Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Safari yangu katika msiba wa Maria na Consolata-2

9519 Safari+pic TZWeb

Tue, 19 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Tumekubaliana watazikwa Tosamaganga siku ya Jumatano,” alisema. Makaburi ya Tosamaganga ni yale ambayo huwa wanazikwa watawa wa Kanisa Katoliki.

“Walichagua wenyewe kuwa watazikwa tunakozikwa sisi kwa hiyo, eneo hilo tunawapeleka kwa sababu ya mapenzi yao,” anasema Mkuu wa Shirika la Masista la Maria Consolata, Jane Nugi.

Wakati Sista Nugi anazungumzia mazishi, tayari walikuwa wamemaliza kikao cha maandalizi kilifanyika kwenye nyumba yao, Kihesa Mjini Iringa na kuhusisha ndugu zao.

Kaka wa Maria na Consolata, David Mwakikuti na mama yake mkubwa, Anna Mshumbusi ni miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo.

David anasema walizaliwa watoto watano kwa baba yao, Wilfred Mwakikuti na mama yao Naomi Mshumbusi.

“Baada ya wazazi wetu kufariki sisi watatu tulichukuliwa na wajomba, Maria na Consolata wakalelewa na masista,” anasema.

Anasema wakiwa wadogo hawakuweza kutembeleana hadi walipofikia umri mkubwa.

“Kwa hiyo nilipokua niliweza kwenda kuwatembelea hasa wakati wa mahafali, nimeumia kuwapoteza dada zangu yapo mengi makubwa niliyojifunza kwao hasa upendo,” anasema.

Jeneza la aina yake

Kati ya maajabu yaliyojitokeza kwenye msiba huo ni aina ya jeneza walilokuwa wamehifadhiwa pacha Maria na Consolata.

Karakana ya Mandela Furniture ndiyo iliyochonga jeneza hilo kubwa. Kutoka Hospitali ya Rufaa Iringa hadi Kitwiru, eneo lilikokuwa linatengenezwa jeneza hilo ni kilomita tatu au nne hivi.

Jeneza la kawaida huwa na upana futi 1.5, la Maria na Consolata lina upana wa futi tatu, urefu wa futi tano pia kina cha futi mbili wakati la kawaida ni futi moja.

Fundi wa jeneza hilo, Oscar Mfugane anasema hajawahi kuchonga jeneza la aina hiyo. “Ni jeneza la kipekee na tunamshukuru Mungu kwa heshima tuliyopewa kuandaa jeneza la pacha hawa,”anasema.

Padre Benedict Chavala aliyepewa kazi ya kusimamia ujenzi wa kaburi lao, anasema kama ilivyo kwa jeneza, ndivyo kaburi lilivyokuwa na ukubwa huo.

Siku ya mazishi!

Tangu saa 11.00 alfajiri, watu walikuwa wameshafurika nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa Iringa.

Ilinibidi kuungana na waombolezaji wengine kusubiri mwili wa Maria na Consolata. Baridi ilikuwa kali japo wengi walikuwa wakitetemeka, hakuna aliyeinua mguu kuondoka, badala yake watu waliongezeka.

Saa 1.00 asubuhi milango ya chumba cha kuhifadhia maiti ilifunguliwa na Watawa (Masista) wakiongozwa na Sista Jane, waliongoza ibada fupi kabla ya kuuchukua mwili. Gari za polisi na pikipiki zenye ving’ora zilikaa tayari kuanza msafara wa kuwapeleka Maria na Consolata katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ruaha kwa ibada ya mazishi.

Wakati miili inatolewa nje ya chumba hicho, nilihisi kupigwa sindano ya ganzi mwili mzima, nguvu ziliisha na huku machozi yakitoka nisijue cha kufanya.

Wakati huo nilipokea pia simu ya maelekezo ya kazi kwa mhariri wangu Esther akinisihi niwe jasiri.

“Juzi na jana ulifanya kazi nzuri, leo napenda kuona kazi kama hiyo, nunua glucose, kunywa maji na jipe nguvu umalize kazi yako,” aliniambia. Nilifuta machozi, nikaingia kwenye gari aina ya Canter, iliyokuwa imepakia wapiga picha.

Msafara uliondoka huku njiani mamia ya watu wakipunga mikono kama ishara ya kuwaaga Maria na Consolata.

Viwanja vya Rucu

Vilio na maombolezo vilikuwa vimetawala. Miili ya pacha hao iliwasili viwanja vya Rucu na kupokewa na umati. Japo ilikuwa asubuhi na siku ya kazi, mji wa Iringa ulizizima kwa huzuni.

“Hawa ni mashujaa, maisha yao yamejaa ushuhuda na lipo jambo la kujifunza kutoka kwao,” anasema Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako.

Baada ya miili hiyo kuwasili iliwekwa kwenye hema maalum ili watu waanze kutoa heshima zao za mwisho.

“Buriani dada zangu, Buriani Maria na Consolata. Najua sitawaona tena niliwapenda mno ila kumbe Mungu anawapenda zaidi ameamua kuwachukua,” ilikuwa sauti ya msichana aliyekuwa akiwahudumia, pacha hao ambaye pia aliwauguza wakiwa Muhimbili.

Nilijisikia uchungu, nikazunguka nyuma ya jukwaa la viongozi ili machozi yangu yasionekane nikiwa kazini.

Shughuli za kuaga miili ya mapacha hao zilianza saa mbili hadi saa nne. Hata hivyo umati mkubwa wa watu uliokuwepo kwenye msiba huo haukuisha.

“Sasa basi, tunapaswa kuanza ibada. Shughuli za kutoa heshima ya mwisho zitaishi hapa,”alisema mmoja wa waratibu wa shughuli hiyo.

Kauli za viongozi

“Wameishi wawili kwa miaka zaidi ya 20. Walichukuliana na kuvumiliana, mabinti hawa naweza kuwaita mashujaa. Ni mashujaa wa taifa letu,” anasema Profesa Ndalichako.

Kila kiongozi aliyesimama alizungumza ujumbe mzito kuhusu Maria na Consolata.Ndalichako na viongozi wote waliowasili kwenye msiba huo hawakuhimili uchungu na wingu zito la simanzi lililogubika eneo hilo, kila mmoja kwa wakati wake alidondosha machozi.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu, Ikupa Alex hakuweza kumalizia hotuba yake kwa sababu kilio kilimkuta njiani.

“Lipo la kujifunza kwa Maria na Consolata, kuzaliwa, kuishi na kifo chao kina sababu. Upendo waliouonyesha, kutokata tamaa kwao, uvumilivu na kujituma kunatupa somo kubwa,” anasema Ikupa.

“Wamepigana vita vikali, imani wameilinda na mwendo wameumaliza”.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe, Mhashamu Alfred Maluma alitumia muda mwingi wa mahubiri yake kuitaka jamii iache kuwatenga watu wenye ulemavu. “Tusiwatenge wenzetu wenye ulemavu, tuwapende na kuwahudumia na kila mmoja wetu anapaswa kuwaomba msamaha,” alisema.

Mbali na mawaziri, msiba huo pia ulihudhuriwa na wabunge, wakuu wa wilaya na viongozi wengine wengi wa dini, akiwamo Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville.

Safari yao makaburini

Saa tisa alasiri safari ya kwenda kuzika ilianza, kwa mara nyingine umati mkubwa ulijipanga barabarani kuwaaga pacha hao ambao walizikwa katika makaburi ya Tosamaganga, eneo ambalo huwa wanazikwa watawa wa Kanisa Katoliki. Baada ya dakika 45 au saa moja, miili yao ikawa imewasili makaburini. Na ilipofika saa 11.50 jioni, walikuwa wameshahifadhiwa kwenye nyumba yao ya milele.

Kuzaliwa kwao

Pacha hao walizaliwa miaka 21 iliyopita katika Hospitali ya Misheni ya Ikonda, Makete, Iringa. Awali hawakujulikana sana hadi walipoanza darasa la kwanza Shule ya Msingi Ikonda. Sista Virgliana Duraviana ndiye aliyewapokea baada tu ya kuzaliwa. “Tuliogopa huenda wasiishi muda mrefu, tulimwomba baba yao ili tuwatunze alikubali na ndipo niliwapatia jina la Maria na Consolata,” anasema.

Ndoto yao

Ndoto yao kubwa ilikuwa ni ualimu. Nakumbuka nilipoongea nao, mbali na ualimu waliniambia wanatamani kuona watu wenye ulemavu wanaishi vizuri na kusaidiwa kama walivyosaidiwa wao.

Siku zote walipambana bila kujali hali zao na kukata tamaa ilikuwa mwiko.

Maisha yao ya kawaida

Sister Nugi anasema: “Waliishi maisha yao kwa imani, walipenda kusali pamoja na wanafunzi wengine”.

Walipenda kuona watu wenye ulemavu wanaheshimiwa na kuthaminiwa, hawakupenda kujitenga na siku zote waliamini wanaweza kufanya chochote.

Kuumwa kwao

Desemba 2017 walianza kuumwa wakapelekwa Hospitali ya Misheni ya Ipamba, wakahamishiwa Hospitali ya Rufaa Iringa, nako pia walipewa rufaa kupelekwa Muhimbili. “Vipimo Muhimbili vilionyesha Maria alikuwa na matatizo ya mapafu, hakuweza kupumua bila Oxygen. Miezi minne baadae walirejeshwa tena Iringa,” anasema.

Dk Kundy anasema wakiwa Iringa, Maria aliendelea kupumua kwa kutumia Oxygen hadi Juni 2, walipoaga dunia..

Hakika tunamshukuru Mungu kwa maisha aliyowajaalia Maria na Consolata. Yapo mengi ya kujifunza toka kwao.urian Maria na Consolata.

Mwisho

Columnist: mwananchi.co.tz