Ni saa 4.30 hivi usiku wa Juni 2 mwaka huu, simu yangu inaita. Naitazama kabla sijapokea, naona jina la Mbunge wa Viti Maalum, mkoa wa Arusha, Amina Mollel.
Napokea simu hiyo kwa furaha nikijua rafiki yangu wa siku nyigi amenikumbuka hivyo ananisabahi. Hata hivyo mara baada ya kupokea nasikia mtu akitamka: “Pole sana Tumaini,” nashtushwa na sauti yake ya huzuni inayoashiria kwamba alikuwa akilia.
“Pole ya nini tena? Kuna nini kwani?” Nilihoji nikishindwa kuitikia pole yake. “Rafiki zako, wadogo zako Maria na Consolata hawapo tena duniani, wamefariki jioni hii…nimethibitisha hilo, kuna mtu yupo Iringa amenihakikishia,”ananieleza Amina kwa sauti yake ileile inayoashiria kwamba yuko kwenye huzuni.
Niliumia sana na sikuweza kuzungumza zaidi na Amina. Badala yake niliikata simu hiyo ambayo iliita mara ya pili.
Kwa hakika sikubisha kuhusu taarifa hizo kwani zilikuwa zimepita dakika chache tangu Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena anipigie akitaka niulizie hali za pacha hao, Maria na Consolata.
Kwa wakati huo taarifa za kifo cha pacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti zilishakuwa zimetua chumba cha habari, Mwananchi.
Wakati naendelea kuhangaika na maumivu ya moyo, huku mwili ukiwa umepigwa ganzi mithili ya mtu aliyepigwa na shoti ya umeme, simu yangu iliita kwa mara nyingine.
Safari hii alikuwa Mhariri wa Habari wa Mwananchi, Esther Mvungi. Wakati huo ilikuwa saa 5.00 usiku. Niliipokea simu yake huku neno la kwanza likiwa kama lile la Amina.
“Pole Tumaini, itabidi usafiri kesho kuelekea Iringa kwenye msiba wa Maria na Consolata, jiandae ili asubuhi mapema uianze safari,” aliniambia. Nilitafakari kabla sijakubali kusafiri, nilipata hofu nikijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.
Kwa sababu nilijua fika safari hiyo ni ya kikazi si ya kwenda kuomboleza kama wengine, nilijikuta nikiishiwa nguvu na baadaye nikavuta pumzi na kumwambia ‘Nitaweza’.
Wakati nikiendelea kutafakari, nilipokea simu nyingine ya maelekezo, safari hii ilitoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Habari wa MCL, Frank Sanga akisisitiza weledi katika kuripoti habari ya kifo cha Maria na Consolata.
“Nikutakie safari njema na kazi njema,” aliniambia. Moyo uliuma zaidi, nilivuta taswira ya Maria na Consolata huku nikikumbuka namna ndoto zao za kuwa walimu watakapohitimu masomo ya chuo kikuu zilivyozima ghafla kama mshumaa.
Nilikumbuka ucheshi, tabasamu na upole wao ambao nilikutana nao nilipowaona mara ya kwanza Desemba 2010, katika kijiji cha Ikonda, wilayani Makete baada ya kuhitimu darasa la saba Shule ya Msingi Ikonda.
INATOKA UK 21
Nakumbuka siku nilipowaona walikuwa wameketi nje kwenye mkeka wakicheza na watoto wenzao. Nilipobisha hodi kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi walinipokea kwa tabasamu kama watu wanaonifahamu.
Tangu mwaka 2010 nilifuatilia maisha yao kila hatua. Walipokwenda sekondari, walipokwenda kidato cha tano na hata walipojiunga na chuo kikuu. Niliendelea kuwa nao karibu hata walipoanza kuumwa na baadaye kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Nilikumbuka kwamba Mei 12, mwaka huu nilishinda Tuzo ya Habari za EJAT, kipengele cha elimu baada ya kuandika makala ya Maria na Consolata kuhusu maisha yao mapya Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu). Hii ilikuwa tuzo yangu ya pili kutoka kwa pacha hawa baada ya ile ya kwanza niliyoipata mwaka 2010 ambayo nilishinda katika kundi la watu wenye ulemavu.
Kwa haraka taswira ya kila hatua ya mzunguko wa maisha waliyoyapitia ilinijia kichwani na ghafla machozi yalimwagika. Moyo uliuma, niliingia kulala baada ya kuwa nimepanga vitu vyangu vichache kwa ajili ya safari. Hata hivyo nililala usingizi wa mang’amu ng’amu. Nilisubiri kukuche niianze safari kuelekea Iringa
Saa 10.00 alfajiri niliamka nikajiandaa kisha nikaondoka kuelekea Stendi ya Mabasi Ubungo.
Safari ya Iringa
Safari ya kuelekea Iringa kwa basi ilianza saa 12.00 alfajiri. Simu yangu iliendelea kupokea ujumbe wa pole kutoka kwa watu mbalimbali waliokuwa wakifuatilia makala na habari nilizowahi kuziandika kuhusu pacha hawa.
Ukweli ni kwamba Maria na Consolata waliniita dada. Kila tulipokutana walinikumbatia na nilipowauliza kuhusu afya zao walinijibu ‘Mungu mwema, tunaendelea vizuri’. Ndani ya basi nililokuwa nimepanda, gumzo lilikuwa ni Maria na Consolata.
“Tuma unaelekea Iringa? Nilijua tu miongoni mwa watu watakaokuwa msibani hutakosekana. Pole sana mdogo wangu,” ilikuwa sauti ya Betty , muuzaji mkuu wa Magazeti katika Mji wa Mafinga, mkoani Iringa.
Maneno yake yaliniumiza, mjadala wa pacha hao ulichukua nafasi hadi nawasili Iringa. Saa 9.15 alasiri basi lilisimama, ile nashuka tu kwenye basi, simu iliita na aliyekuwa akipiga alikuwa mhariri wangu Esther.
Aliniuliza; Umefika wapi? Nikamwambia ndio nashuka kituo cha mabasi eneo la Ipogoro. Esther alinipa pole kisha alinielekeza niende moja kwa moja Hospitali ya Rufaa Iringa kuona mazingira yalivyo. Nilimuahidi kwamba nakwenda huko punde kisha tukaagana.
Mji wa Iringa ulikuwa umetulia huku watu wakizungumzia kifo cha pacha hao. Nilielekea Hospitali ya Rufaa kama nilivyoelekezwa.
Japo ilikuwa jioni, mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Museleta Nyakiroto na daktari bingwa wa magonjwa ya ndani aliyekuwa akiwatibu mapacha hao, Dk Faith Kundy walikuwa kazini.
Nilikuwa na wakati mgumu baada ya kuingia katika mazingira ya hospitalini hapo. Wakati naendelea na kazi zipo nyakati nilizidiwa, hivyo nilikuwa natafuta sehemu ya faragha, nalia kwa sauti ya chini ili watu wasinisikie, kisha narejea kuendelea na kazi.
Nilifanya hivyo mara kadhaa maana moyo ulishindwa kuhimili majonzi niliyokuwa nayo. Kwa upande mwingine ilikuwa lazima kazi ifanyike. Kila wakati nilikumbuka sauti ya Esther aliyeniambia ‘nenda utaweza’ na ile ya Sanga aliyenitaka nikafanye kazi.
Dk. Kundy alinisimulia namna kifo cha Maria na Consolata kilivyotokea. “Dk Faith tunakufa” hili ndilo neno la mwisho ambalo Consolata alimweleza daktari huyo baada ya mwenzake, Maria kuwa kwenye hali ya umauti.
Kabla hajaruhusu nimchukue video kwa ajili ya MCL Digital, Dk Kundy alivuta pumzi nzito akasema “Ni vigumu kusimulia, lakini wacha nikueleze.”
“Consolata alikuwa ananisukuma niache kuwahudumia wakati akiwa ameshakata tamaa, japo alikuwa kwenye maumivu makali, sikukubali kumvunja moyo,” anasema.
Anasema Juni 2, 2018, saa 11 jioni alipigiwa simu kuwa hali ya Maria na Consolata imebadilika. “Nilikuja hospitali haraka, nikaenda wodini na nilipofika nilikuta tayari wauguzi na madaktari wengine wanaendelea kutoa huduma ya kwanza hivyo niliungana nao,” anasema.
Dk Kundy anasimulia kuwa aliwapatia dawa zinazotumika kumtibu mtu aliyeishiwa pumzi. “Wakati huo hali ya Maria ilikuwa mbaya, alianza kubadilika mwili, hakuwa na ufahamu. Ilikuwa hata ukimuita haitiki wala kuonyesha kama anasikia,” anasema.
Dk Kundy anasema mfumo wa upumuaji wa Maria ulikuwa chini japo baadaye alirejea hali ya kawaida kabla ya kuzidiwa tena. Saa 1.00 usiku Dk Kundy aliitwa tena, hali ya Maria ilikuwa mbaya zaidi.
“Safari hii nilipoenda, Maria alikuwa kwenye hali mbaya zaidi, sikumbuki hasa ila ilikuwa kama saa mbili usiku Maria alipofariki dunia,” anasema.
Daktari huyo anasema Maria akiwa kwenye umauti, Consolata pia alianza kutetemeka na kulalamika maumivu makali mwili mzima.
“Alikuwa anaona kama hamsikii ‘hamfeel’ mwenzake, akawa ananisukuma huku akiniita kwa jina kuwa ‘Dk Faith sisi tunakufa’ aliniambia akisisitiza niwaache,” alisema na kuongeza: “Maria hakuweza kuongea chochote dakika za mwisho na wakati huo Consolata anasema hivyo Maria alikuwa tayari ameshafariki.”
Simulizi ya Dk Kundy ilinitoa machozi upya. Niliumia na wakati huo nililazimika kumpigia simu Mwandishi wa Mwananchi Iringa, Beldina Majinge ili tuungane kwenye kazi hiyo ngumu.
Beldina aliwasili wakati nikiendelea kuzungumza na daktari huyo ambaye mapacha hao walikuwa wakimtania kiasi cha kumuita wifi!
Dk Kundy anasema kati ya dakika kumi hadi 15 tangu Maria alipofariki, Consolata naye aliaga dunia. Alifumba macho, akalala usingizi ambao hakuamka tena.
“Wakati tunampa Maria huduma ya kwanza na namna alivyokuwa anatapatapa, Consolata alianza kuhisi hali hiyo ndio maana alikuwa akinisukuma na kusema ‘tuache, tuache, tuache, na nilikuwa nawaambia pumua pumua pumua niliwasisitiza hivyo,” anasema.
Anaeleza kuwa tangu wanawapokea kutoka Muhimbili pacha hao hawakuwa kwenye hali nzuri kwa sababu Maria alikuwa akitumia oksijeni kupumua.
Ingekuwaje mmoja angechelewa kufariki?
Kati ya maswali magumu niliyowahi kujiuliza wakati nikiripoti habari za Maria na Consolata wakati wa uhai wao ni kuhusu kifo chao.
Si mimi tu, hata wasomaji wa Mwananchi wengi walijiuliza kifo chao kitakuwaje ikiwa mmoja atafariki na mwingine kubaki hao madaktari watafanya nini? Watamuua au watamuondoa aliyepoteza uhai wake?
Dk Museleta Nyakiroto alitegua kitendawili hiki akisema uamuzi wa mwisho kwa aliye hai ungefanyika kama jambo hilo lingetokea.
“Kwa kuwa haikutokea mmoja wao kuchukua muda mrefu basi hatua ambazo tungechukua mmoja angetumia muda mrefu hatuwezi kuzungumzia kwa sasa, sheria zetu haziruhusu kukatisha uhai wa mtu, lakini majibu tungeyapata ingetokea,”anasema.
Baada ya simulizi ya kifo cha pacha hao, niliwasiliana na bosi wangu Esther, nikakamilisha kazi niliyotumwa. Usiku ule nilitamani kulala msibani kama ilivyo mila na desturi za kiafrika lakini kwa kuwa hakukuwa na nyumba iliyoandaliwa matanga, nilitafuta sehemu nyingine na kwenda kupumzika.
Maria na Consolata waliungana kuanzia chini ya kifua. Waliungana matumbo, nyonga na walikuwa na miguu mitatu huku mmoja ukiwaunganisha wote.
Ilikuwa ukiugusa mguu wao wa tatu upande wa kwanza Maria anaitika na upande wa pili Consolata anaitika.
Dk. Kundy anasema licha ya kuwa katika kuungana kwao kuna viungo vilikuwa pamoja, upo mshipa mmoja mkubwa uliokuwa unapeleka damu kwenye moyo ulikuwa wa pamoja.
“Anaweza kula Consolata na Maria akasema ameshiba na hata suala la maumivu ataanza kulalamika Consolata na baada ya muda mfupi Maria analalamika,” anasema
Siku ya pili Iringa
Jambo la kwanza ilikuwa ni kupokea maelekezo toka kwa mhariri wangu Esther. Siku hiyo nilielekea kwenye ofisi za mkuu wa mkoa wa Iringa walau nikapate taratibu za mazishi.
Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa, ambako mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, alitoa taarifa ya mazishi ya pacha hao.