Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ruge ameniambia mengi katikati ya usingizi wa umauti

44694 Pic+usingizi Ruge ameniambia mengi katikati ya usingizi wa umauti

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

RUGE Mutahaba ‘Scofield’. Yes, akili nyingi na bingwa wa ufumbuzi katika mambo magumu mithili ya Michael Scofield wa kwenye series ya Prison Break. Scofield ni muvi, Ruge ni maisha halisi. Ruge ni Scofield katika maisha halisia.

Nyote semeni hamna mlango wa kupita, lakini Ruge angeuona na kuwaonesha namna ya kupita. Alipenda kuishi ndani ya watu bila kujionesha na kutengeneza athari kubwa kwenye jamii. Mwisho kabisa, maisha aliyoishi ndiyo yaliyomzika.

Ruge alifariki dunia Februari 26, mwaka huu nchini Afrika Kusini alikokuwa anatibiwa. Juzi (Machi Mosi), mwili wake ulipokelewa Dar.

Msafara wa kuutoa mwili wake Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mpaka ofisi za Clouds Media Group (CMG) kisha Hospitali ya Lugalo, umeweka rekodi ya aina yake.

Naam, Ruge ni Kaka wa Taifa. Dar es Salaam ilijaa watu barabarani kama ilivyokuwa mwaka 1999 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipofariki duniani. Kishindo cha msiba wa Ruge kimepita cha supastaa Steven Kanumba aliyefariki dunia mwaka 2012.

Kwa rekodi hiyo, Ruge ananiambia bila kufunua kinywa, akiwa kwenye usingizi wa mauti kwamba mtu anayeishi ndani ya mioyo ya watu ni mkubwa kuliko yule mwenye kujionesha na kujipa ufahari kwa watu.

Ruge ananiambia kuwa umaarufu siyo kujiweka mbele kila wakati, unaweza kuwa daraja la wengine na pasipo kutarajia ukavuna kwenye jamii matunda yenye thamani.

Ni kama Ruge ananiuliza: “Luqman, nani alitegemea ningezikwa kwa heshima hii?” Jibu langu ni “Hakuna Mkurugenzi”. Ni kweli, wengi walimchukulia poa Ruge. Waliompa uzito, hawakufikiri kwamba alishasafiri ndani mno kwenye mioyo ya Watanzania.

Watanzania hawakupata nafasi ya kusema kabla ni kiasi gani walimpenda Ruge. Hakuwa na mikutano ya hadhara kusema wangejaa kwa wingi anapohutubia. Hakuwa mwanamuziki kusema wangenunua kwa wingi santuri zake. Si mcheza sinema, kwamba mauzo ya filamu zake yangedhihirisha mtaji mkubwa wa watu alionao.

Ruge ananiambia kuwa huhitaji vichwa vya habari vingi kwenye vyombo vya habari ili uwe maarufu. Si mpaka uingie bungeni au uwe unakula kiyoyozi kwenye gari na ofisi ya waziri. La! Mtindo bora maisha wenye kuigusa jamii, unaweza kukufanya uwe lulu.

Tumewapoteza wanasiasa wangapi wakubwa lakini misiba yao haijagusa nyoyo kama Ruge? Wasanii wangapi? Ni kama Ruge ananiambia kuwa hata yeye mwenyewe hakujua kama anapendwa kwa kiasi kilichodhihirika baada ya umauti kumfika.

Ruge ananiambia kwamba huhitaji kuwa kiongozi wa kiroho ili ushike roho za watu. Viongozi wangapi wa kidini tumeshawazika lakini hawakutikisa kama Ruge inavyoifanya nchi yetu iwe na hekaheka?

Wakati nashangazwa na mtikisiko wa nchi kwa kifo cha Ruge, naona dhahiri Ruge anajaribu kuniambia maana halisi ya uongozi, kwamba si mpaka ugombee na uchaguliwe na wananchi au uteuliwe na Rais nafasi fulani serikalini. Ruge ananiambia kuwa uongozi ni vile unajichukulia.

Hakika! Ruge alijitafsiri kuwa ni kiongozi. Si uongozi wa Serikali, siasa au dini. Ruge aliamua kuwa kiongozi wa mtaa. Mitaa ikamuona ni kiongozi wao na ikamuelewa. Mitaa haikupaza sauti kumtangaza Ruge ni Kaka wa Taifa, bali walimhifadhi moyoni. Alipokufa, wameshindwa kuficha.

Ruge aliamua kuwa daraja la wengi. Alichagua kuwa mnyoosha njia ili wengine wapite. Harakati za Clouds FM kufungulia watu dunia na kampeni nyingine, pamoja na mradi wa Fursa wenye maudhui ya kuwafanya watu kuchangamkia fursa mbele yao. Hayo kwa uchache yamemfanya awe kiongozi ndani ya mioyo ya wengi.

RUGE ANAONYA CHUKI

Niliposhika jeneza lenye mwili wa Ruge, nikahisi Ruge ananiuliza: “Luqman, umejifunza nini kuhusu chuki na matamko ya ubaya dhidi ya watu wengine?” Swali gumu eeeh, lakini ni rahisi pia.

Nimejifunza kuwa usipende kutangaza kwa umma kuhusu chuki zako dhidi ya mtu mwingine. Unaweza kudhani unagombana na unaemchukia, kumbe unagombana na jamii kubwa.

Jiulize, maelfu waliojaa mitaa ya Dar es Salaam kwa ajili ya Ruge walijisikia vipi pale mtu alipotangaza hadharani kuwa anamchukia Ruge wanayempenda? Kumbe unaweza kusema humpendi Ruge kisha ukavuna chuki ya mamilioni ya watu wanaompenda unayemchukia.

Kuna wakati badala ya kutimiza wajibu wa kusherehekea maisha ya Ruge, nikajikuta nautafsiri ki-Bongo Fleva umati uliokusanyika barabarani kumpokea Ruge kutoka Afrika Kusini. Kwamba msanii akipata mapokezi makubwa huwa tunaambiwa watu wamelipwa kwenda kujaza shangwe barabarani.

Ruge amelala akiwa hana uhai, hizo pesa kawalipa akina nani? Yes, watu wamelipwa pesa nyingi ndani ya nyoyo zao. Ruge aliwapa pesa nyingi Watanzania pasipo yeye mwenyewe kujua. Ni pesa za moyoni, siyo pesa za mfukoni wala benki. Nao hawajamwangusha.

Tatizo Ruge ananiambia yeye na kuniuliza pasipo kuruhusu nami nimuulize. Nikimuuliza hajibu. Ananiuliza: “Uliwahi kunisikia wakati wowote nikitangaza kuwa mtu fulani ni adui yangu?” Hili ni kweli, sikupata kumsikia Ruge akijiweka wazi kuwa na vita binafsi na mtu fulani. Hata hivyo, ni wengi walijitangaza kuwa adui wa Ruge.

Ruge aliongoza redio yenye kuaminika kusikilizwa na watu wengi kuliko nyingine zote nchini. Angeweza kutumia redio yake au televisheni yake kupambana na watu kila siku.

Ruge hakuwa hivyo. Kuna ambao walitumia magazeti yao kumshambulia binafsi mara kwa mara. Ruge akachagua kukaa kimya. Hakupenda kujibizana, ila alijibu alipoona kuna ulazima wa kufanya hivyo.

Zaidi Ruge ananiuliza: “Maisha ya binadamu ni mafupi hivi na hayana uhakika, yanini kujengeana chuki za kuendelea?”

Swali hilo linanikumbusha kuwa kuna watu wanatamani kufika msibani na kumzika Ruge lakini nafsi zinawasuta. Wataanzaje? Wataelewekaje?

Hawakuona ulazima wa kushusha silaha chini kipindi ikitangazwa kuwa anaumwa. Walipenda chuki iendelee. Wapo watatamani kumuomba msamaha lakini nafasi hiyo wataipata wapi? Ruge ameshalala usingizi wa dawamu. Ukimsemesha hakujibu. Ni mimi tu napata fursa hii ya kuzungumza naye.

Kimsingi Ruge alitoa nafasi nzuri kwa watu kumaliza tofauti naye. Kumtakia heri tu kipindi anaumwa ilikuwa jambo jema mno. Bado kukawa na kipindi kifupi cha mwishoni cha kuhamasishana kuchangia matibabu yake kwa sababu gharama zilikuwa juu mno. Wastani wa Sh5-6 milioni kwa siku.

Kilikuwa kipindi cha watu wenye tofauti naye kujikosha. Hata tu kuposti mitandaoni kuhusu kuhamasisha watu kumchangia Ruge. Je, nani anaweza kujiita shujaa leo kwa sababu Ruge amefariki dunia akiwa na kinyongo naye? Hili pia Ruge ananiambia kuwa ni funzo kuhusu chuki. Kibinadamu tutofautiane, ila tusichukiane. Chuki ni mbaya mno. Unamchukiaje binadamu na hujui kama kesho utaamka?

Rest In Paradise Kaka wa Taifa.



Columnist: mwananchi.co.tz