Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SIO ZENGWE: Aishi Manula alikosea wapi?

101623 MANULA+PIC Manula

Wed, 8 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

LOCK down haijafika Tanzania, lakini mazingira ya wanamichezo kwa sasa ni sawa na kufungiwa kutoka nyumbani na hivyo matukio mengi ni kama yale wenzetu wa Ulaya wanavyofanya kwa sasa ndani ya nyumba zao au katika maghorofa yao.

Kwakuwa Serikali bado haijakataza wananchi kutoka nyumbani—in fact mkuu mmoja wa mkoa anasema watakaojizuia ndani watakufa njaa—wachezaji wanapata nafasi ya kwenda studio kadhaa za redio na televisheni na kufanya mahojiano.

Wengine kama vile wako katika lock down maana hufanya mahojiano hayo kutoka nyumbani kwao wakitumia simu kujipiga picha za video wakati wakiwa mubashara katika mahojiano. Kwa hiyo unaona raha fulani hivi—si ya kufurahia kuwa tumeshazoea lock down kabla haijafika—bali maendeleo waliyofikia wachezaji wetu katika teknolojia ya mawasiliano.

Wapo wanaojipiga picha za video wakiwa uwanjani kufanya mazoezi na watu wachache, wapo wanaotuma picha wakiwa gym na wengine ufukweni ili mradi raha tu.

Katika fuatiliafuatilia zangu mitandaoni nikamuona Tanzania One, Aishi Manula akizungumzia bao lililoizamisha Simba katika mechi ya watani wa jadi.

Alikuwa mkweli na muwazi kana kwamba anachezea klabu moja ya Premier League ya England ambako mchezaji kuzungumzia ukweli wake kuhusu tukio fulani ni kitu cha kawaida.

Pia Soma

Advertisement
Siku moja baadaye nikasikia ofisa habari wake akionyesha unyumbani; kana kwamba Manula hakutakiwa azungumze kama mchezaji wa Premier League ya England, bali mchezaji wa Simba Sports Club inayoshiriki Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara!

Yaani, angesema “ile ilikuwa kubahatisha tu”, au “unajua nilipiga hesabu vibaya ndio maana yule Morrison akapata bahati ile” au “mpira una matokeo matatu; kushinda, kushindwa na kutoka sare” au “ah sisi tulipata nafasi hatukuzitumia, na wao wamepata moja wakaitumia”.

Pengine ndio maelezo ambayo msemaji wa “taasisi kubwa” kama Simba Sports Club ya Mtaa wa Msimbazi, karibu na Kariakoo ndio alitakiwa aeleze na si ufundi wa mchezaji aliyepiga lile shuti lililozaa bao pekee katika mechi baina ya Simba na Yanga.

Mpaka leo bado nimeshikwa na butwaa yule msemaji alitaka kipa aseme nini wakati mpira ulipita juu ya ukuta wa mabeki wa Simba waliopangwa vizuri; warefu kuanzia upande wa kushoto na huku akijikita zaidi kwenda upande wa kulia.

Lakini Morrison akaupeleka kulekule alikopanga warefu—ingawa wa kwanza alikuwa mfupi—na kuupitisha juu yao mpira ambao mbele ulikunja kona kwa staili ya nose-dive kujaa wavuni.

Ni bao la kawaida ambalo linahitaji mazoezi ya nguvu ya timu nzima kuchambua na kuweka mikakati ili siku nyingine isitokee makosa kama hayo, labda awe mjuzi mwingine mwenye mbinu tofauti.

Haya ni matukio ya kawaida na ni jambo jema wachezaji wanajitokeza na kuwa wawazi kuyazungumzia kwa mujibu wa maoni yao, yaani kwa mujibu wa maoni ya Aishi Manula ambayo hawezi kuwa nayo Haji Manara, Senzo, Mohamed Dewji au Manula hawezi kumtuma Manara akayazungumze kwa niaba yake.

Tuache kujaribu kutawala hata maoni binafsi.

Ningeelewa kama Manula angekuwa amezungumzia masuala ya kisera ya Simba, angekuwa amekwenda kinyume na taratibu za klabu hiyo.

Lakini kutoa maoni yake binafsi kuhusu mechi aliyocheza na hata ambayo hakucheza, haiwezi kuwa sera ya Simba na naamini kuwa si sera ya Simba.

Simba imepiga hatua kubwa katika siku za karibuni na hivyo kurejea katika mawazo kama hayo ya kumzuia mchezaji kutoa maoni yake, ni kurudi nyuma sana kimaendeleo.

Columnist: mwananchi.co.tz