Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Polisi, wanahabari wakae pamoja wajadili tofauti zao

13229 Pic+polisi TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Matukio ya Jeshi la Polisi na baadhi ya viongozi serikalini kuwashambulia na kuwatia mbaroni waandishi wa habari yameendelea kuibuka, licha ya suala hilo limekemewa mara nyingi na wadau wa habari.

Miongoni mwa matukio ambayo napenda kuyazungumzia ni yale yaliyotokea hivi karibuni likiwamo la mwandishi wa habari za michezo, Silas Mbise wa Wapo FM kushambuliwa na polisi wakati akitekeleza majukumu yake.

Tukio jingine ni la mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma kukamatwa na polisi akiwa wilayani Tarime mkoani Mara alikokwenda kuripoti habari za uchaguzi mdogo katika kata ya Turwa.

Matukio hayo yamewaibua wadau wa habari kulaani vitendo vinavyofanywa na polisi kupinga vitendo vya askari wake kuwashambulia, kuwapiga, kuwatia mbaroni na waandishi wa habari wanapotimiza majukumu yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari nchini (UTPC), Abubakar Karsan anasema vitendo hivyo vinamong’onyoa uhusiano kati ya vyombo vya habari na jeshi la polisi ambao ni wadau muhimu.

Amesema tabia za askari kuwapiga waandishi walishaziona siku nyingi tangu mwandishi wa kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi alipouawa na polisi wakati akitekeleza majukumu yake.

Alisema kati ya Februari 15, 2017 hadi Novemba 27 UTPC iliandika barua tatu ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuomba mkutano wa kujadiliana uhusiano na utendaji kati ya polisi na waandishi wa habari lakini barua zote hazijajibiwa.

Pengo la uhusiano wa wanahabari na polisi limeonekana kuongezeka kutoka na kauli ya mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP), Simon Sirro aliyoitoa wiki ilitopita jijini Arusha kuwa Mbise alishambuliwa na polisi kwa kutotii sheria, haiko sahihi.

Kwa mjibu wa Sirro, taarifa za awali walizonazo ni kwamba mwandishi huyo alikuwa mbishi kutii agizo na alimtendea uovu askari kwa kumkaba, hali iliyomfanya askari huyo kukasirika na kufikia hatua iliyoonekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni.

Siafikiani na kauli ya IGP kwa kuwa Katiba ya nchi sura ya 18, kila mtu anayo haki kupata taarifa ya habari. Wakati huohuo sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 (7)(1) kinamruhusu mwandishi wa habari kukusanya na kuchakata habari.

Kama polisi walijua huyo ni mwandishi wa habari na ameenda pale uwanjani kwa mujibu wa sheria, kwa nini wamzuie kutekeleza majukumu yake kama ambavyo wao walivyoenda kutekeleza majukumu yao?

Tunaweza kuondoa msuguano na migogoro baina ya waandishi wa habari na Jeshi la Polisi, endapo tu kila mmoja atatekeleza majukumu yake kwa mjibu wa sheria.

Isifikie hatua jeshi hilo ikawa linawatumia waandishi wa habari kwa masilahi ya Taifa pale wanapokuwa na jambo linalotakiwa kuifikia jamii, pia wanahabari wahakikishiwe kupata taarifa za jeshi hilo pale wanapozihitaji.

Tukumbuke kuwa pale ambapo hakuna fursa ya kukaa meza moja kuzungumza na kujadiliana masuala mbalimbali ya utendaji kazi katika kundi lolote au jamii yoyote, kinachofuata ni vurugu.

Hatupendi kuwe na vurugu bali tunataka kuwa na Taifa moja linalofanya kazi kwa pamoja na umoja bila mabishano, tusiruhusu hayo yatokee kila mmoja akubali kufanya kazi na mwenzake.

Columnist: mwananchi.co.tz