Kuna minyukano kila mahala. Juu ya muswada wa sheria mpya kwa vyama vya siasa. Ambao unatakiwa kupelekwa Bungeni hivi karibuni upitishwe rasmi kuwa sheria. Vyama pinzani vimekuja juu vikidai kuwa muswada huu ukipita ni kiama kwao.
Kabla ya kelele zao. Nilifahamu ujio wa sheria hii mpya. Mapema wanoko walianza kunong’ona. Nilikaa kimya, nikisubiri baadhi ya watu na taasisi zitoe neno. Ili nipate sehemu ya kuanzia kama kupongeza au kuponda. Sipendi kukurupuka kukosoa mambo palipo na wazee.
Watu wa kwanza ni taasisi ya Mwalimu Nyerere. Mzee Joseph Butiku na wenzake kama Issa Shivji. Hawa wazee ni mara chache hukaa kimya pale jambo lolote linapoenda tofauti. Ukiona wako kimya ujue ni jambo jema. Kumbuka Rasimu ya Katiba Mpya ya Warioba walivyoitolea macho.
Mzee Butiku kimya. Salim Ahmed Salim kimya. Issa Shivji kimya. Hawa wazee na wenzao kama wako kimya ina maana mambo yako sawa. Kwa maana hiyo muswada huu ni sahihi Kwa ustawi wa jamii ya kidemokrasia. Sasa mimi ni nani nipinge jambo ambalo wazee hawa wanaona yafaa lifanyike?
Haiingii akilini kupinga jambo la sheria ambalo Jaji Warioba, na Majaji kibao wastaafu wako kimya. Unataka kuniambia kama huu muswada ni tatizo kwa ukuaji wa demokrasia wastaafu hawa wa sheria wangekaa kimya? Kama wako kimya ina maana kila kitu safi. Mimi ni nani mpaka nipinge?
Mambo yanakuzwa tu bila sababu. Pengine wanatafuta kiki. Binafsi nimepitia baadhi ya vifungu. Asilimia 90 ni kwamba vyama vya siasa ni kama vitaongozwa na Msajili wa Vyama. Wenyeviti na Makatibu watakuwa kama sanamu kwenye chama. Msajili ndo kila kitu.
Sasa tatizo liko wapi kama majukumu ya kuongoza vyama kapewa Msajili? Viongozi wamepunguziwa majukumu. Mambo ya kulumbana na vyombo vya dola yataisha. Kama Mwenyekiti wa chama yupo Segerea haina shida Msajili yupo na ndiye kila kitu.
Sheria hii pia inakataza mambo ya kususia chaguzi. Lazima mtumie pesa za walipa kodi hata kama hamna mgombea. Mkisusia uchaguzi kama mlivyozoea chama kinafutiliwa mbali. Kifupi hii sheria haitaki wanasiasa visirani. Msajili akifuta ndo basi hutakiwi kupinga mahakamani.
Binafsi nataka sheria hii ipitishwe haraka ili kukuza demokrasia nchini. Hao wanaopiga kelele siwezi kuwasikiliza kama marais wastaafu wako kimya. Kama huu muswada ni wa sheria kandamizi wastaafu wetu wa kisiasa na kisheria wasingekaa kimyaa.