Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sekta ya uvuvi ina utajiri mkubwa kuliko migodi

59799 Mtatiro

Sun, 26 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kama kuna sekta ambayo imebeba utajiri wa nchi yetu na bado haijatumiwa ipasavyo ni ya uvuvi. Nchi yetu ina maziwa ya kutosha. Sehemu ya uso wake takribani kilomita za mraba 61,500 imekaliwa na maziwa – Victoria, Tanganyika, Nyasa, Rukwa, , Natron, Manyara, Burigi, Barangida, Jipe, Babati na mengineyo.

Tanzania pia ina mito mikubwa mingi kama Rufiji, Ruaha, Pangani, Wami, Malagarasi, Kagera, Mara, Ruvuma, Songwe, Ruvu na mingine. Mjadala huu utajiepusha kidogo na utajiri uliopo katika Bahari ya Hindi ambao haujatumika ipaavyo.

Utajiri wa kipekee

Maziwa na mito ni migodi ya kipekee ambayo haina uwekezaji mkubwa, inahitaji uwekezaji wa kawaida kufanikisha uvunaji wa utajiri ukilinganisha na uwekezaji wa migodi ya madini.

Kwa hakika, hakuna anayepeleka chakula ziwani au mtoni. Mito na maziwa vinajilisha vyenyewe, ni kama tu mbugani kwenye wanyama pori, hakuna apelekaye chakula kulisha kuwalisha swala wala nyumbu.

Kama utafiti mkubwa ukifanyika, tutagundua kuwa mito na maziwa vilivyoko Tanzania ni utajiri mkubwa kuliko utajiri wa madini yote tuliyonayo ikiwa yataunganishwa pamoja.

Pia Soma

Tumekwama wapi?

Tumesahau dhana muhimu ya sekta inayoajiri watu wengi dhidi ya sekta inayoajiri watu wachache. Kitakwimu, ziwa na mito vinaajiri Watanzania wengi zaidi kuliko migodi yote mikubwa ya madini.

Kwa kufuata ile kanuni ya maendeleo ya kuwekeza kwenye sekta inayoajiri watu wengi zaidi ili kujenga maendeleo ya vitu na ya watu kwa pamoja, Tanzania haina budi kuendelea kujielekeza katika kuhuisha utajiri uliomo maziwani na mitoni.

Tumekwama kwa sababu hatujamuua kuwekeza nguvu zetu kidogo, nguvu za rasilimali fedha na uvunaji stahili wa mazao ya majini.

Wavuvi wakiinuliwa

Inawezekana wavuvi wakainuliwa. Ziko changamoto kadhaa zinazowakabili na ambazo zinapaswa kuwa msingi wa maamuzi yetu ili tuisaidie sekta ya uvuvi ambayo inaweza kulikomboa taifa.

Moja ya changamoto inayoendelea ziwani na mitoni ni uvuvi haramu, japo kwa sasa umepungua sana lakini bado upo na unaendelea kwa sababu wapo watu wenye dhamana za kuudhibiti na wameamua kutofanya hivyo.

Iko changamoto ya wavuvi kutoka Kenya na Uganda. Hawa huvuka mipaka ya ziwa kutoka kwenye nchi yao na kuingia upande wa Tanzania. Hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tanzania ikiwemo ile ya kudhibiti uvuvi haramu au kuzuia uvunaji samaki wachanga vinakwamishwa na majirani zetu. Wakati Tanzania inazuia, wenzetu wanaendelea kuvamia eneo letu la ziwa na kuvuna samaki waliokua kidogo.

Uholela wa uvuvi

Sekta ya uvuvi imeachwa kuwa holela mno, kila mvuvi anaingia ziwani na mtoni kwa njia anayoijua yeye na anatoka kwa njia anayojiua yeye.

Mialo yetu ambayo ingelitumika kudhibiti nani wanaingia na nani wanatoka ziwani imekufa. Tumebaki na mialo ambayo haina tija kubwa kwa taifa kama ilivyotegemewa.

Utaratibu wa sasa wa uingiaji na utokaji wa ziwani na mitoni unafanya wavuvi wengi zaidi wasilipe kodi hata kama wamevuna samaki wengi kwa ajili ya biashara, wavuvi hao wanapotoka hutumia mialo isiyodhibitiwa na serikali na hutokomea na samaki sokoni, mapato ya nchi yanapotea.

Maziwa ya utajiri wa hali ya juu, wa uhakika, utajiri wa nyavu na ndoano usiohitaji kuchimba mashimo wala kuajiri wataalamu wa kimataifa na ujuzi wa hali ya juu kama kwenye madini.

Tufanye nini?

Tuweke sheria ambayo itataka kila mvuvi awe amesajiliwa kwa kubaini mvuvi mdogo na mvuvi mkubwa, na kisha kila mmoja apitie mwalo unaoeleweka, na akitokea kwenye mwalo awepo ofisa uvuvi na aidhinishe kuwa samaki waliovuliwa wako salama.

Kuwekwe sheria, kuwa mtu akivua kilo 0 - 20 hizo ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na asitozwe ushuru wowote. Na kwamba kuanzia kilo 21 kwenda mbele hao ni samaki wa biashara na watozwe kodi kulingana na viwango stahiki.

Mfano, kwa kila kilo moja ya samaki, Sh1 – 5 itengwe kurudi kusaidia sekta ya uvuvi kwa maana ya kutoa mikopo nafuu, elimu ya ujuzi wa uvuvi wa kisasa na kusaidia manunuzi ya vifaa vya kisasa vya uvuvi kwa makundi mbalimbali ya wavuvi.

Kuwe na mkakati wa kutafuta fedha na kuwakopesha wavuvi wadogo na kuzizungusha kwa wavuvi mbalimbali. Hizi fedha zitasaidia kuwapa uwezo wavuvi ambao wanakuza uwezo wao wa kimitaji na zitasaidia kuwafanya waanze kukua na kuwa wavuvi wa kati na hatimaye wakubwa.

Tukiamka kutoka usingizini bila shaka tutajihakikishia uvuvi ukitupatia fedha nyingi kuliko sekta zingine zozote hapa Tanzania. Kwa fikra za mbali zaidi hatujazungumza kuhusu ufugaji majumbani.

Huu ni ufugaji unaokwenda kisasa na ambao umeyasaidia mataifa mengi duniani. Hatuwezi kwenda kwenye fikra hiyo kwa sababu uvunaji wa samaki wa maziwa yetu na mito yetu bado hatujaufanyia kazi. Tunahitaji nguvu na mikakati zaidi, tumekalia utajiri usiotumika, ambao unaendelea kunufaisha matajiri wachache.

Columnist: mwananchi.co.tz