Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Polisi watambue mitandao ya kijamii mdau dhidi ya uhalifu

23274 Mtandao+pic TanzaniaWeb

Mon, 22 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jicho hasi lina kawaida ya kutoona ukweli. Katika karne ya 16, mhubiri wa Kikristo na alama ya mwanzo ya U-protestant, William Tyndale aliingia kwenye mgogoro na Kanisa Katoliki alipoandika kitabu kinachoitwa “The Obedience of a Christian Man”, yaani ‘Utiifu wa Mkristo’.

Kitabu hicho kilikuwa na elimu kubwa kuhusu mafundisho ya Ukristo. Hata hivyo, uongozi wa Kanisa jijini Vatican haukuona yote mazuri ndani yake. Ulijikita kwenye eneo moja tu, kwamba Tyndale kupitia kitabu chake alichochea uasi dhidi ya Kanisa Katoliki.

Tyndale, raia wa Uingereza, ndiye binadamu wa kwanza duniani, kuandika Biblia ya Kiingereza kwa kutafsiri maandiko yaliyokuwepo kwa lugha za Kigiriki na Kiebrania. Hili pia lilikuwa chukizo kwa uongozi wa Vatican, kwa hoja kuwa kuiweka Biblia kwa Kiingereza kulipunguza au kupotosha maudhui.

Alichokisema Tyndale ni kwamba kwa kusoma Biblia ya Kiebrania, alibaini makosa mengi katika ile ya Kigiriki. Hivyo, Biblia ya Kiingereza iliyaweka maandiko kwa usahihi zaidi kutoka asili yake ya Kiebrania. Haikukubalika kwa Wakatoliki. Kwao Kiingereza hakikuwa lugha sahihi ya kuandikia neno la Mungu.

Mwisho Tyndale alikamatwa, akanyongwa na mwili wake kuchomwa moto. Baada ya kifo chake, dunia ikashuhudiwa maandiko ya Biblia yakisambaa duniani na kueleweka kwa urahisi kupitia Kiingereza. Baadaye lugha nyingine zikapokea. Hata sisi Waswahili tuna Biblia ya lugha yetu hadi za kilugha.

Hekima ndani yake

Hekima katika mfano wa Tyndale na adhabu ya kifo aliyohukumiwa na Kanisa ni kwamba si unachoamini wewe ndiyo sahihi kwa asilimia 100. Inawezekana unayepingana naye ana ukweli wenye nguvu zaidi. Ni vizuri kuwa na utaratibu wa kusikilizana. Si nia njema uliyonayo wewe ndiyo inafunika wengine wote. Unapaswa kutoa nafasi na wengine kudhihirisha nia zao. Kwa kufanya hivyo, unaweza kupata mafanikio zaidi. Kumbe sasa, Kanisa hilo lingemuona Tyndale ni mshirika wao katika kueneza neno la Mungu, mafanikio yangeweza kuwa makubwa.

Polisi na mitandao

Jeshi la Polisi Tanzania linapaswa kufahamu kwamba mitandao ya kijamii ni mshirika wa mapambano dhidi ya uhalifu. Kuitazama kwenye maeneo mawili tu ya uchochezi na kuingilia upelelezi si sawa. Linapaswa kuitumia vizuri mitandao na lijenge ushirikiano na jamii ya watumia mitandao.

Hivi sasa nchi imefunikwa na wingu la utekaji. Hili limeshika upana zaidi baada ya mfanyabiashara Mohammed Dewji (Mo) kutekwa Oktoba 11, mwaka huu. Hofu ni kubwa kwa Watanzania. Wanateseka zaidi kihisia kwa sababu inaonekana kama wahalifu wa vitendo vya utekaji wana maarifa mengi zaidi, kiasi kwamba vyombo vya nchi vinaambulia patupu.

Kwa tafsiri hiyo ni kwamba Jeshi la Polisi ambalo ni chombo kinachoratibu usalama wa raia na mali zao, linatakiwa kujenga ushirika mpana na wananchi hasa jumuiya ya watumia mitandao ya kijamii. Haipaswi kuendelea kuiona mitandao ni adui.

Katika mapambano dhidi ya uhalifu, wananchi wana nafasi kubwa ya kulisaidia Jeshi la Polisi kwa kuusema uhalifu, kuupigia kelele au kusaidia kuufichua. Yeyote ambaye kwa namna moja au nyingine anapaza sauti au anawanong’oneza polisi kuhusu uhalifu ni rafiki wa amani.

Anayepaza sauti kuhusu uhalifu hata katika njia ambazo si rasmi, hapaswi kutafsiriwa ni adui, bali ni mtu mwema mwenye kutamani kuona uhalifu unatokomezwa. Kumpuuza au kumwadhibu mtu wa aina hiyo si jambo jema kabisa.

Polisi wanaweza kuitumia mitandao ya kijamii kuukabili uhalifu. Wananchi wanapoona utekaji, waseme haraka kwamba mtu au watu fulani wametekwa. Hiyo isaidie habari kusambaa kwa haraka na polisi waweze kuukabili utekaji au uhalifu husika kwa kuweka mitego yao.

Mathalan, alipotekwa Mo Dewji, inaelezwa polisi walichelewa kupata taarifa rasmi. Hata hivyo, mitandaoni tayari habari zilishawahi kusambaa. Hapa polisi walitakiwa kujiona wapo nyuma na waiheshimu mitandao ya kijamii kwamba inaweza kuwafanya waende na kasi sahihi.

Mshangao wa sasa ni kuwa badala ya polisi kujiona wapo nyuma na wafanyie kazi kasoro ya kuzidiwa kasi na mitandao ya kijamii, wanaanza kuwaona watumia mitandao ni tatizo. Inaelezwa kwamba katika kamatakamata ya watu wenye kuhusishwa na tukio la Mo kutekwa, hata wale waliosambaza habari mitandaoni nao walishikiliwa.

Mtu aliyewahi kusambaza habari za Mo kutekwa anatakiwa kuonekana rafiki wa mapambano dhidi ya uhalifu wa kumteka mfanyabiashara huyo. Aliyepaza sauti kisha ikasambaa mitandaoni, aliwezesha nchi kupata taarifa kwa haraka. Huo ndiyo mchango wake.

Kama polisi wangeona analo la kuisaidia polisi, wangeweza kumwita na kumhoji ili aeleze kingine alichonacho kisha limwachie. Haipendezi mtu anayesambaza taarifa zenye kuufichua uhalifu aonekane mhalifu na hata kumlaza mahabusu siku tano. Hivi ni kuwaogopesha watu. Itawafanya siku nyingine wakiuona uhalifu wakae kimya. Hiyo itakuwa nafuu kwa wahalifu.

Zaidi, polisi kujitokeza mbele ya uso wa vyombo vya habari na kutaja jina la mtu kwamba wanamshikilia kwa sababu alisambaza mitandaoni habari za Mo kutekwa ni sawa na kumchongea kwa watekaji. Wao pengine walitaka polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vichelewe kupata taarifa. Wanaweza kumwona ana kiherehere hivyo kumdhuru. Hili lifikiriwe kwa mapana sana. Kwamba mtu wa kwanza angesema Mo katekwa, akaibuka wa pili na kubainisha aina ya gari ambalo watekaji walilitumia pamoja na rangi yake. Angetokeza mwingine mwenye kujua namba ya gari hilo kuiweka wazi. Polisi hawaoni kama wangekuwa wanarahisishiwa kazi? Polisi wahamasishe watumia mitandao kuusema uhalifu na si kuwatisha wakae kimya.

Teknolojia ifanywe rafiki

Ulimwengu unakua, teknolojia inashika hatamu. Polisi wanapaswa kuendana na kasi ya kiteknolojia. Wapanue njia za kunasa uhalifu kupitia mitandao. Waache kauli za kwamba “hatufanyii kazi taarifa za mitandaoni” wakati watoa taarifa wanakamatwa.

Kukataa mchango wa mitandao ya kijamii au kuwachukulia watoa maoni mitandaoni kuwa ni maadui, ni kutojitofautisha na yaliyompata mwanasayansi na mwanafalsafa wa Italia, Galileo Galilei, Karne ya 17.

Galilei baada ya kufanya utafiti wake wa kisayansi, alitoa ripoti kwamba dunia ni duara na hulizunguka Jua kutengeneza majira ya mwaka, vilevile hujizungusha kwenye mhimili wake ndipo usiku na mchana hupatikana.

Kwa ripoti hiyo, Galilei, alikiona cha mtemakuni kwa kusema dunia inazunguka. Papa Paul V aliyeliongoza Kanisa Katoliki kati ya Mei 16, 1605 mpaka Januari 28, 1621, aliamuru Galilei afungwe na atengwe kwa sababu alisema uongo.

Msimamo wa Galilei kuwa dunia inazunguka ulikuwa utovu wa nidhamu kwa Kanisa Katoliki wakati huo, kwani neno lilikuwa kwamba dunia haizunguki, isipokuwa Jua ndiyo huizunguka dunia.

Galilei aliugua msongo wa mawazo, akaishi maisha ya dhiki lakini msimamo wake kuwa dunia inazunguka ulibaki palepale. Alipofariki dunia Januari 8, 1642, aliyekuwa Mfalme wa Italia, Ferdinando II de’ Medici, alitamani kumzika Galilei jirani na kaburi la baba yake.

Hata hivyo, Kanisa Katoliki likiongozwa na Papa Urban VIII (aliyemrithi Papa Paul V) na mtoto wa dada yake, Kadinali Francesco Barberini walipinga Galilei kupewa heshima hiyo kwa madai kuwa alitenda dhambi kubwa kusema dunia inazunguka. Hivyo, Galilei alizikwa kwenye kichumba kidogo.

Baada ya miaka mingi kupita nani mkweli leo? Ni Galilei aliyeteswa hadi kufikwa na mauti akiwa na kihoro kwa sababu ya ugunduzi wake au viongozi wa kanisa nyakati hizo waliopingana na sayansi? Sasa hivi sote tunakubali kuwa dunia inalizunguka Jua.

Hii hapa inayoitwa leo, Galilei ni mwanasayansi anayeheshimika sana ulimwenguni kwa ugunduzi wake. Dunia inakiri kuwa alionewa, aliteswa kwa kufanya ugunduzi wa kimapinduzi kuhusu majira ya mwaka.

Polisi wasiwafanye watu wema wanaotumia mitandao ya kijamii kuwa akina Galilei. Waogope kuusema ukweli wanaoujua. Waunyamazie uhalifu. Wanapopaza sauti ya kuusema uhalifu, badala ya kuonekana washirika wa mapambano ya uhalifu, wanaadhibiwa kwa kuwekwa mahabusu. Galilei hakupongezwa kwa ugunduzi wake, aliadhibiwa.

Polisi wanayo nafasi pana ya kuanzisha urafiki na mitandao. Hata mitaani, polisi wanao wajibu wa kujenga uhusiano mwema na raia ili kupambana na uhalifu.

Vinginevyo watabaki nyuma au watachelewa sana kwenda na wakati. Haifai watumia mitandao ya kijamii wapuuzwe au waadhibiwe kwa nia zao njema kama Galilei na Tyndale.

Columnist: mwananchi.co.tz