Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

SAUTI YA MNYONGE: Wamlilia JPM mauaji ya binti yao

68410 PIC+MDADA

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rombo. Familia ya binti aliyeuawa na baadaye mwili wake kutupwa pembeni ya barabara imemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati suala hilo.

Binti huyo, Emma Lang’oye, 22, mkazi wa kijiji cha Samanga wilayani Rombo aliuawa na mwanamke mmoja ambaye alikamatwa na baadaye kuachiwa huru.

Taarifa iliyotolewa na familia hiyo inadai kuwa mtu anayetuhumiwa kufanya mauaji hayo alikamatwa Juni 18, 2019 lakini aliachiliwa huru na Jeshi la Polisi baada ya kukaa kituo cha Usseri kwa wiki mbili.

Binti huyo aliyekuwa mkulima, aliuawa Juni 17 kwa kuchomwa visu sehemu mbalimbali na mwenzake katika tukio ambalo lilizua taharuki na pia lilikemewa na viongozi wa dini. Alizikwa nyumbani kwao Juni 25.

Sixmundi Lang’oye, ambaye ni baba wa binti huyo, aliliambia Mwananchi jana kuwa hawaoni Jeshi la Polisi likitenda haki kwa kuwa familia yao ni maskini, hivyo wanamuomba Magufuli awasaidie ili haki itendeke.

Hata hivyo, kamanda wa polisi mkoa, Hamis Issah alisema kama familia imeona kuna tatizo katika kituo hicho cha polisi, wafike katika kituo kikuu cha Moshi awasikilize.

Pia Soma

“Nimetoa agizo familia ije,” alisema Kamanda Issah.

“Kama kule Rombo wanaogopa, wasiende huko waje kwangu ili nione hii kesi tunaipanga vipi. Mtoto huyu (marehemu) aliwahi kugombana na huyo aliyekamatwa na waligombana siku nyingi. Kama wana ushahidi, niko hapa nitahakikisha hili jambo linaenda vizuri.”

Mzazi wa binti huyo alisema japo familia yao haina uwezo wa kifedha wa kupeleka watu wanaotakiwa kutoa maelezo mjini, watajitahidi kufanya hivyo.

Akilalamikia jinsi suala hilo linavyoshughulikiwa, baba huyo alisema wamekuwa wakiishi kwa hofu tangu mtuhumiwa alipoachiwa huru kwa kuwa wanapokea vitisho kutoka familia yake ambayo inadai haiwezi kufanywa chochote.

“Tunamwomba Rais wetu mpendwa, Rais wa wanyonge, atusaidie haki itendeke,” alisema.

“Sisi ni wanyonge hatuna chochote. Marehemu ameniachia watoto wawili wadogo na unyonge wetu huu ndio umesababisha sisi tunyimwe haki yetu. Haiwezekani mtuhumiwa wa mauaji anakamatwa baada ya wiki mbili anachiwa.

“Mtuhumiwa wa mauaji anafahamika na maelezo yote tuliyatoa kituo cha polisi Usseri, lakini cha ajabu tunashangaa mtuhumiwa anaachiwa. Hii ni haki kweli? Rais wetu tunaomba utusaidie sisi wananchi wako ambao tunanyimwa haki zetu kwa sababu ya unyonge wetu.”

Alisema waliwafuata polisi wa Usseri kutaka kujua sababu za kumuachia huru mtuhumiwa na kutofikishwa mahakamani, ndipo mmoja wa askari akawajibu kuwa maelezo waliyotoa hayawezi kumfikisha mahakamani.

“Akatueleza kuwa wanaangalia baada ya wiki mbili wakithibitisha mtuhumiwa ana kosa watamkamata tena,” alidai mzazi huyo.

Naye babu wa marehemu, Aloyce Ndekise alisema jambo hilo sio la kufumbia macho kwa kuwa matukio kama hayo yameendelea kutikisa wilayani hapo kutokana na watuhumiwa wa mauaji kutofikishwa mahakamani na baadaye kuwatambia wananchi kwamba wao hawawezi kufanywa chochote.

“Kwanini mtuhumiwa kaachiliwa huru na ushahidi upo na tumeshautoa polisi? Tunaiomba Serikali ihakikishe mtuhumiwa huyu anapelekwa mahakamani kwa sababu ushahidi tunao,” alisema Ndekise.

“Suala la kumwachia huru mtuhumiwa ni jukumu la mahakama. Ndiyo inayotoa uamuzi kama mtuhumiwa ana kesi ya kujibu au hana.

“Tukio lilipotokea Juni 17, usiku wa saa 2:00 kwanini kesho yake asubuhi walienda kumchukua mtuhumiwa huyo? Kwanini wasimchukue mtu mwingine wakamchukua yeye? Nani aliwapa hizo taarifa? Polisi wanajua kabisa muuaji ni kitu gani kinachowafanya wasitende haki? Na mtuhumiwa kutofikishwa mahakamani, ni siri gani iliyofichika hapo?”

Naye mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Fransisca Francis alisema siku ya tukio walisikia binti huyo akiita ndugu zake kwa sauti huku akimtaja mtuhumiwa huyo kama mzazi wa toto anayejulikana kuwa wake.

“Nikiwa nyumbani nilisikia sauti ya binti huyu ikiita mama fulani unataka kunifanyia nini? Nilifika eneo la tukio nikakuta mtoto wake wa miezi kumi amewekwa chini huku mama yake akiwa ameshachomwa visu,” alisema.

“Kwa kweli kifo cha huyu dada kimetuumiza. Ni binti mdogo ambaye hana maneno na mtu. Kinachotuumiza zaidi ni kwamba siku anauawa alikuwa na mtoto wake mdogo.”

Columnist: mwananchi.co.tz