Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Rais John Magufuli kanena, polisi ondoeni kibanzi

46491 Daniel Mjema

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mimi si mwepesi kumpongeza mtu, lakini kwa hili la Rais John Magufuli kuwaeleza ukweli polisi juu ya namna wanavyofanya uchunguzi wa jinai na kuacha maswali mengi sina budi kumpongeza.

Ni kweli, kama ni kuua nyoka, basi Rais amepiga fimbo kichwani kwa sababu katika siku za karibuni yapo matukio ambayo yameacha maswali mengi ambayo kumbe Rais anataka majibu kama tulivyo sisi.

Wengine wakaenda mbali na kudhani labda matendo yanayoendelea nchini na kigugumizi cha polisi kufikia hitimisho la upelelezi yana mkono wa wakubwa kumbe wala, Rais kawaanika peupe wachawi wetu.

Jeshi la Polisi ndio limepewa dhamana ya kuchunguza matukio ya uhalifu sambamba na vyombo vingine vya uchunguzi, lakini yapo matukio uchunguzi wake unatia shaka na kuacha maswali mengi.

Rais alizungumzia tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji (Mo)na namna polisi walivyochunguza kiasi hata raia wengine walifika mahali wakabeza kuwa ilikuwa ni maigizo.

Nilimsikiliza Rais kama ambavyo siku zote namsikiliza, namna anavyoongea kuonyesha uchungu na dhamira njema aliyonayo kwa Watanzania na nasema kwa hili ya Mo Dewji, hongera Rais.

“Najaribu kutoa dosari hizi ndogo ambazo zinalichafua Jeshi la Polisi. Mnatakiwa muelewe kuwa Watanzania sio wajinga. Wanafahamu na wanajua ku-analyse (kuchambua) mambo,” alisema.

Niwatolee mfano tu alipotekwa huyu Mohamed (Dewji) tulipata stori nyingi za maelezo. Walimteka aina fulani ya wazungu lakini ilipokuja kumalizika lile suala linaweka maswali mengi zaidi”.

Rais akaenda mbali na kueleza namna hadithi ya Mo Dewji kuachwa Gymkana usiku, watekaji kumuachia na silaha, na hata yaliyofuata baada ya kuonekana yanaacha mashaka mengi mno.

Amiri Jeshi Mkuu alihoji ukimya wa Jeshi la Polisi licha ya kuwaonyesha Watanzania hadi nyumba waliyodai ndimo alimofichwa Dewji na mtu aliyedaiwa ndiye aliyewasafirisha watekaji.

“Haya kama hata Watanzania watanyamaza, lakini mioyo yao inauma. Hizi dosari ndogondogo zinachafua Jeshi la Polisi,” Rais aliongea maneno ambayo naamini yaligusa mioyo ya Watanzania wengi.

Ni kutokana na mwenendo wao katika matukio ya kushambuliwa kwa risasi kwa Tundu Lissu na mengine ya aina hiyo, yanaifanya Serikali ibebeshwe lawama kwa kutokamatwa mshukiwa hata mmoja.

Tukio la kukamatwa kwa gari ambalo lilielezwa ni la Ikulu ya Kenya mjini Moshi, nalo linaacha maswali mengi kwa sababu limeisha kimyakimya, wala hatukuelezwa nani alikuwa anapelekewa.

Kwa staili hii ya upelelezi wa Jeshi letu kamwe hatuwezi kukomesha mitandao ya magenge ya kihalifu kama ya wizi wa magari, dawa za kulevya na wimbi la wahamiaji haramu wanaoingia nchini.

Rais amezungumza, huu ni wakati sasa wa Jeshi la Polisi kuondoa kibanzi jichoni na kujisafisha na kufanya kazi kwa weledi ili lionekane kweli ni jeshi la kulinda raia na mali zao.



Columnist: mwananchi.co.tz