Inakera sana. Kuna mambo yanajirudia kila wakati mpaka yanachosha. Unapokaribia uchaguzi ndani ya Chadema kuna maneno kuhusu Mbowe lazima uyasikie – Mbowe anajilipa ruzuku yote. Kateka mali zote za chama. Mbowe anaendesha chama kama ofisi binafsi. Maneno haya yanajirudia kila msimu wa uchaguzi wa chama hicho.
Tuliyasikia wakati wa Chacha Wangwe. Wakati wa Zitto Kabwe. Sasa Kigogo wa ‘twita’ anayarudia kwa namna ileile. Kwa mwenye akili timamu hii inachosha.
Kama hizi ndiyo propaganda basi hizi ni za kipumbavu. Kichekesho zaidi ni wanaozitumia kushindwa kuelewa kuwa hazina mashiko. Uchaguzi wao ukiisha na haya maneno yanaisha.
Tuwekane sawa kwenye hili. Chama kinachopigania ukombozi au kutaka kushika dola, kikipata kiongozi imara hakimbadilishi ovyoovyo. Hii ni ‘prinsipo’. Yasser Arafat kafa akiwa kiongozi wa PLO kwa miaka mingi kule Palestina. Dunia nzima, kiongozi wa namna hii huondolewa kwa kushindwa kustawisha chama na si vinginevyo. Huyu ndiye Mbowe.
Ukiwa na kiongozi asiye na msimamo mtaishia kuwa na vyama visivyosikika. Akili za Mbowe, msimamo wake, uchumi wake. Ndiyo yaliyopelekea akute chama kina wabunge watano na sasa wako sabini. Unamuondoaje? Labda kama huna nia ya kushika dola. Propaganda za kula ruzuku lazima zife kibudu.
Kuna watu wakisikia shamba la Mbowe limeharibiwa na DC wanawaza matembele, nyanya chungu, sukuma wiki, kabeji na matuta ya viazi – wanalifananisha na mashamba ya bibi na babu zao huko Mpwapwa au Malinyi kama siyo Matombo. Tunatakiwa kumshangaa Mbowe kuacha utajiri chekwa wa familia yake na kuja kuhangaika na siasa huku mitaani na kina Sugu.
Pia Soma
- Mwanamke Uganda ahukumiwa kifungo kwa kumlisha mtoto hedhi
- 292 waumwa na mbwa wilaya ya Ulanga, Malinyi 2019
- Watu 500 huru waokolewa katika jumba la mateso Nigeria