Nchi ya neema ni ya neema tu. Ina kila kitu unachokijua duniani. Tuna madini kila kona kila chimbo. Kuanzia Kusini, Kaskazini, Magharibi na Mashariki. Hakuna mkoa usio na madini labda majini. Tuna utajiri wa hofu na umilionea wa woga na pia usisahau sisi ni ‘madon’ wa kusahau. Vitu vyote hivi tumepewa na Mungu Baba. Hii husaidia pale ambapo panahitajika kufanya maandamano tupate hofu. Jambo la kukemea sisi hupata woga na kumuachia Mungu aamue. Na zaidi matatizo tuliyoletewa hapo nyuma tuna upedeshee wa kusahau.
Utajiri wa kusahau unaotupa neema ya kuchagua mbunge yuleyule. Hata kama bungeni anasinzia kama pono na kuunga mkono hoja za kilofalofa. Akija jimboni msimu wa kampeni kuomba kura tunasahau upuuzi wake wote tunampa kura tena kwa wingi. Hii ndo faida ya ‘udon’ wa kusahau yaliyopita. Bila hivyo hakuna mbunge wa kukaa misimu miwili nchi hii.
Bongo tunapendwa sana na Mungu Baba Mwenyezi. Achana na hayo. Kuna vitu aliendelea kutuletea kwa njia za roho mtakatifu. Yaani alitubariki kwa utajiri wa vitu vilivyoshuka kimiujiza. Unakumbuka vichwa vya treni? Ghafla tu viliingia bandarini na kila mtu akijiuliza vya nani? Baada ya kukosekana mwagizaji. Na uzuri wa roho mtakatifu vile vichwa aliviandika kabisa jina la shirika letu la reli.
Sisi tumebarikiwa sana. Halafu roho mtakatifu huyo alihamishia makazi yake kwenye mwili wa raia namba moja wetu. Kila alipotembelea bandarini alikutana na magendo yanayotoroshwa. Mara ya mwisho alikuta magari ya wagonjwa yamepaki kibao kama kumbikumbi na hayana mwenyewe. Mungu anatuhusudu sana. Unakumbuka kontena za makinikia? Yeye alijiendea tu kukagua uendeshaji wa bandari mara akakutana na lundo la kontena kibao za makinikia. Akayazuia kindava na kuibua balaa kubwa zaidi. Ni dhahiri pale tulioneshwa kupitia raia namba moja kuwa kuna ‘maibilisi’ kibao waliopo kwa njia ya uwekezaji wanaotorosha utajiri wetu Huyo ni roho mtakatifu jamani alitenda miujiza.
Ila mbona siku hizi miujiza hii imetoweka kabisa? Au roho mtakatifu ametususa? Maana hata kupona kwa Tundu Lissu ukijiuliza kwa umakini kabisa utagundua kuwa mbali na madaktari pia mkono wa roho mtakatifu ulihusika kaa asilimia 90. Kuna haja ya kurudi kwenye maombi ili tuendelee kuletewa vitu kimiujiza. Kama tulikosea atusamehe, na safari hii roho mtakatifu kwa mapenzi yako ukipenda tuletee hata bunge jipya kimiujiza.