Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sare ya mwalimu ni maadili aliyonayo

11161 SARE+PIC.png TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sare ni nguo rasmi zinazofanana ama zinazovaliwa na kikundi cha watu kama vile wanafunzi, wafanyakazi au askari.

Watu katika kada nyingine zaidi ya ualimu huweza kutambulika kiurahisi shughuli wanazofanya, kwa sababu ya kuwa na sare za kazi.

Kwa mfano, tunaweza kumtambua muuguzi, daktari, askari polisi, askari magereza, askari wa usalama barabarani au mwanajeshi kwa sababu ya sare yake.

Madereva hutii maelekezo ya mtu aliyevaa sare ya askari wa usalama barabarani na kuongoza magari katika makutano ya barabara fulani bila kulazimika kuwa na mashaka juu yake.

Hata hivyo, matumizi yasiyo sahihi ya sare yamewatia hatiani baadhi ya watu. Tumeshuhudia mara nyingi watu wakikamatwa kwa kosa la kujifanya ni askari, daktari au mwanajeshi kwa kuvalia mavazi rasmi ya kada hizo.

Maadili, nidhamu na weledi

Maadili ni sare pekee ya walimu ambayo imekuwa ikiwatambulisha popote pale wanapokuwa. Sare hii inapokosekana kwa mwalimu, jamii huanza kuwa na mashaka kuhusu mwalimu huyo kama kweli ni mwalimu au ni ‘kanjanja’.

Kwa mfano, walimu wanapokuwa njiani, sokoni, katika nyumba za ibada, viwanja vya michezo na burudani au wanapokuwa katika foleni wakingoja kuhudumiwa jamii, imezoea kuwatambua kutokana vitendo vya maadili wanayoonyesha.

Maadili hupaswa kwenda sambamba na uwajibikaji na nidhamu katika taaluma yenyewe yaani weledi. Tunategemea mwalimu bora awe na nidhamu na maadili ya ualimu; aonyeshe weledi katika taaluma yake.

Zipo sheria, kanuni na maadili ya kazi ya ualimu ambazo walimu hawana budi kuziheshimu ili kuendelea kuaminiwa na jamii. Duniani kote, ualimu ndiyo kada pekee iliyokasimiwa dhamana ya kujenga na kuendeleza taifa husika.

Dhamana hiyo waliyonayo walimu inatokana na ukweli kwamba kada nyingine zote ni mazao ya walimu. Hatutaweza kupata wahandisi, makarani, madaktari, wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi bora katika jamii kama hakuna walimu bora.

Hapa nchini, mwalimu amekuwa akisimamiwa na mamlaka mbalimbali kama vile Chama cha Walimu (CWT), vyama vya wafanyakazi na tume ya utumishi wa walimu. Pamoja na vyombo hivyo, bado changamoto za walimu zimekuwako miaka nenda rudi. Pengine huu uwe wakati mwafaka wa jamii na mamlaka husika kutafakari kama kuna haja ya kuwa na bodi ya walimu itakayosimamia shughuli za kitaaluma, maadili, nidhamu, maslahi bora na weledi.

Mwalimu ni kioo cha jamii

Faraja kubwa ya mwalimu ni kuona wanafunzi wake wakistawi na kusababisha mabadiliko chanya katika jamii.

Matendo ya mwalimu huaminiwa na kuigwa kwa haraka sana na wanafunzi wake. Wanafunzi wengine hufikia hatua ya kuwa na misimamo kama ya walimu wao. Kuongea, kutembea, kutafakari na kufanya mambo kama vile walimu wao.

Jamii haina budi kutambua kuwa mwalimu aliyeajiriwa serikalini na yule wa sekta binafsi, wote hawa wana dhamana sawa ya kujenga taifa. Hivyo, sheria, kanuni za maadili na nidhamu kwa watumishi zinawahusu wote.

Mwalimu anapoacha kuvaa sare yake

Walimu ni binadamu, nao wana mahitaji kama binadamu wengine. Tofauti yao inaanza mara tu pale walipoamua kuwa walimu. Ualimu ni wito na mtu akitaka kujua kuwa huo ni wito, ajaribu kuielimisha jamii kwa njia yoyote ile. Vile vikwazo atakavyovikabili na uamuzi sahihi atakaochukua, utathibitisha kilichomo ndani yake kama ni mtu wa maslahi ama utu.

Kwa kuwa nao wana mahitaji na udhaifu wa kibinadamu, wakati mwingine wanahitaji kukumbushwa. Wakati mwingine hukata tamaa, wanahitaji kutiwa moyo; wakati mwingine stahiki zao hucheleweshwa, wanahitaji kuhudumiwa ipasavyo.

Walimu wanapoacha kuvaa sare yao pekee ya maadili, matatizo lukuki huiandama jamii husika. Kwa mfano, mwalimu mlevi au anayetumia madawa ya kulevya hujiondolea heshima mbele ya umma.

Jamii inategemea kuona mwalimu akiwa mzalendo kwa nchi yake, huku akijivunia taaluma yake pasina kuionea haya.Pia, awe mwenye staha, lugha safi, mavazi ya heshima, tabia njema, mwonekano nadhifu ulio tofauti na watu wenye tabia zisizofaa.

Hoja hizi zinashadadiwa na walimu wastaafu, Mzee Kapongo wa Tanga na mwalimu Katunzi wa Nzega. Wanasema kuwa heshima ya ualimu nchini inaporomoka, kutokana na baadhi ya walimu kutofuata maadili ya ualimu hivyo kuwaondolea heshima yao ya kuwa kioo cha jamii.

Walimu wanapoacha kuhubiri maadili mema kwa vitendo, wanakuwa kama chumvi iliyoharibika. Wanakuwa wamefanya hujuma kwa taaluma yao na madhara yake hata wao huwapata.

Wanaporuhusu mnyororo wa matatizo uendelee badala ya kuukata, nao ipo siku wataendeshwa na dereva waliyemharibu alipokuwa mwanafunzi; watachomwa sindano na muuguzi au daktari asiye na maadili.

Watatozwa hongo na watafanyiwa matendo mabaya na waharifu waliowatengeneza wao wenyewe darasani pasipo kujua wakati mwingine kwa kuwaonyesha majibu ya mtihani. Pia, watadhulumiwa haki na mahakimu waliowaharibu wenyewe.

Kwa hiyo, ustawi wa taifa lolote duniani upo mikononi mwa walimu. Ni kwa jinsi gani shule zitasaidia ujenzi wa taifa hilo imara, inategemea ni kwa namna gani walimu wanavalia sare yao ya maadili, taaluma, nidhamu na weledi.

Pia, jamii kwa jumla nayo ina wajibu wa kuhakikisha walimu hao wanaondolewa vikwazo vinavyowasababisha washindwe kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Walimu pia, wathamini dhamana waliyonayo kwa mwanafunzi kuwa ni ya kipekee, hivyo watimize wajibu.

Columnist: mwananchi.co.tz