Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Rais Uhuru Kenyatta amechagua kutokufa kwa presha

42348 Edo+kumwembe Rais Uhuru Kenyatta amechagua kutokufa kwa presha

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Huwa namfuatilia Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya na yale macho yake ya rangi nyekundu. Huku mtaani kwetu huwa tunaweza kujenga hisia kwamba kuna kitu anatumia. Ni kitu gani, au ni dawa gani hatuwezi kujua.

Baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu nimegundua urais ni mtamu lakini Uhuru hataki kufa kwa presha. Katika nchi iliyojaa ukabila, ufisadi, usomi mwingi, hasira za kisiasa, nadhani Uhuru amechagua kuishi bila ya presha.

Tabasamu usoni muda wote, hasira kando, ujuaji kando, ameamua kufaidi urais kisha aende zake. Ukitaka demokrasia anakupa. Ukimpinga anatabasamu, anakuminya kidogo kisha anaacha maisha yaendelee akiwa na tabasamu lake. Hataki shida na mtu. Anakuacha unatabasamu, na yeye anatabasamu.

Yeye na Raila Odinga wako poa tu kwa sasa. Yeye ndiye Rais, presha ya nini? Anamwita Ikulu wanakunywa mvinyo, wanateta, wanacheza Pool kisha Raila anaondoka zake. Hasira za nini? Yeye ndiye Rais. Amechagua kufanya anachotaka madarakani, kisha aufaidi urais, aondoke zake.

Huku katika demokrasia anajua kuchezesha karata zake. Anajua ana dola. Aliweza kuamuru uchaguzi urudiwe akijua kwamba atashinda. Alijua kama angeng’ang’ania ushindi wa uchaguzi wa awali basi mbu wangepiga sana kelele sikioni mwake asingefaidi utamu wa urais awamu ya pili.

Marais wengi wa Afrika wanapaswa kwenda kujifunza urais kwake. Urais unaweza kuwa kitu rahisi kama unaweka kutabasamu na wapinzani wako wa ndani na nje ya nchi. Mwishowe Rais anabaki kuwa Rais. Hii ndiyo kanuni ya kawaida anayoitumia Uhuru. Na kama kweli kuna kitu dawa anatumia basi anaitumia vyema.

Nchi za Afrika matatizo huwa hayaishi. Huwezi kuibuka shujaa hata kama unafanya makubwa kiasi gani. Wapinzani lazima watakughasi tu. Baadaye unaweza kufa kwa presha bila ya sababu. Nadhani Uhuru anatumia kanuni ya kufanya anachofikiri huku akicheka na kila mmoja.

Kenya ni nchi ngumu kuliko nchi nyingi za Afrika. Ina siasa za ajabu. Ina watu wasomi wakorofi. Wanatukana hadharani, wanajifanya wababe hadharani, lakini Uhuru bado anaiweza kwa sababu anajaribu kuufanya urais kuwa kazi rahisi. Anajua kucheza na wote. Wanaomsapoti na wanaompinga.

Mwanadamu aliyezaliwa katika tumbo la mwanamke siku zake za kuishi ni chache. Kwa nini ufe kwa presha?



Columnist: mwananchi.co.tz