri alipendekeza Serikali imfilisi Mengi mali zote.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha alimpa Mengi siku saba awe amethibitisha madai yake. Mengi akamjibu siku saba alizompa ni nyingi sana, kwamba angempa siku moja ingetosha. Siku iliyofuata, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, wakati huo akiwa mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alimtaja Masha kuwa ndiye alitoa wazo la kumfilisi Mengi kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri. Sakata hilo likaisha kimyakimya.

Hautasahaulika mzozo kati ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo dhidi ya Mengi. Mzozo ulihusu uwekezaji sekta ya madini na uvunaji gesi asilia. Muhongo alisema hakuna mzawa mwenye uwezo. Mengi aliamini wazawa wakipewa kipaumbele wataweza.

Aliwahi kufanya kikao na vyombo vya habari na kuelezea taarifa alizozipata ndani ya Jeshi la Polisi kuwa kulikuwa na mpango wa kumwekea dawa za kulevya mtoto wake ili kumkamata nazo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ili kuifanya jamii imuone yeye na familia yake ni wauza dawa za kulevya.

Mizozo hiyo ya mara kwa mara ambayo Mengi alikuwa nayo dhidi ya Serikali, na kwa kukumbuka kauli yake kwamba Watanzania wazawa (weusi), walianza kubaguliwa kwenye fursa za kiuchumi kwa hofu kwamba wangehodhi siasa na utawala, je, Serikali ilikuwa ikimuogopa Mengi au ilimchukia?

Pamoja na misimamo hiyo, Mengi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magazeti ya Serikali (TSN), Kamishna wa Tume ya Mishahara (SRC), Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu Tanzania (NBAA), Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Kamishna wa Tume ya Kupambana na Ukimwi (TACAIDS) na kadhalika. Nafasi hizo zote ni za kuteuliwa na Rais. Amekuwa akiteuliwa tangu wakati wa Nyerere hadi Kikwete. Je, Serikali ilimpenda?

Mengi hakufurahia mfumo wa Serikali kujigeuza dereva wa biashara badala ya kuwaacha huru wafanyabiashara. Aliumia kuuawa kwa vyama vya ushirika. Alisema, vyama hivyo viliuawa ili kuwafanya Watanzania weusi wasiendelee na kupata nguvu kubwa ya kiuchumi. Kwamba wangehodhi siasa.

Aliamini kuwa Watanzania wenye asili ya Asia walipendelewa na Serikali. Takriban muongo mmoja uliopita, alitaja majina matano ya wafanyabiashara Watanzania wenye asili ya Asia kuwa wanafilisi nchi. Aliwaita mafisadi papa. Je, Mengi alikuwa mbaguzi? Hakuwapenda Watanzania wenye asili ya Asia.

Tumuombee Mengi pumziko jema. Kila mja ni wa Mwenyezi Mungu na kwake ndipo yalipo marejeo ya lazima.



Columnist: mwananchi.co.tz