Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sababu za kutopeleka bweni watoto chini ya miaka 10

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Zipo sababu lukuki za kuwapeleka watoto wetu shule za bweni ikiwa ni pamoja na kufiwa na wazazi wao, majukumu ya kusaka riziki kwa wazazi, elimu bora na zingine kadha wa kadha.

Leo tutajadili athari za shule za bweni kwa watoto wa umri mdogo. Umri chini ya miaka 10 na vipi elimu ya bweni inaweza kuwa ama chachu ya maendeleo ya mtoto au kumdidimiza kimaendeleo.

Mtoto kuanzia miaka miwili hadi minne huwa hana ufahamu wa kutosha kujua baya na jema. Anachopenda yeye ndicho kizuri, asichokipenda si kizuri.

Ni muhimu mzazi kuelewa hili ili kutoa muongozo na uangalizi kwa mtoto kwa upendo pasipo kumhukumu kuwa ana tabia mbaya kwani bado uwezo wa kupambanua baya na jema ni mdogo.

Ingawa bado hajawa na uwezo binafsi kung’amua mwenyewe mema na mabaya, mtoto wa miaka mitano hadi sita anaweza kufuata vyema maelekezo ya mzazi, anaamini kila asemacho mzazi. Bado hana uwezo kujua kwa utashi wake mwenyewe lakini ana uwezo mkubwa kufuata maelekezo ya mzazi/mlezi. Wataalamu wa makuzi wanashauri wazazi wawe makini kutoa maelekezo katika umri huu kwani unachomweleza huwa ni kama mbegu unayoipanda. Misimamo yako katika unayoyaamini kama ibada, vyakula, anavipokea kama kilivyo.

Miaka saba hadi minane, mfumo binafsi wa kung’amua jema na baya wa mtoto unaimarika. Anaanza kujua mifumo ya maisha ya jamii husika na anao uwezo wa kuelewa madhara ya kutenda mabaya.

Pia Soma

Mara nyingi katika umri huu, wataalamu wa makuzi wanaeleza kuwa kutotenda makosa hujengwa na woga wa adhabu zizotolewazo na si kwa sababu nyinginezo. Mfano, mtoto anajua kuwa sababu kubwa ya watu kutoiba ni kukamatwa na polisi na si kwa sababu maadili mema yanakataza kuiba. Unaweza kusikia watoto wa umri huu wakitishana kuwa wakiiba watakamatwa na polisi au mzazi atawaadhibu. Kama mzazi, ni vyema kumuelewesha mtoto kuwa watu hawaibi kwa kuogopa polisi tu bali wizi ni tabia mbaya, si maadili mema.

Jambo jema kuanzia miaka tisa na kuendelea, mtoto anaanza kuelewa maumivu ya kutenda kosa na faraja ya kutenda mema. Kadri alivyolelewa, huumia anapotenda jambo analohisi si jema.

Uelewa wa dhana ya kuwa ‘watendee wengine vile ambavyo ungependa utendewe wewe’ huingia, hivyo ni vyema mzazi/mlezi kuwa mfano mwema kwa mtoto. Usimtendee vitendo vya kionevu mtoto ukidhani kuwa haelewi, anaelewa.

Jitahidi kutenda haki kwani utamuandaa kupenda kutenda haki kwa wengine.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba watoto wanajifunza kwako zaidi kuliko kwa mtu mwingine. Muongoze awe na uelewa wa kung’amua jema na baya pasi kushurutishwa.

Kwa mifano hiyo ya kitaalamu kuhusu uwezo wa mtoto sanjari na umri wake, inakuwa rahisi kwetu kushauri kwamba iwapo sababu za kumpeleka mtoto shule ya bweni kabla ya umri wa walau miaka zaidi ya 10 zinaweza kuepukika, muache asome shule ya kutwa.

Hii ni fursa adhimu kwako kupanda mbegu ya matarajio yako katika maisha ya mwanao kwani unapata kujenga ukaribu siku hata siku.

Ikishindikana kuwa naye katika shule ya kutwa, basi hakikisha unajenga ukaribu na waangalizi/waalimu wake huko anakoishi ili angalau ujue namna bora ya kuhakikisha makuzi kwake.

Columnist: mwananchi.co.tz