Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Reginald Mengi: Tasnia ya habari itakukumbuka

59037 Pic+mengi

Wed, 22 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni matarajio yangu kuwa siku historia ya vyombo vya habari katika Tanzania katika robo karne itakayopita itakapoandikwa, basi waandishi wa historia hiyo watampa nafasi pekee na maalumu, Reginald Abraham Mengi (RAM), mwenyekiti wa kampuni za IPP, aliyeaga dunia usiku wa kuamkia Alhamisi ya Mei 2, akiwa Dubai, Mashariki ya Kati.

Nianze na jambo ambalo pengine si muhimu. Lakini ni vizuri likaeleweka kwa sababu litasaidia kuweka msingi wa ninayotaka kuyasema kuhusu marehemu Mengi.

Nia yangu ni kukwepa mtego wa kuongozwa na unafiki, kama ilivyo desturi ya tulio wengi katika nchi yetu, wakati mtu anapofariki.

Kukutana kwa mara ya kwanza

Uhusiano wangu na mzee Mengi ulitawaliwa na vipindi vifupi vya urafiki, lakini zaidi na vipindi virefu vya mivutano, na mpaka anaaga dunia, nilikuwa sijawasiliana naye kwa kipindi kirefu, kwa sababu mara ya mwisho uhusiano wetu ulikuwa mbaya.

Nilikutana na mzee Mengi ana kwa ana, kwa mara ya kwanza, mwaka 1991 katika hafla moja iliyofanyika Hoteli ya Forodhani (sasa Makahama ya Rufani) mjini Dar es Salaam. Nilikuwa nimejerea nchini kutoka masomoni Uingereza. Katikati ya tafrija hiyo alinijia mwenyewe na akajitambulisha, ingawa dhahiri nilikuwa namfahamu. Wakati huo, alikuwa tayari ameanzisha IPP. Lakini kubwa zaidi wakati huo, alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya magazeti ya Serikali ya Tanzania, yaani Standard Newspapers (TSN).

Baada ya kujitambulisha, alinieleza kuwa alikuwa amesikia habari zangu kutoka kwa baadhi ya Watanzania niliokuwa nao Uingereza. Hili halikunishangaza, kwa sababu wanafunzi wengi walinijua vizuri kwa sababu nilikuwa mwenyekiti wao wa Chama cha Wanafunzi wa Tanzania Uingereza na Ireland. Pia alinialika nipate muda nimtembelee ofisini kwake katika jengo la IPS, katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Ofisini kwake, aliniambia mambo kadhaa. Kwanza, kuwa alikuwa na nia ya kuanzisha magazeti. Pili, aliniambia kuwa mimi nilikuwa mtu wa kwanza kuambiwa habari hizo, akiomba mazungumzo yetu yabakie siri kwa muda. Tatu, akaniomba niwe mhariri wa kwanza wa magazeti hayo. Nne, akaniomba nimwandalie, kwa mhutasari kabisa, namna ya kufanikisha azma yake hiyo. Tano na mwisho, akaniomba nianze “kutazamatazama” watu ambao wangefaa kushiriki katika “mradi” huo kama yeye alivyokuwa anauita.

Kazi hiyo niliifanya vizuri nadhani, na vilifuatia vikao vingine vingi tu baina ya mzee Mengi, tukimwita “Mwenyekiti” na baadhi ya watu ambao niliwapendekeza kwake na yeye akawakubali. Sitawataja kwa sababu hapa si mahala pake na hasa kwa sababu wote walikuwa ni waajiriwa ama wa Serikali (Maelezo) au kwenye magazeti ya wakati huo ya CCM na Serikali. Wale ambao Mwenyezi Mungu amewajalia kubakia hai, wanajijua.

La msingi ni kwamba, hatimaye, sikufanikiwa kuwa mhariri mwanzilishi wa magazeti ya mzee Mengi, kama tulivyokuwa tumepanga. Sababu za hili nazo tuziache kwa sasa. Zitazungumzwa siku nyingine, mahali pengine na wakati mwafaka. Kubwa la kusema hapa ni kwamba badala ya kuwa mhariri mwanzilishi wa magazeti ya mzee Mengi, nikawa mmoja wa waanzilishi wa gazeti la Dimba, gazeti mama la michezo Tanzania na chimbuko la kile kilichokuja kujulikana baadaye kama Habari Corporation na magazeti yake.

Uamuzi wangu wa kutojiunga na himaya ya mzee Mengi, pamoja na imani kubwa aliyokuwa amenionyesha, haikumfurahisha. Alikasirika. Hata hivyo, uhusiano wetu ulikuja kurudia hali yake nzuri baadaye wakati nikiwa mwenyekiti wa tawi la Tanzania la Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan), na baadaye kwenye Kanda ya Kusini mwa Afrika.

Uhusiano huo ulikua zaidi wakati nilipokuwa mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), chama ambacho mzee Mengi alikiongoza tokea kuanzishwa kwake hadi umauti ulipomfika. Baadaye, wakati wa msiba wa mwanangu Brian, mzee Mengi alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kunifariji kwa kila hali na alishiriki kikamilifu katika mazishi.

Uhusiano wetu kuharibika

Uhusiano wangu na mzee Mengi uliharibika tena mwaka 1996, wakati gazeti la Mtanzania ambalo nilikuwa mhariri mtendaji wake, lilipoandika habari kuwa alikuwa mdaiwa mkuu na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Huo ulikuwa wakati wa misukosuko mikubwa ya kubinafsishwa kwa benki hiyo. Wala hakuficha hasira zake kuhusu kuandikwa kwa habari hiyo. Alitufungulia kesi ya madai, akitaka kulipwa mabilioni ya fedha, kwa kuvunjiwa heshima na hadhi.

Hatukuishia hapo. Uhusiano wangu na mzee Mengi ulivurugika mno wakati nilipotumikia katika nafasi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu. Kwa sababu ambazo, binafsi sikupata kuzijua vizuri ingawa naamini zilikuwa za uongo, uhusiano wangu na mzee Mengi ulifikia kiasi cha yeye kukataa kunipa mkono wakati wa hafla moja ya kitaifa pale Ikulu.

Tena kwa maneno ya kuambiwa tu, alifikia mahali pa kunipigia simu siku moja, kunishutumu kwa kuwa kizabizabina, ambaye nilikuwa nasambaza maneno ya kumsema kwa watu. Lakini baya zaidi, akanishutumu kuwa nilikuwa kwenye mpango wa kutaka kumuua. Kwa nini? Sikupata kujua. Sijui kwa sababu siamini hata kama binafsi nina hata uwezo wa kuua inzi, achilia mbali mtu maarufu katika jamii kama mzee Mengi.

Mpaka anaaga dunia hatujapata nafasi ya kuzungumza ana kwa ana, kuhusu shutuma hizo dhidi yangu, ukiondoa hatua yangu ya kujiunga naye katika ibada ya kumuaga mke wake wa zamani, marehemu Mercy Mengi.

Pamoja na hayo

Lakini hata kama uhusiano wetu ulikuwa wa kupanda na kushuka milima kwa miaka yote 28 tuliyojuana, bado kwangu mimi, na naamini kwa mamilioni ya Watanzania na hasa Waafrika wa nchi hii, mzee Reginald Abraham Mengi alikuwa mtu muhimu sana. Ameonyesha njia na kufungua milango kwa mamilioni ya watu, hasa katika eneo la uthubutu wa Waafrika kufanya biashara.

Aidha, uhusiano huo haukupata kubadilisha maoni na msimamo wangu kuhusu mchango wake mkubwa, tena mkubwa mno, pengine kuliko wa Mtanzania mwingine yeyote, katika maendeleo ya tasnia ya habari katika nchi yetu, kwa hakika katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki.

Kwa maoni yangu, siamini kama kuna mtu mwingine amechangia zaidi tasnia hii kama alivyofanya mzee Mengi. Si kama mwandishi wa habari-- kwa sababu hakuwa mwandishi wa habari-- bali kama mfanyabiashara na mchumi halisi wa vyombo vya habari. Alikuwa na uthutubu wa ajabu sana, dhamira na maono ya kuhusudiwa katika eneo hili.

Hakuiona tasnia ya habari kama eneo la kuchuma na kupoteza fedha zake, kama walivyo wafanyabiashara wengine. Aliiona tasnia kama dimba mwafaka la kuwahabarisha, kuwaelimisha na kuwaburudisha Watanzania  wana-Afrika Mashariki.

Kwetu sisi wakati huo tukiwa Habari Corporation, mzee Mengi kupitia magazeti yake ya IPP, alikuwa mshindani mkubwa. Mshindani, kwa maana ya magazeti tu, siyo vinginevyo, kwa kutilia maanani kuwa sisi hatukuwa na vyombo vingine vya habari na yeye alikuwa na rasilimali nyingi zaidi kifedha na kibiashara. Lakini alikuwa ni mshindani hodari ambaye mchango wake ni lazima tuuenzi. Sura ya tasnia ya habari ya Tanzania ya sasa ni matokeo ya mchango wake mkubwa. Tasnia isingekuwa kama ilivyo sasa bila mchango mkubwa wa mzee Mengi. Huo ndio ukweli usiopingika - tupende, tusipende.

Nataka kusema jambo ambalo linaweza kuwa lenye utata. Lakini nitalisema, wacha lizae utata. Kama iko siku historia ya vyombo vya habari katika Tanzania, ikiandikwa kwa haki na wanahistoria wanaojali ukweli, itaonyesha kuwa katika miaka 30 iliyopita ya kuchipuka upya kwa vyombo vya habari binafsi na kuchanua kwa uhuru wa habari Tanzania, makundi matatu yalitoa mchango wa aina pekee katika hali hiyo na katika kukua kwa tasnia ya habari.

Kundi la kwanza ni la IPP likisukumwa na dhamira na utashi pamoja na rasilimali kubwa za Mzee Mengi, Habari Corporation ikisukubwa na uthubutu na kiwango cha juu kabisa cha weledi na taaluma, na Business Times ikiongozwa na ubunifu mkubwa wa Marehemu Richard Nyaulawa na Rashid Mbughuni ambao kwa pamoja walianzisha gazeti la kwanza la kila siku la Kiswahili la Majira katika kipindi cha baada ya kurudishwa kwa uhuru wa kujieleza na vyama vingi katika Tanzania.

Yapo makundi mengine mawili muhimu yaliyochangia na yanayoendelea kuchangia, kwa kiasi kikubwa, maendeleo ya tasnia katika kipindi hicho. Kuna Kampuni ya Mwananchi Communications na Sahara Communications ya Mwanza. Haya yamechangia kwa namna ya pekee pia. Lakini historia yao ni tofauti kidogo na makundi yale matatu yaliyotajwa hapo juu.

Mzee Mengi alikuwa Mtanzania wa kwanza kuwawezesha watu wengi kupata matangazo mbadala ya redio wakati alipoanzisha Radio One na ikaanza kutoa matangazo ya ushindani, kwa mara ya kwanza na redio za Serikali za Radio Tanzania na Sauti ya Tanzania, Zanzibar ambazo baadaye zilikuja kubadili majina na kuitwa Tanzania Broadcasting Corporation (TBC) na Zanzibar Broadcasting Corporation (ZBC). Redio nyingine binafsi nchini zilifuata nyayo tu za mzee Mengi na Radio One.

Sikatai, kuwa kabla ya Radio One, ilikuwepo redio ndogo binafsi ya Sauti ya Injili, ikitangaza kutoka Moshi, lakini hii ilikuwa redio iliyowafikia watu wachache kwa sababu ya maudhui yake ya dini na ya madhehebu ya Kilutheri, na hata mipaka ya mapokeo yake.

Lakini kwa maana ya broadcasting, yaani kutupa wavu mpana zaidi wa matangazo yanayorushwa na mawimbi kufikia watu wengi kwa wakati mmoja bila mtu yeyote kupoteza ubora na maudhi ya matangazo yenyewe, mbali ya Serikali, mzee Mengi alikuwa kinara katika nchi hii. Wengine wote wanaotamba leo walifuata nyayo zake kama nilivyoeleza hapo juu.

Mzee Mengi alikuwa Mtanzania wa kwanza kuanzisha televisheni binafsi nchini, Independent Television (ITV). Kweli, hata katika eneo hili, Tanzania tayari ilikuwa na televisheni (Television Zanzibar-TVZ). Hii nayo ina historia yake muhimu. Ilikuwa televisheni ya kwanza ya rangi kuanzishwa  barani Afrika na mzee mwingine mwenye maono makali, Abeid Amaan Karume, Kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar na muasisi wa Muungano wa Tanzania. Lakini hii ilikuwa televisheni ya Serikali. Na isitoshe, matangazo yake yalikuwa hayasambai nchi nzima kiasi cha yalivyokuja kuwa matangazo ya ITV.

Mzee Mengi alikuwa Mtanzania wa kwanza na mpaka mauti yanamfikia anabakia Mtanzania pekee, kuwa na uthubutu wa kuanzisha na kumiliki vyombo vya habari nje ya Tanzania, katika masoko magumu kama vile Uganda na hasa Kenya.

Siasa za kuanzisha chombo cha habari katika nchi yoyote, iliyoendelea au inayoendelea, ni ngumu. Chombo cha habari ni uwanja wa kusambaza utamaduni na ni nguvu ya uongozi. Ni tofauti na kuanzisha kampuni ya kuuza matofali ambayo mwekezaji anaweza kuianzisha katika nchi yoyote kwa urahisi kabisa. Kwamba aliweza kupata leseni na vibali vya kufungua redio Uganda--na hasa Kenya, inayolinda sana soko lake kwa kila bidhaa-- si jambo dogo wala la mchezo, hata kidogo. Ni jambo kubwa sana.

Mzee Mengi hakuwa mwanzilishi katika eneo la magazeti. Wapo wengi waliomtangulia katika historia ya nchi yetu, wawe binafsi, umma au hata mashirika ya dini. Lakini himaya yake ya magazeti, ambayo wakati mmoja ilikuwa na magazeti manane, imetoa ajira kwa mamia ya watuy-- Watanzania na wasiokuwa Watanzania-- kuliko kampuni nyingine yoyote ya magazeti na vyombo vingine vya habari hapa nchini. Huo, si mchango mdogo, wala wa kubeza. Kwa hakika ni lazima liwe jambo la kutia hofu, kwa hata kufikiria tu, nini kinaweza kutokea kwa himaya hiyo baada ya kifo cha ghafla cha mzee wetu huyo.

Buriani ARM.

 Salva Rweyemamu, ni mwandishi wa habari wa zamani wa magazeti mbalimbali nchini.

Columnist: mwananchi.co.tz