Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sekta ya michezo ina majibu mepesi yasiyojibiwa

14123 Goshashi+allan TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kamwe sitachoka kuuliza hivi Tanzania tumefanya dhambi gani katika ardhi yetu yenye rasilimali nyingi ambazo zingeweza kusaidia katika sekta mbalimbali ikiwamo michezo?

Je, ni kwa nini Serikali haitaki michezo iwe ni moja ya kipaumbele chake katika mipango ya taifa ili kuiondoa michezo katika kundi la ajira zisizo rasmi?

Hivi Serikali haitambui kwamba michezo nchini haiwezi kufanikiwa bila Serikali kutia mkono? Je, ni kwa nini Serikali haitaki kuibadilisha sera ya maendeleo ya michezo nchini ambayo imepitwa na wakati?

Je, hivi Serikali Kuu haioni Halmashauri za Miji, Manispaa na Vijiji zinabadilisha matumizi ya maeneo ya wazi na viwanja vya michezo kuwa sehemu za biashara? Hivi ni kweli hakuna kiongozi wa Serikali anayeweza kuvirudisha viwanja hivyo kutumika kwa shughuli za michezo?

Je, kwa nini hatupati viongozi serikalini watakaojenga vituo vya michezo katika kila Wilaya? Je, ni kwa nini hatupati viongozi serikalini watakaowahamasisha Watanzania mijini na vijijini kuwa na viwanja vipya vya michezo kwa ajili ya watoto wao mitaani mwao?

Hivi ni kwa nini Serikali yetu haijiulizi kwa nini michezo nchini imekosa mikakati ya kibiashara, wadhamini na viongozi weledi? Pia, ni kwa nini wawekezaji wa ndani na nje ya nchi hawawekezi fedha zao katika sekta ya michezo nchini?

Je, ni kweli Baraza la Michezo la Taifa (BMT) linakidhi mahitaji ya wakati tulio nao? Ni kwa nini Wizara inayohusika na michezo isiwe ni Wizara ya Michezo na Utamaduni tu?

Je, ni kwa nini shule za msingi na sekondari nchini zinakosa viwanja vya michezo? Au ni kwa nini zile baadhi ya shule zenye viwanja vya michezo vinabadilishwa matumizi?

Je, ni kwa nini hatuyaboreshi mashindano ya Umitashumta na Umisseta? Je, ni kwa nini katika ngazi ya Wilaya, Mkuu wa Wilaya asihamasishe mashirika, viwanda na wafanyabiashara kudhamini mashindano hayo ya Umitashumta na Umisseta? Na kwa nini isifanyike hivyo hivyo katika ngazi ya Mkoa?.

Je, Serikali haioni kwamba kuna upungufu mkubwa wa makocha katika shule za sekondari na shule za msingi nchini? Je, Serikali haioni somo la michezo linahitajika kufundishwa katika shule za msingi mpaka sekondari kama masomo mengine?

Je, kwa nini Serikali inataka tufanye vizuri katika mashindano ya Afrika, Dunia, michezo ya Jumuiya ya Madola au michezo ya Olimpiki wakati inajua haina mfumo wa kumuandaa mwanamichezo nchini kutumia kipaji alichopewa na Mwenyezi Mungu kujikwamua katika lindi la umaskini?

Hivi ni kwa nini Serikali inakwepa gharama ya kuandaa wanamichezo wetu?, Je, haifahamu kwamba haiwezi kukwepa jukumu la kuweka miundombinu ya michezo tofauti tofauti nchini?

Je, ni kitu gani kinachowazuia wabunge kufanya kazi yao ya kuisimamia Serikali ili iweze kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika miradi ya maendeleo ya michezo kama kuweka miundombinu ya michezo?

Je, viongozi wa michezo nchini wanajua majukumu yao kama viongozi wa michezo? Je, wanajua matatizo, changamoto na vikwazo vya maendeleo ya michezo nchini? Je, viongozi wetu wa michezo ni sehemu ya suluhisho au ni sehemu ya tatizo? Je, wana mipango bora ya kuwa na vyanzo vya mapato? Je, wana program bora za vijana na grassroots?

Nimalizie kwa kuuliza tena swali hili, Je, Tanzania tumefanya dhambi gani katika ardhi yetu yenye rasilimali nyingi ambazo zingeweza kusaidia sekta mbalimbali ikiwamo michezo?

Columnist: mwananchi.co.tz