Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sawa bosi wa mkoa, walevi pia ni nguzo ya uchumi

35151 Edo+kumwembe Eddo Kumwembe

Tue, 8 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maisha yanakwenda kasi. Nimeona mahala mkuu wa mkoa amebadili agizo lake la zamani. Awali alipoingia madarakani alitaka baa zifunguliwe saa kumi jioni na kufungwa saa tano usiku. Sijui ilitokana na sababu za usalama au maadili. Sijui kwa kweli.

Majuzi bosi wangu wa mkoa amesema anaandaa utaratibu ili baa zifunguliwe kwa saa 24 ili mradi tu wauzaji wawe na mashine za EFD.

Sitaki kujua kwa nini hii sababu ya EFD isingewekwa tangu nyakati za tamko la awali. Sitaki kujua kabisa.

Hata hivyo, ninachojua ni kwamba wakubwa wetu kila siku wanajifunza kitu kuhusu mchezo wa uchumi. Mchezo huu haueleweki. Wakati ukiwa na nia njema ya kudhibiti hili, kumbe unabomoa uchumi kwa njia nyingine. Inashangaza.

Binafsi nimeishia darasa la saba tu lakini kila siku najifunza uchumi kutokana na mienendo ya mabosi wetu wa kisiasa. Kwa mfano, kwa sasa hali ya mapato ipo taabani kidogo na Namba Moja anataka kuhakikisha tunakusanya kila senti ya kodi.

Unapofungua baa saa kumi jioni halafu unaifunga saa tano usiku anayeathirika zaidi sio mlevi. Wanaanza kuathirika watu wa TBL na wenzao, kisha inaathirika Serikali na mapato yake. Hawa watu wa TBL na wenzao ni vinara wa kulipa kodi serikalini. Kama mauzo ya bidhaa zao yanakuwa saa saba tu kwa siku ni wazi kwamba wanakosa fedha nyingi na Serikali inakosa fedha nyingi.

Dunia inashangaza sana. Kumbe watu ambao wanaonekana hawana maadili ndio wanaongoza kwa kulipa kodi. Miongoni mwao wapo walevi. Uchumi wetu kwa kiasi fulani unashikiliwa na wao, kisha wavuta sigara. Wanaouza vitabu vya dini nadhani hawapo katika orodha hii.

Baniani mbaya kiatu chake dawa. Nadhani sasa wakubwa wetu wameanza kuelewa jinsi misingi ya uchumi ilivyo na utata. Leo unatoa agizo hili kwa jazba na labda kufikiria kwamba unaisafisha jamii na kuiweka katika maadili safi, kesho unakuta agizo lako linaathiri uchumi kwa kiasi kikubwa.

Nadhani mabosi wetu wawe wanashauriana vema na washauri wao kabla hawajafika katika majukwaa au vipaza sauti na kutoa maagizo mbalimbali. Bosi wetu wa mkoa angetafakari mapema kabla ya agizo la mwanzo nadhani wachumi wangemshauri vema zaidi.



Columnist: mwananchi.co.tz